Hivi karibuni hali ya usalama nchini Lebanon imekuwa mbaya. Mjini Beirut, mji mkuu wa Lebanon imetokea milipuko mingi mfululizo inayowalenga raia. Rais Emile Lahoud tarehe 27 aliahidi kuwa, serikali yake itafanya juhudi kadiri iwezavyo ili kuizuia milipuko isitokee tena na kulinda hali ya muungano na usalama wa nchi yake.
Rais Lahoud siku hiyo aliposhiriki kwenye sherehe ya siku ya Pasaka ya madhehebu ya Maronite alisema kuwa, watu wa Lebanon lazima washikamane na kushirikiana na serikali ili kuidhibiti hali nchini Lebanon. Askofu wa madhehebu ya Maronite Kadinali Nasrallah Sfeir alipokutana na rais Lahoud alisema kuwa, mikasa iliyotokea hivi karibuni imeonesha kuwa Lebanon sasa imekuwa na machaguo mawili, ama kushikamana au kufarakana. Alimsihi rais Lahoud na serikali ya Lebanon kufanya juhudi halisi ili kulinda usalama wa watu wa Lebanon.
Katika wiki iliyopita mikasa mitatu ya milipuko ilitokea mjini Beirut, na sasa hali ya usalama imekuwa mbaya. Usiku wa tarehe 26, mlipuko mkubwa ulitokea katika kiwanda cha uchapaji kilichoko katika sehemu ya Bouchrieh, kaskazini-mashariki ya Beirut, ambao ulisababisha watu wasiopungua 6 kujeruhiwa, na kuleta wasiwasi kwa Wakristo waliokuwa wanajiandaa kuadhimisha siku ya Pasaka. Kabla ya hapo, mnamo tarehe 19 na tarehe 24, milipuko ilitokea kwa nyakati tofauti katika sehemu iliyoko mashariki ya Beirut na mji wa Jounieh, ambayo ilisababisha vifo vya watu watatu na watu karibu 20 kujeruhiwa.
Milipuko hiyo imefuatiliwa na pande zote. Serikali ya Lebanon iliulaani mlipuko uliotokea tarehe 26 kuwa ni kusudio la kisiasa linalotaka kuharibu utulivu wa nchi. Kundi la wapinzani la Lebanon linaona kuwa, idara ya usalama ya Lebanon lazima iwajibike na mikasa hiyo, na mkuu wa idara hiyo lazima ajiuzulu. Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Bw. Adam Ereli alisema akitumai kuwa, serikali ya Lebanon itachukua hatua halisi ili kulinda usalama wa watu wa Lebanon, na kuchunguza chanzo cha mikasa hiyo mapema iwezekanavyo ili kuwaadhibu kisheria wazushaji wa mikasa hiyo. Pia alitaka uchaguzi wa bunge la Lebanon utakaofanyika mwezi Mei uwe huru na wa haki, na Syria iondoe kikamilifu jeshi lake kutoka Lebanon.
Milipuko hiyo mfululizo imewafanya watu wawe na wasiwasi na mwelekeo wa hali ya Lebanon. Milipuko hiyo mitatu yote iliwalenga waumini wa kawaida wa Kikristo, hivyo madhumuni yake ni kuchochea vurugu za kidini nchini Lebanon. Ni bayana kuwa wazushaji hao hawataki Lebanon iwe na utulivu na amani.
Migongano kati ya madhehebu mbalimbali nchini Lebanon iliwahi kusababisha vita wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa miaka 15. Sasa msingi wa maafikiano ya kitaifa bado ni dhaifu. Jeshi la Syria nchini Lebanon, ambalo lilifanya kazi muhimu katika mambo ya kumaliza vita wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon na kuituliza Lebanon, limeanza kuondoka baada ya kuuawa kwa Bw. Rafik Al-Hariri kutokana na shinikizo la nchi za magharibi. Hali hii inatoa mwanya kwa wale wanaotaka kuharibu utulivu wa Lebanon.
Katika kushughulikia mikasa ya kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw. Hariri na milipuko iliyotokea baadaye, serikali ya Lebanon inaonekana kuwa dhaifu na haikuchukua hatua halisi ili kuzuia hali isiwe mbaya zaidi. Nchi kubwa za magharibi kama Marekani zinatumia fursa hii kuingilia kati katika mambo ya Lebanon na kuishinikiza Syria kuondoa jeshi lake kutoka Lebanon. Nguvu hizo za nchini na nje zinaifanya hali ya Lebanon izidi kuwa na kutatanisha.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-28
|