|
Mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran kati ya Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kwa upande mmoja, na Iran kwa upande mwingi, yalianza tena tarehe 23 huko Paris. Hayo ni mazungumzo ya mara ya tano tokea mwezi wa Desemba mwaka jana. Inasemekana kuwa mazungumzo hayo yalifanyika kwa muda wa saa 7, lakini hayakupata matokeo yoyote. Pande mbili zimeamua kuendelea tena katika siku za karibuni.
Kama ilivyokuwa kwenye mazungumzo ya zamani, mazungumzo hayo pia hayakupata matokeo yoyote. Lakini kwa sababu mazungumzo hayo yalifanyika baada ya Marekani kujisogeza karibu na msimamo wa nchi hizo tatu, mazingira ya mazungumzo hayo kwa ujumla yamebadilika kidogo. Si muda mrefu uliopita, Marekani kwa ghafla ilibadilisha msimamo wake na kutangaza kuwa haitapinga Iran kujiunga na Shirika la Biashara Duniani, WTO, na italegeza masharti ya kuiuzia Iran vipuri vya ndege za kiraia. Marekani imekuwa na "kauli moja" na Umoja wa Ulaya katika suala hilo.
Mabadiliko ya msimamo huo wa Marekani unatokana na hali ya kulazimika. Ingawa Marekani siku zote ilikuwa ikishutumu Iran kujaribu kuendeleza silaha za nyuklia kwa kisingizio cha matumizi ya amani, lakini haikupata ushahidi bayana. Marekani inaelewa kuwa msimamo wake mkali haukupata na hautapata matokeo yoyote. Kama hali hiyo ikiendelea hadhi yake ya kidiplomasia itaporomoka katika mapambano dhidi ya silaha za maangamizi makubwa. Kwa upande mwingine vita dhidi ya Iraq imekwisha izamisha Marekani katika matope, na haina uhakika wa kupata ushindi kama itaanzisha vita nyingine; Zaidi ya hayo, mazungumzo yaliyoanzishwa hivi karibuni kati ya Palestina na Israel na hali ya utatanishi ya Syria na Lebanon yanaisumbua. Na kitu muhimu zaidi ni kuwa Marekani lazima irekebishe uhusiano kati yake na Umoja wa Ulaya ulioharibika kutokana na vita ilivyoanzisha dhidi ya Iraq ili kuungwa mkono zaidi na nchi za Ulaya katika masuala ya kimataifa. Kutokana na fikra hizo, Marekani imerekebisha msimamo wake kuhusu suala la Iran.
Bila shaka nchi za Ufaransa, Uingereza na Ujerumani ambazo zimesakamwa katika mazungumzo na Iran zinafurahia mabadiliko hayo ya msimamo wa Marekani. Kwani zinaelewa fika kuwa bila ya msaada wa Marekani, haziwezi kutimiza ahadi zao kwa Iran kujiunga na WTO. Lakini kutokana na kuungwa mkono na Marekani sera za nchi hizo za "upole" zimekuwa na nguvu zaidi na zinaweza kuinua uwezo wa kuwa na masikilizano na Iran katika mazungumzo. Magazeti ya Ulaya yanaona kuwa ingawa nchi tatu hazitabadilisha sera zao za kutatua suala la nyuklia kwa njia ya amani lakini msimamo wao utakuwa mkali. Kwa mtazamo wa mbali, nchi hizo tatu zinalichukulia suala la nyuklia la Iran kama ni fursa nzuri ya kutimiza imani yao ya kidiplomasia. Kushinda ni lazima na kushindikana hapana!
Mstari wa mwisho wa Iran ni kushikilia haki yake ya kuendeleza na kutumia nishati ya nyuklia kiamani. Iran inaona kuwa hii ni haki iliyopo kwenye katiba ya kimataifa, na Iran inaungwa mkono na nchi nyingi wanachama wa Shirika la Nishati la Atomiki. Siku za karibuni, msimamo wa Russia unaogongana na msimamo wa Marekani unaitia moyo Iran katika suala hilo. Kama Iran inataka kuendeleza nishati ya nyuklia kwa "kujitegemea" lazima ifufue shughuli za kusafisha uranium, lazima ifahamu teknolojia yote ya nyuklia ikiwa ni pamoja na teknolojia ya kujenga kinu cha maji mazito. Iran kwa mara kadhaa inasisitiza kuwa haitaacha maslahi ya taifa kwa ajili ya kupata faida iliyoahidiwa na Marekani. Kabla ya mazungumzo hayo kufanyika, msemaji wa kamati ya usalama ya Iran alisema kuwa ama mazungumzo yafikie mkataba wa kukubali Iran kurudisha shughuli za kusafisha urnium, ama kusimamisha kabisa mazungumzo. Kiongozi wa ngazi ya juu wa Iran Seyyed Ali Khamenei tarehe 21 alitoa kauli ya kushtusha, akisema kuwa kama Marekani ikianzisha vita dhidi ya Iran kwa kisingizio cha suala la nyuklia, atavaa sare ya askari kushiriki na hata kufia vitani.
Vyombo vya habari vinaona kuwa mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran yamefikia kipindi muhimu. Lakini kutokana na hali ilivyo sasa, misimamo kati ya Marekani, Umoja wa Ulaya na Iran inatofautiana sana, sakata la mazungumzo litaendelea.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-24
|