Bw. Paul Wolfowitz, mtu aliyependekezwa na rais Bush wa Marekani kuwa mgombea wa ukurugenzi wa benki ya dunia, tarehe 30 aliwasili Brussels na alikutana na waziri mkuu wa Luxenbourg, nchi mwenyekiti wa zamu ya Umoja wa Ulaya, Bw. Juncker na waziri wa fedha na waziri wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya. Baada ya mazungumzo, kwenye mkutano na waandishi wa habari Bw. Juncker alisema, nchi za Umoja wa Ulaya zitamwunga mkono Bw. Wolfowitz awe mkurugenzi wa benki ya dunia.
Kutokana na mwaliko wa kamati ya Umoja wa Ulaya Bw. Wolfowitz alitembelea Bruselss kabla ya bodi la wakurugenzi watendaji la benki ya dunia kumpigia kura tarehe 31. Safari hii ni juhudi ya Bw. Wolfowitz aliyofanya kwa ajili ya kuondoa wasiwasi wa Umoja wa Ulaya, na pia ni "mtihani wa uso kwa uso" wa Umoja wa Ulaya. Akiwa naibu waziri wa ulinzi wa Marekani Bw. Wolfowitz anachukuliwa kama ni mmoja wa waanzilishi wa vita vya Marekani dhidi ya Iraq, hata baadhi ya watu wanamwita "msanifu wa vita vya Iraq", naye pia ni msukumaji wa "sera ya upande mmoja" ya Marekani. Tarehe 16 mwezi huu rais Bush wa Marekani alimpendekeza kuwa mkurugenzi wa benki ya dunia, jambo hilo limesabaisha baadhi ya nchi ziwe na malalamiko, zinaona kuwa Bw. Wolfowitz sio mtaalamu wa kutatua matatizo ya umaskini, na hana uzoefu wa kuendeleza uchumi wa jumuiya ya kimataifa. Watu wengi wana wasiwasi kuwa benki ya dunia itakayoendeshwa naye itakuwa ni chombo cha kutumiwa na Marekani katika sera za Marekani.
Kabla ya ziara hiyo, mbele ya waandishi wa habari Bw. Wolfowitz aliwahi kusema kuwa hakika hatailazimisha benki ya dunia kwa sera za Marekani. Bw. Wolfowitz anafahamu moyoni kuwa kuna mabishano kuhusu yeye kuwa mkurugenzi lakini anatumai kuwa ataaminika baada ya kumfahamu zaidi. Baada ya kuzungumza na maofisa wa Umoja wa Ulaya Bw. Wolfowitz alisema, kuwasaidia watu kujiondoa katika umaskini ni jukumu kubwa la benki ya dunia, "Hakuna jambo lolote linalofurahisha zaidi kuliko kuwasaidia watu mahitaji yao" alisema.
Vyombo vya habari vinaona kuwa sababu ya nchi za Umoja wa Ulaya kumwunga mkono awe mkurugenzi, kabisa sio unyenyekevu wake bali hazitaki mgogoro utokee kati ya kando mbili za Atlantiki. Ingawa tofauti kati ya Ulaya na Marekani hazijatoweka kutokana na maoni tofauti ya vita vya Iraq, lakini kutokana na maslahi pande zote mbili zina hamu kubwa ya kupatana. Baada ya mazungumzo Bw. Juncker kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, nchi za Umoja wa Ulaya zinatumai mkurugenzi wa benki ya dunia atachukulia lengo la maendeleo ya milenia kuwa msingi wa kazi yake, na kuhakikisha watu wa Ulaya watakuwa na "uwakilishi mkubwa" katika maamuzi. Imefahamika kuwa Umoja wa Ulaya umependekeza kuongeza naibu mkurugenzi mmoja katika benki ya dunia na kumpendekeza Mfaransa, mwenyekiti wa "Klabu ya Paris" awe na wadhifa huo, ili kuongeza uzito katika maamuzi ya benki ya dunia na kumzuia Wolfowitz kwa kiasi fulani ili kukwepa benki ya dunia iwe jukwaa la Marekani kutekeleza "sera ya upande mmoja". Katika ziara yake, Bw. Wolfowitz hakuahidi wazi kuwa atamteua fulani awe naibu mkurugenzi wa benki ya dunia, lakini alisisitiza kwamba benki ya dunia ni "jumuyia ya kimataifa ya pande nyingi", na uwakilishi wa pande nyingi utaoneshwa katika safu ya vingozi wa juu.
Benki ya dunia ni moja ya mashirika chini ya Umoja wa Mataifa, madhumuni yake ni kuzisaidia nchi wanachama wa Umoja huo kuendeleza uchumi kwa njia ya mikopo. Marekani ni nchi yenye hisa nyingi katika benki hiyo, hisa zake zinachukua 16.41%. Kwa hiyo ni kawaida nafasi ya ukurugenzi iwe kwa Mmarekani na marais wa mashirika ya fedha yaliyo chini ya benki hiyo watakuwa watu wa Ulaya.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-31
|