Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-30 20:33:27    
Elimu ya afya ya saikolojia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari yazidi kuzingatiwa nchini China

cri

Tukizungumzia afya ya kisaikoloja, watu wengi wataona kuwa suala hilo linahusiana na watu wazima tu, lakini kutokana na sababu mbalimbali, wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari pia wamekumbwa na matatizo ya kisaikolojia. Kama matatizo hayo hayataweza kutatuliwa kwa hatua mwafaka na kwa wakati, yanaweza kuathiri ukuaji wa wanafunzi hao katika siku za baadaye. Kutokana na sababu hiyo, hivi sasa idara za elimu za China zinazingatia sana kutoa mafunzo kuhusu afya ya kisaikolojia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Bi. Zhan Jing ni mwalimu wa shule ya sekondari huko Baotou katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ulioko kaskazini mwa China. kuanzia mwaka 1996, alianza kushughulikia kazi ya kutoa misaada ya kisaikolojia kwa wanafunzi, na hivi sasa amepata mbinu nzuri ya kuwasaidia wanafunzi kutatua matatizo ya kisaikolojia.

Alisema:

"kuna mwanafunzi mmoja anayeishi mbali na shule, baada ya kujiunga na shule yetu, alikuwa ni vigumu kwake kushirikiana na wanafunzi wengine. Baada ya kugundua tatizo lake, nilimwambia kuwa 'wewe huko peke yako, na mimi ni rafiki yako, katika siku za baadaye, ukiwa na matatizo, niambie tu.'"

Nusu mwaka baadaye, mwanafunzi huyo aliomba misaada mara nyingi kwa Bi. Zhan Jing. Bi. Zhan alimwambia kuwa kitu muhimu kabisa katika masomo na maisha ni kuwa na imani na kujiamini kuwa unaweza kushinda matatizo. Kutokana na msaada wa Bi. Zhan, mwanafunzi huyo hatimaye aliondokana na usumbufu huo na alipata maendeleo makubwa katika masomo yake.

Afya ya kisaikolojia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ilianza kuzingatiwa nchini China katika miaka ya karibuni. Kutokana na China kutekeleza sera ya uzazi wa mpango, wengi wa wanafunzi zaidi ya milioni 100 katika shule za msingi na sekondari nchini China ni mtoto mmoja wa pekee, ambaye hudekezwa kupita kiasi katika familia zao. Hali hiyo inawaletea matatizo kadhaa yakiwemo ubinafsi, uvumilivu dhaifu wa kisaikolojia na kuogopa kazi ngumu. Aidha, maendeleo ya kasi ya uchumi na jamii ya China yanaathiri sana mtazamo wa umma, wakiwemo wanafunzi hao wa shule za msingi na sekondari. Kutokana na hali hiyo, wizara ya elimu ya China inataka shule za msingi na sekondari kote nchini zizingatie afya ya kisaikolojia kwa wanafunzi na kutoa mafunzo ya afya ya kisaikolojia kwa njia mbalimbali.

Profesa wa chuo kikuu cha ualimu cha Beijing Gu Ming yuan aliainisha kuwa, elimu ya kisaikolojia ni msingi wa elimu zote. Alisema:

"kuhusu elimu ya afya ya kisaikolojia, lazima tuzingatie kuwasaidia wanafunzi kuwa na moyo wa kujiamini, kujiheshimu na kujikakamua, na kushughulikia kwa njia sahihi maumbile, jamii, watu wengine na binafsi."

Hivi sasa, suala la afya ya kisaikolojia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari linazingatiwa kote nchini. Kwa mfano, mji wa Hangzhou mkoani Zhejiang umeanzisha mafunzo ya kisaikolojia katika ngazi za mji, wilaya na shule. Ofisa wa kamati ya elimu ya mji huo Bw. Sun Yinong alieleza:

"tunazingatia sana kutoa elimu ya afya ya kisaikolojia. Hivi sasa, mji wa Hangzhou umeanzisha simu tatu maalum za kutoa mafunzo ya afya ya kisaikolojia, yaani simu maalum ya wanafunzi, simu maalum ya kuelekeza elimu ya familia na simu maalum ya walimu. Kuhusu masomo ya afya ya kisaikolojia shuleni, tunataka kila shule iweke zaidi ya vipindi vitatu katika kila muhula. pia tumechapisha vitabu vingi kuhusu suala hilo."

Shule ya sekondari ya tatu ya mji wa Foshan mkoani Guangdong inajulikana sana huko. Shule hiyo inazingatia sana mafunzo ya afya ya kisaikolojia, na imeanzisha klabu ya afya ya kisaikolojia na kuweka "wasaidizi maalum" kushughulikia matatizo ya kisaikolojia ya wanafunzi. Aidha, kuhusu hali kuwa wengi wa wanafunzi wanaokaribia kwenye mtihani wa kuingia chuo kikuu wanakabiliwa na shinikizo kubwa moyoni, shule hiyo imeweka mkazo katika kutoa mafunzo kwa wanafunzi hao, na kuwaalika wataalamu wa saikolojia kufanya mihadhara mikubwa kila mwaka, na kupeleka barua wazi kwa wanafunzi wanaokaribia kuhitimu ili kuwasaidia wakabiliane na mtihani katika hali ya kawaida.

Kuhusu hatua hizo zinazochukuliwa na shule, mwanafunzi Gao Liang aliyeingia chuo kikuu mwaka jana alisema:

"mazoezi ya kujilegeza yaliyoandaliwa na shule kabla ya mtihani wa kuingia chuo kikuu yalitusaidia sana kuondoa wasiwasi na kufanya mtihani huo katika hali ya kawaida."

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa msisikiliza maelezo kuhusu China kutoa elimu ya afya ya kisaikolojia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kipindi hiki cha elimu na afya yanaishia hapa kwa leo. Asanteni kwa kutusikiliza!

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-30