Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-28 15:52:59    
Miaka mia moja ya maendeleo ya sekta ya kurekodi nchini China

cri
Mliyosikia ni sauti ya opera ya Kibeijing kutoka kwenye sahani ya santuri iliyorekodiwa zamani sana nchini China. Sahani hiyo inahifadhiwa na Mchina Bw. Liu Dingxun wa mji wa Tianjin. Meneja mkuu wa Shirika la Kurekodi la China Bw. Zhao Daxin alisema,

"Kutokana na kumbukumbu tulizo nazo, sahani ya zamani kabisa ya santuri nchini China, ni ya opera ya Kibeijing iliyoimbwa na mchezaji Sun Juxian, kwa hiyo tunaona sekta ya kurekodi nchini China ilianza kutoka kwa kurekodi sauti ya opera ya Kibeijing na kuendelea mpaka muziki wa kisasa."

Sekta ya kurekodi nchini China hapo mwanzo haikuwa kubwa, wakati huo mashirika ya nchi za nje yalikuja nchini kurekodi, kisha yalikwenda kutengeneza sahani nchi za nje. Kazi kamili ya kurekodi na kuchapisha sahani za santuri ilianza hasa kwenye miaka ya 30 ya karne iliyopita. Wakati huo kulikuwa na mashirika matatu yenye uwezo wa kurekodi na kutenteneza sahani laki kadhaa za opera ya Kibeijing na nyimbo. Nyimbo nyingi za wanamuziki wakubwa kama Nie Er na Xian Xinghai pamoja na nyimbo alizoimba mwimbaji nyota Zhou Xuan zote zilichapishwa katika miaka hiyo.

Baada ya Jamhuri ya Watu wa China kuasisiwa mwaka 1949, sekta ya kurekodi iliendelea haraka. Mwaka 1957 Shirika la Kurekodi la China lilianzishwa kwa msingi wa mashirika matatu ya zamani, na lilikuwa na ofisi nchi nzima. Hadi kufikia mwaka 1979, shirika hilo lilichapisha jumla ya aina 20 za michezo kwenye sahani milioni 260. Na baadaye shirika hilo liliwahi kuchapisha sahani nyembamba za plastiki, na mwishoni mwa karne iliyopita pia lilifanikiwa kuchapisha diski zenye sauti ya sterio.

Kuanzia mwaka 1979, kutokana na jinsi mageuzi yalivyoendelea, aina nyingine ya rekodi yaani kanda za audio zilitapakaa kila mahali nchini China, na redio-kaseti ilikuwa kitu cha fahari kilichotamaniwa na kila familia. Wakati huo Shirika la Kurekodi la Pasifiki lilianzishwa. Kuanzishwa kwa shirika hilo kulivunja ukiritimba wa Shirika la Kurekodi la China, na zama mpya ya audio na video ilianza.

Tokea hapo na baadaye, katika muda wa miaka 10, mashirika ya audio na video zaidi ya 300 yalijitokeza ambayo yalikuwa msingi imara wa kustawisha sekta ya kurekodi. Wakati huo diski za CD. LD. VCD na DVD zilianza kuingizwa kukoka nchi za nje, na China pia ilikuwa na uwezo wa kuchapisha, kwa hiyo "sahani za santuri" zilipitiwa na wakati. Mwaka jana, diski zilizotengenezwa nchini China zilifikia aina elfu 28 na mauzo yalifikia yuan bilioni 2.7. Diski hizo zimetoa mchango mkubwa katika kustawisha utamaduni na sanaa, kukidhi mahitaji ya wananchi ya maisha yao ya kiutamaduni na zimechangia maingiliao ya utamaduni na nchi za nje.

Mpiga filimbi ya mwanzi, Bw. Wang Tiequi alisema,

"diski zina faida nyingi, ambazo kwanza, zinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu, pili zinaweza kuwaburudisha watu wengi na tatu, zinasaidia maingiliano ya utamaduni na nchi za nje."

Lakini kwenye safari ya maendeleo ya audio na video pia kuna matatizo, nayo ni kuwa hali ya kurudufu diski kinyume cha sheria bado ipo tena ni vigumu kuikomesha. Kutokana na hali hiyo serikali ya China imechukuka hatua nyingi za kupambana na hali mbaya ya kurudufu diski, na kuingiza mitaji kutoka nchi za nje ilitatua tatizo la ukata. Mwenyekiti wa Shirikisho la Chila la Audio na Video Bw. Liu Guoxiong alisema,

"Katika miaka miwili ya karibuni tumeanza kushiriki kwenye maonesho na mauzo ya diski za audio na video katika nchi za nje, ingawa diski zetu katika maonesho zilikuwa sio nyingi, lakini tumeanza."

Bw. Liu alisema, kutokana na maendeleo ya sekta ya kurekodi, uzalishaji wa vifaa vya umeme vya nyumbani kwa familia pia unaendelea haraka, tuna uhakika kuwa miaka mia moja ijayo itakuwa kipindi kingine cha maendeleo makubwa zaidi ya sekta ya kurekodi nchini China.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-28