|
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan tarehe 21 alitoa ripoti kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa, baada ya hapo, nchi kadha wa kadha duniani zimetoa dai moja baada ya nyingine kupinga Japan isiwe mjumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama.
Watu wenye busara wanaona kuwa, kama Japan haitatambua kwa usahihi historia yake, na haitaomba radhi kwa udhati kwa hatia ilizofanya, si rahisi kwake kuheshimiwa na kuaminiwa na nchi jirani zake za Asia hata dunia nzima, tena haina haki ya kuwa mjumbe wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Mageuzi ya baraza la usalama ni kazi muhimu zaidi katika mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Katika ripoti yake kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa, Bwana Kofi Annan alisisitiza kwa kudhihirisha kuwa, kufanikiwa au la kwa mageuzi ya Umoja wa Mataifa kutategemea mageuzi ya baraza la usalama. Ripoti yake imependekeza kuongezwa kwa idadi ya wajumbe wa baraza la usalama kutoka 15 hadi 24.
Katika miaka mingi iliyopita, Japan siku zote inafanya juhudi kutafuta hadhi yake ya nchi kubwa ya kisiasa. Kutokana na rekodi ya serikali ya Japan, haitaweza kuonesha vilivyo umuhimu wa Japan katika mambo ya dunia nzima na kuanzisha utaratibu mpya wa kimataifa, bila kuwa mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama. Mwaka 1994, kwenye mkutano wa 49 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Japan ilitoa ombi rasmi kuwa nchi ya kudumu ya baraza la usalama. Ili kutimiza lengo hilo, serikali ya Japan imefanya juhudi kubwa pamoja na "kucheza karata za kuhonga fedha". Hivi sasa Japan inajihisi kuwa inaweza kuwa mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama, hivyo tarehe 21 Bwana Annan alipotoa ripoti kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa, ndipo Japan iliposhirikisha India, Brazil na Ujerumani kutoa taarifa kukaribisha ripoti hiyo ya mageuzi, na kwa mara ya kwanza ilieleza wazi matumaini yake kuwa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa litapitisha azimio kuhusu ripoti ya mageuzi.
Lakini ndoto hiyo ya Japan imepingwa vikali na nchi jirani zake. Korea ya kaskazini inaona kuwa, kuipata Japan kiti cha ujumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama, ni jambo lisiloweza kuvumiliwa, hatia za Japan dhidi ya binadamu, na sera yake ya kufufua uzayuni pamoja na tishio lake dhidi ya nchi jirani, yanaonesha kuwa Japan imekiuka jukumu la Umoja wa Mataifa. Serikali ya Korea ya kusini pia imedhihirisha kuwa, Japan ikitaka kuwa mjumbe wa kudumu katika baraza la usalama, kwanza lazima ipate uaminifu wa nchi jirani zake, kwani walimwengu wana mashaka kuwa Japan ni nchi inayotafuta kikweli amani au siyo? Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bwana Kong Quan alidhihirisha kuwa, kama nchi moja ikitaka kufanya kazi yake ya kuwajibika katika mambo ya kimataifa, inapaswa kutambua kwa usahihi suala la historia yake. Uchunguzi uliofanywa kwa watu zaidi ya elfu 20 kwenye nchi 23 umeonesha kuwa, nchi jirani za Japan zinapinga vikali Japan kuwa mjumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, miongoni mwao asilimia 51 ya raia wa China wanapinga, asilimia 32 ya raia wa Korea ya kusini wanapinga, na asilimia10 ya raia wa Russia wanapinga. Hivi sasa watu wengi zaidi wanajiunga na harakati za mamilioni ya watu duniani kutia saini kupinga Japan kuwa mjumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama.
Vyombo vya habari vimeainisha kuwa, miaka 60 imepita tangu vita kubwa vya pili vya dunia vimalizike, Japan si kama tu haijikosoi kutokana na vitendo vyake ya mashambulizi vya zamani, bali inajaribu kurembusha historia yake ya aibu. Vyombo vya habari vya Korea ya kusini vimedhihirisha kuwa, watu wana mashaka kama Japan itaweza au la kufuata moyo wa Umoja wa Mataifa na kutoa mchango kwa jumuiya ya kimataifa kama itakuwa mjumbe wa kudumu kwenye baraza la usalama, ambapo azma yake kubwa itafichuliwa na itazidisha migongano ya kimataifa.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-24
|