Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-29 14:12:55    
Barua 0329

cri
Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483

Dubai, Falme za kiarabu, ametuletea barua akiandika makala yake isemayo "Kabila la watibet ni urithi mkubwa wa dunia". Makala hiyo inasema kuwa, ingawa watibet wanahesabika kama ni moja ya watu wa makabila madogo madogo nchini China, lakini umashuhuri wao kote duniani ndio umemfanya aandike barua hii. Mara nyingi anaposoma vitabu vya historia, majarida na makala mbalimbali kupitia Radio China Kimataifa, hakosi kukuta habari kuhusu historia, mila, tamaduni na desturi za kijadi za maisha ya kabila la watibet. Anasema jambo hili limemfanya yeye na wasikilizaji wetu wengine wafahamu mengi kuhusu kabila hilo.

Kwa kweli kuna sababu nyingi za kimsingi ambazo zimelifanya kabila la watibet lipate umashuhuri kote duniani, ikilinganishwa na makabila mengine madogomadogo nchini China.

Watibet ambao wanaishi katika mkoa unaojiendesha wa Tibet kusini magharibi mwa Jamhuri ya watu wa China, eneo lao la kimaumbile na mazingira yake ni ya kuvutia sana, kutokana na kuzungukwa na milima iliyojaa theluji, ikiwemo ile milima mashuhuri duniani ya Himalaya. Hata mji mkuu wa mkoa huo Lhasa upo katika uwanda wa milima hiyo na kuhesabiwa kuwa ni moja kati ya miji wanayoishi watu, ikiwa katika eneo la juu kabisa juu ya usawa wa bahari duniani na kupewa jina la "mji wa paa la dunia."

Pia kasri la Potala mjini Lhasa lilijengwa kwa utaalamu wa kipekee karne zilipopita, ambapo mwaka 1994 shirika la Elimu, Sayansi na utamaduni duniani UNESCO, lililiorodhesha kasri hilo kuwa miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia, utenzi mashuhuri wa Mfalme Caesar ambao ndio utenzi mrefu kuliko yote duniani ni baadhi tu ya mambo yaliyowapatia watibet umashuhuri mkubwa katika historia ya dunia.

Kutokana na hayo na mengine mengi, kabila la watibet nchini China limeonesha kuwa na umuhimu mkubwa katika urithi wa historia ya mwanadamu duniani, na ni wajibu wetu kuthamini na kutukuza nafasi ya watibet katika maendeleo ya mwanadamu.

Bwana Mbarouk pia anasema kuwa, anapenda kuchukua fursa hii kutoa pongezi zake za dhati kwa maadhimisho ya mwaka mpya wa kijadi wa China, ambapo mwaka huu umekuwa ni mwaka wa alama ya "Jogoo". Ni matumaini yake makubwa kwamba, wale wote waliosherehekea sikukuu hiyo mwezi Februari mwaka huu, alama hiyo ya "Jogoo" itakuwa ni ishara njema yenye mafanikio na baraka tele.

Anasema hata jamii za kiislamu mnamo tarehe 9 na 10 mwezi wa Februari mwaka huu, walishehekea kuingia mwaka mpya ya kiislamu wa "Hijivice" ambao unahesabiwa kuwa ni mwaka 1426 tangu pale Mtume Mohammad alipohama kutoka mji wa Makka na kwenda mji wa Madinah nchini Saudi Arabia ya leo. Kwa hivyo sote tulikuwa katika sherehe za kuadhimisha tarehe mpya za kalenda za kichina na kiislamu katika mwezi wa Februari mwaka huu, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kumpongeza na kumtakia kila la heri mwenzake.

Tunamshukuru sana Bwana Mbarouk ambaye mara kwa mara ametuletea barua akitoa maelezo yake baada ya kusikiliza vipindi vyetu, barua zake hutufurahisha na kututia moyo tufanye juhudi kubwa zaidi kuandaa vizuri vipindi vyetu ili wasikilizaji waridhike. Tunashukuru kwa salamu zako za heri ya mwaka mpya wa kichina, nasi tunakupa wewe na waislamu wengine salamu za heri ya mwaka mpya wa kiislamu.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff wa sanduku la posta 172 Bungoma Kenya anasema katika barua yake kuwa, amepokea barua yetu pamoja na kadi ambayo ina maelezo kuhusu utambulisho wa Tovuti ya idhaa ya Kiswahili.

Isitoshe kadi hiyo inawafahamisha wasikilizaji ratiba ya siku na vipindi vya Radio China kimataifa katika bara la Afrika. Hii itakuwa rahisi kwa wasikilizaji na hasa wasikilizaji wageni kufahamu vipindi vinasikika muda gani, anatushukuru sana. Shukurani nyingine ni kwa kadi za salamu, anasema kwani hiki ni chombo kizuri ambacho kila mara anakitumia kuwafikia wasikilizaji wengi. Anawatakia kila la heri watu wa China.

Na sisi pia tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff kwa barua aliyotuandikia na tunamtakia kila la heri, na kumtaka aendelee kusikiliza vipindi vyetu kwenye radio na mtandao wa internet. Pia tunapenda kuwakumbusha wasikilizaji wetu wote msisahau kutembelea tovuti ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, anuani yetu ni www.cri.com.cn chagua kiswahili.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-29