Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-24 21:01:35    
China yaunga mkono mageuzi ya Umoja wa Mataifa

cri

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw.Kofi Annan tarehe 21 alitoa ripoti kuhusu mswada wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Mambo yaliyomo katika ripoti hiyo ni pamoja na usalama, maendeleo, haki za binadamu na mageuzi ya miundo ya Umoja huo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bwana Liu Jianchao alisema kuwa, China inaunga mkono kufanyika kwa mageuzi ya Umoja wa Mataifa, na kumsifu Bw. Annan kwa juhudi zake alizofanya katika kuhimiza uhusiano wa pande nyingi na demokrasia katika uhusiano wa kimataifa.

Bw. Liu Jianchao alisema:

"Ripoti hiyo imetoa mapendekezo mengi muhimu kuhusu masuali ya amani, maendeleo, haki za binadamu na mageuzi ya Umoja wa Mataifa. China siku zote inaunga mkono kuimarisha uwezo wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia matishio na changamoto za aina mbalimbali duniani kwa kufanya mageuzi yanayohitajika."

Ripoti hiyo ya mageuzi ni ripoti yenye mambo mengi zaidi kuliko ripoti nyingine tangu Umoja wa Mataifa uanzishwe. Mjumbe wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Bw. Hua Liming alisema kuwa, ripoti hiyo kimsingi imeonesha migongano miwili mikubwa iliyopo duniani, yaani mgongano kati ya umwamba, siasa ya mabavu na uhusiano wa pande nyingi na wenye demokrasia wa kimataifa, na mgongano wa kuimarika kwa hali ya nchi mbalimbali kutegemeana na kuongezeka kwa pengo kati ya matajiri na maskini uliosababishwa na utandawazi wa kiuchumi duniani. Hivyo ripoti hiyo inafuatilia sana maendeleo, umaskini na maradhi.

Lakini vyombo vya habari na wataalamu kadhaa wanaona kuwa, maneno yaliyotumiwa na kanuni zilizofuatwa kwenye ripoti hiyo zinaipendelea Marekani. Bw. Hua Liming alisema kuwa, hii imeonesha hali ya Marekani kutawala mambo ya kimataifa na Umoja wa Mataifa, wala siyo matakwa ya Annan pekee yake.

Ripoti hiyo inalitaka Baraza la Usalama kuafikiana kuhusu wakati gani na jinsi ya kutumia nguvu, ikipendekeza Baraza la Usalama kudhihirisha kanuni zitakazofuatwa wakati wa kupewa haki za kutumia nguvu ili kuzuia vitendo vya nchi kubwa. Ripoti hiyo pia inazitaka nchi mbalimbali kuafikiana kuhusu jinsi ya kubaini tafsiri sahihi kuhusu "ugaidi" kabla ya mwezi Septemba mwaka kesho, na kupitisha "mkataba wa kimataifa kuhusu ugaidi". Bw. Hua alisema kuwa, Marekani ilianzisha vita dhidi ya Iraq kwa kukwepa Umoja wa Mataifa, lakini katika suala la kupambana na ugaidi, Marekani bado inahitaji msaada wa Umoja huo. Bw. Li alisema:

"Ukweli wa mambo katika miaka miwili iliyopita umeonesha kuwa, japokuwa Marekani ni nchi kubwa kabisa duniani, lakini haiwezi kushughulikia mambo yote ya duniani peke yake. Umoja wa Mataifa bado ni jukwaa la kidiplomasia la pande nyingi, nchi moja kubwa haiwezi kushurutisha nia zake zote juu ya jumuiya ya kimataifa."

Sehemu ya mwisho ya ripoti hiyo ni kuhusu suala nyeti la upanuzi wa Baraza la Usalama. Kuna miswada miwili kuhusu suala hilo, wa kwanza ni kuongeza nchi 6 za ujumbe wa kudumu zisizokuwa na haki ya kupiga kura ya turufu na kuteua nchi 3 wasio wajumbe wa kudumu. Mswada wa pili ni, kuongeza nchi nane zenye hadhi ya nusu ujumbe wa kudumu na kipindi chao ni miaka minne na zinaweza kuendelea kugombea viti hivyo, pamoja na nchi moja isiyo mjumbe wa kudumu. Ripoti hiyo inaunga mkono kanuni nne zilizotolewa na kikundi cha watu mashuhuri kuhusu kupanuka kwa Baraza la Usalama, ambazo ni pamoja na kuzingatia kwanza nchi zilizotoa mchango mkubwa kwa Umoja wa Mataifa katika mambo ya kifedha, kijeshi na kidiplomasia, kuongeza viti vya nchi zinazoendelea ili kuimarisha uwakilishi wa baraza hilo.

Msemaji Liu Jianchao alisema kuwa, China inafanya utafiti kuhusu ripoti ya Annan na kufanya mawasiliano na mashauriano na pande mbalimbali, ili kusukuma mbele kwa pamoja mchakato wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Alisema kuwa, mageuzi ya Umoja wa Mataifa yanapaswa kufuata "katiba ya Umoja wa Mataifa", kuzingatia zaidi matakwa ya nchi zinazoendelea, kuonesha demokrasia katika nchi wanachama wote, na kujaribu kufikia makubaliano juu ya msingi wa kufanya mashauriano ya kutosha.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-24