Utaratibu wa jamii wa Bishkek, mji mkuu wa Kyrgyzstan tarehe 27 unaelekea kutulia. Siku hiyo, ugomvi kati ya bunge la zamani na bunge jipya ulimalizika, bunge jipya lilianza kufanya kazi na wabunge 54 waliapishwa kushika madaraka.
Asubuhi ya siku hiyo, kikundi cha utekelezaji cha bunge la zamani na bunge jipya kilijadili masuala kuhusu uhalali wa bunge na kujiepusha na matatizo ya kisheria kutokana na uhalali huo, wabunge wapya na wa zamani walifikia makubaliano hatua kwa hatua. Msuluhishi wa wizara yenye nguvu ya nchi hiyo ambaye pia ni makamu wa rais wa zamani Bw. Feliks Kulov alisema kwenye mkutano wa utekelezaji kuwa watu wote wanapaswa kufanya kazi kulingana na katiba ya taifa, kipindi cha madaraka ya wabunge wa zamani ni miaka 5. Kama bunge la zamani litaendelea kufanya kazi, hali isiyotarajiwa itatokea katika nchi hiyo. Alionya kuwa, iwapo wabunge wa zamani hawatatii uamuzi wa tume kuu ya uchaguzi na kuwachochea watu waandamane mitaani, basi wizara yenye nguvu itachukua hatua za lazima zikiwemo kuwatia nguvuni watakaoleta matata.
Bunge jipya la Kyrgyzstan lilifanya mkutano wa dharura ambao ulimteua naibu mwenyekiti wa tume kuu ya uchaguzi Bw. Turgunaly Abdraimov kuwa mwenyekiti wa tume hiyo. Habari zinasema kuwa mwenyekiti wa zamani wa tume hiyo Bw. Sulaiman Imanbayev alijiuzulu kutokana na "afya". Baadaye mwenyekiti mpya alitangaza kuwa kuundwa kwa bunge jipya kunaambatana na katiba ya taifa na sheria ya uchaguzi, na mamlaka ya bunge la zamani yamemalizika. Wabunge wapya waliapishwa kushika madaraka kwenye mkutano huo na bunge jipya lilianza kufanya kazi. Kutokana na mpango, bunge jipya litachagua spika mpya tarehe 28.
Hivi sasa, utawala wa kundi la upinzani linaloongozwa na kaimu rais Bakiyev umeeleza kuunga mkono bunge jipya. Wachambuzi wanaona kuwa utawala mpya na bunge jipya zimefikia makubaliano na kutambuliana uhalali wa kila upande.
Suala kuhusu uhalali wa bunge la Kyrgyzstan ni jambo linaloamua utatuzi wa mgogoro wa kisiasa nchini humo, ambao unahusu uhalali wa uamuzi kuhusu uchaguzi wa rais mpya utakaofanyika tarehe 26 mwezi Juni.
Ugomvi kati ya bunge jipya na bunge la zamani ulipotulia, utulivu ulianza kurejea mjini Bishkek kama zamani.
Tarehe 27, kaimu rais Bakiyev alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Russia, alisema kuwa uhusiano kati ya Kyrgyzstan na Russia utaboreshwa na ana matumaini kuhusu jambo hilo. Bw Bakiyev alisisitiza kutovunja mikataba ya kimataifa inayohusika. Vituo vya kijeshi vya Russia na Marekani vitaendelea kuwepo nchini humo, na masuala yote yanatakiwa kutatuliwa kwa mujibu wa mikataba iliyosainiwa. Kabla ya siku hiyo, rais Vladmir Putin wa Russia alipozungumza na Bw Bakiyev kwa simu alieleza kuwa Russia itashirikiana na Kyrgyzstan katika kutuliza hali ya nchi hiyo, kutokana na ubinadamu na urafiki kati ya nchi hizo mbili.
Habari zinasema kuwa ujumbe unaoundwa na bunge na serikali ya Russia utawasili tarehe 30 mwezi huu mjini Bishkek na ujumbe wa jumuiya ya usalama ya Ulaya umewasili tarehe 27 alasiri mjini humo na kufanya usuluhishi wa kisiasa.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-28
|