Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan jana alitoa taarifa akionya kuwa, askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire ni wachache, na makundi mbalimbali nchini humo yanaharakisha kujiandaa kwa vita, hivyo hali nchini humo ina hatari ya kutodhibitiwa, na vita vya wenywe kwa wenyewe huenda vitatokea ambavyo vitawaletea watu wa Cote d'Ivoire na sehemu ya Afrika ya Magharibi hasara kubwa.
Mwezi Septemba mwaka 2002, jaribio la mapinduzi lilitokea nchini humo na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ingawa makundi mbalimbali yalisaini mkataba wa amani mwezi Januari mwaka 2003, na kukubali kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuunda serikali ya usuluhishi wa kitaifa, lakini kundi la upinzani "the New Forces" bado linakataa kuacha silaha, na kuendelea kudhibiti sehemu ya kaskazini wakati jeshi la serikali linapodhibiti sehemu ya kusini.
Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokea nchini Cote d'Ivoire, Ufaransa kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ilipeleka kikosi chenye askari 4000 nchini humo, baadaye Umoja wa Mataifa pia ulipeleka kikosi cha kulinda amani chenye askari 6000. Vikosi hivyo viwili vilikaa katika sehemu ya katikati ili kutenganisha kundi la "the New Forces" na jeshi la serikali.
Wachambuzi wanaona kuwa, upungufu wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ni sababu moja iliyosababisha hali nchini Cote d'Ivoire kutodhibitiwa. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kinashughulikia kulinda katika sehemu ya katikati, pia kinashughulikia kusimamia kuzuia usafirishaji wa silaha nchini Cote d'Ivoire na kulinda usalama wa wafanyakazi na idara za umoja huo, hivyo askari 6000 hawatoshi. Mwezi Desemba mwaka jana, Bw. Kofi Annan aliwahi kupendekeza kuongeza kikosi chenye askari 1200 kulinda usalama wa wafanyakazi na idara za umoja huo nchini humo, ili kuwawezesha askari 6000 wa sasa washughulikie kazi ya kulinda amani, lakini pendekezo hilo halikupitishwa kutokana na kuzuiliwa na Marekani.
Muda wa kulinda amani kwa kikosi cha Ufaransa utaisha mwanzoni mwa mwezi kesho. Rais Jacques Chirac aliwahi kusema kuwa, kama viongozi wa Afrika akiwemo Rais Laurent Gbagbo wa Cote d'Ivoire wanataka Ufaransa kuondoa kikosi chake, kikosi hicho kitarudi nchini Ufaransa kwa wakati. Wachambuzi wanaona kuwa, hivi sasa watu wanaopinga Ufaransa nchini Cote d'Ivoire ni wengi, Ufaransa huenda itaondoa kikosi chake, lakini kikosi hicho kikiondoka, nguvu ya kulinda amani itapungua, na hali nchini Cote d'Ivoire itakuwa mbaya zaidi.
Aidha, hivi sasa kundi la "the New Forces" linadhibiti kimsingi sehemu ya kaskazini kwa nguvu kubwa ya kijeshi, lengo lake la kujipatia uhuru ni wazi zaidi. Hivi karibuni kundi hilo mara nyingi lilitoa matangazo ya kuwa katika hali ya tahadhari katika pande zote likisema kuwa jeshi la serikali litalichukulia hatua za kijeshi, na kusema kuwa likishambuliwa halitachukua hatua ya kujilinda tu. Wachambuzi wanaona kuwa, ila kupata ushindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Okotoba mwaka huu, kundi hilo halitasalimisha silaha zake, la sivyo, litasukuma mbele uhuru wa sehemu ya kaskazini kwa nguvu za kijeshi.
Wakati huo huo, makundi mbalimbali katika sehemu ya kusini yanayounga mkono serikali pia yamechukua hatua nyingi. mwanzoni mwa mwezi huo, askari kadhaa wanaounga mkono serikali wanapita sehemu ya katikati na kuvishambulia vituo vya kijeshi vinavyodhibitiwa na kundi la "the New Forces". Ingawa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kilimaliza mgogoro huo, lakini makundi yanayounga mkono serikali yamesema kuwa, wataanzisha mashambulizi tena, na lengo la mwisho ni ukombozi wa nchi nzima.
Ili kutatua hali mbaya nchini humo kwa amani na kurejesha mchakato wa amani, Umoja wa Afrika, mashirika na nchi husika zimechukua hatua nyingi za kidiplomasia, lakini maendeleo ni kidogo. Wachambuzi wanaona kuwa, jumuiya ya kimataifa inahitaji kuchukua hatua nyingi zaidi ili kuzuia hali nchini Cote d'Ivoire isiwe mbaya zaidi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-25
|