Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-30 14:02:19    
Serikali mpya ya Lebanon bado yakabiliwa na matatizo

cri

    Kutokana na kushindwa kulishawishi kundi la wapinzani kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa, waziri mkuu wa serikali ya uangalizi ya Lebanon Bw. Omr Karami tarehe 29 alitangaza kuwa atajiuzulu tena uwaziri mkuu.

    Mnamo tarehe 28, mwezi uliopita, kwenye mkutano maalum ulioandaliwa na bunge la Lebanon kujadili mkasa wa kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani Bw. Rafik Al-Hariri, Bw. Karami alitangaza ghafla kuwa watu wote katika serikali iliyoongozwa naye watajiuzulu. Baadaye, mnamo tarehe 10, mwezi Marchi rais Emile Lahoud alimteua tena Bw. Karami kuendesha serikali ya uangalizi na kuunda serikali mpya. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Lebanon, baada ya kujadiliana mara nyingi, tarehe 29 pande zote za Lebanon ziliafikiana kuhusu kuunda serikali mpya. Pande hizo zilikubali kumteua mtu anayekubaliwa na pande zote kuunda serikali ndogo ya maafikiano yenye watu 6 hadi 10 ili kuendesha na kusimamia uchaguzi wa bunge utakaofanyika mwezi Mei. Pande hizo zinaona kuwa, katika hali ya hivi sasa ya kutoweza kuunda serikali ya pamoja, jambo muhimu ni kuifanya serikali kuanza kazi tena haraka iwezekanavyo ili kutunga sheria ya uchaguzi na kusimamia uchaguzi. Kama uchaguzi wa bunge hautaweza kufanyika mwezi Mei, basi hali nchini Lebanon itakuwa haiwezi kudhibitiwa, na kutoa fursa kwa kundi la wapinzani kuongeza athari yake.

    Lakini Bw. Karami alisisitiza kuwa serikali mpya lazima ishirikishe vyama vyote likiwemo kundi la wapinzani, na kuweza kuwakilisha watu wa pande mbalimbali, ama sivyo haitaweza kudhibiti hali ya nchini humo, wala kuzuia mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na kuuawa kwa Bw. Hariri usiwe mbaya zaidi, au haiwezi kuendesha uchaguzi wa bunge wa mwezi Mei. Hivyo, alisema kuwa, hatapokea maoni ya kuunda serikali ndogo ya maafikiano, na kuamua kujiuzulu tena.

    Kabla ya hapo kundi la wapinzani la Lebanon lilieleza wazi kuwa, litashiriki kwenye serikali ikiwa masharti matatu yanakidhiwa, ambayo kwanza, kuunda kikundi cha uchunguzi cha kimataifa ili kufichua ukweli wa mkasa wa kuuawa kwa Bw. Hariri; pili, mkuu wa idara ya usalama ya Lebanon na maofisa wengine husika lazima wajiuzulu kutokana na kutofanya kazi vizuri katika kuchunguza mkasa huo; tatu, jeshi la Syria nchini Lebanon na wapelelezi lazima waondoke kikamilifu kutoka Lebanon kabla ya uchaguzi wa bunge kufanyika.

    Kutokana na mashinikizo kutoka kundi la wapinzani na pande nyingine, serikali ya Lebanon tarehe 26 ilikubali baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuunda kikundi cha uchunguzi cha kimataifa ili kufichua ukweli wa kuuawa kwa Bw. Hariri. Tarehe 29 mkuu wa idara ya upelelezi wa kijeshi ya Lebanon Bw. Raymond Azar alitangaza kuruhusiwa "kupumzika" kwa mwezi mmoja, baadaye huenda atatangaza kujiuzulu. Kwa upande wa Syria, imemaliza kipindi cha kwanza cha kuondoa jeshi kutoka Lebanon, na askari wa Syria nchini Lebanon wamepunguzwa kutoka 14,000 hadi 8,000.

    Wachambuzi wanasema kuwa, kujiuzulu tena kwa Bw. Karami kumeonesha kuwa, serikali mpya ya Lebanon bado inakabiliwa na matatizo, na mvutano kati ya serikali ya Lebanon na kundi la wapinzani huenda utaongezeka.

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-30