Tarehe 30 mwezi Machi, waandishi wa habari kutoka ndani na nje ya Iran kiasi 30 walitembezwa na rais Khatami wa Iran katika sehemu ya Natanz palipofichwa zana za kusafisha uranium hapo zamani. Kitendo hicho kisicho cha kawaida kimefuatiliwa sana. Vyombo vya habari vinaona kuwa kitendo hicho kwa upande mmoja kinalenga kuufanya mpango wa nyuklia wa Iran uwe wazi na kufichua uzushi unaoishutumu Iran kuendeleza silaha za nyuklia, na kwa upande mwingine Iran inataka kuonesha nia yake ya kufufua shughuli zake za kusafisha uranium.
Kiwanda cha kusafisha uranium katika Natanz kinatiliwa sana mashaka. Mwezi Februali mwaka 2002 baada ya kuifanyia uchambuzi picha iliyopigwa kutoka setilaiti wanasayansi wa Taasisi ya Usalama wa Kimataifa ya Marekani walisema "Iran inajenga kiwanda cha nyuklia chini ya ardhi". Mwezi Februari mwaka 2003 katibu mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Bw. Al Baradei baada ya kufanya ukaguzi nchini Iran alidokeza kuwa ingawa kulikuwa na zana za nyuklia lakini shughuli zake "hazikuruka mpaka". Mwezi Oktoba mwaka huu, kutokana na mkataba kati ya Iran na nchi tatu za Ulaya, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, shughuli za kujaribu kusafisha uranium zilisimamishwa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa.
Ofisa wa Iran alieleza kuwa sababu ya kujenga kiwanda hicho chini ya ardhi ni kwa ajili ya "usalama" wake iwapo Marekani na Israel zitafanya mashambulizi, wala sio kabisa kwa ajili ya kuendeleza silaha za nyuklia. Ofisa huyo aliongeza kusema kuwa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wanakuja kukagua si chini ya mara moja kila mwezi. Rais Hatami alisema, hivi sasa Iran imesimamisha kwa muda tu shughuli nyeti za nyuklia, lakini anadhamiria kuanzisha tena shughuli zote za kusafisha uranium.
Mazungumzo kati ya Iran na nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza sasa yamefikia katika kipindi muhimu. Imefahamika kuwa tarehe 23 mwezi Machi kwenye mazungumzo ya mara ya tano Iran ilitoa pendekezo la maandishi la "kuzalisha uranium kwa kiwango kidogo". Magazeti barani Ulaya yanaona kuwa kwa kufikiria Umoja wa Ulaya umekuwa ukichunguza pendekezo leke, Iran inawatembeza waandishi katika sehemu hiyo, pamoja na kwamba mazungumzo ya raundi nyingine yataanza mwezi Aprili, Iran inatumai kuleta mazingira bora ili Umoja wa Ulaya ukubali pendekezo lake.
Siku za karibuni, msimamo wa Marekani kuhusu suala la nyuklia la Iran umekuwa laini, lakini kikanuni msimamo wake haukubadilika. Marekani inaamini kuwa Iran inafanya uchunguzi wa kutengeneza silaha za nyuklia kisirisiri, hali hiyo ikiwa pamoja na maingiliano yake na makudi mbalimbali ya ugaidi, suala la nyuklia la Iran limekuwa fundo la moyo kwa Marekani. Umoja wa Ulaya unatetea kutatua suala la nyuklia la Iran kwa mazungumzo, lakini kutokana na sababu fulani, kwa kweli hauna uhakika wa kufanikiwa. Licha ya hayo, teknolojia ya nyuklia ina pande mbili, moja ni kuendeleza silaha na nyingine ni kuiendeleza kwa ajili ya maendeleo ya uchumi, na mambo hayo mawili ni vigumu kuwekwa mpaka ulio wazi. Kutokana na mambo hayo mawili kuingiliana, suala la nyuklia la Iran ni la kutatanisha sana.
Kwa upande wa Iran, inaona kuwa ina haki kamili kuendeleza na kutumia nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kwa hiyo ina hoja za kutosha kisheria na huu ndio mstari wake wa mwisho katika mazungumzo. Kutokana na hayo hadi sasa sera zote aidha za upole au za ukali haziwezi kuifanya Iran iache haki yake ya kusafisha uranium. Isitoshe, nchi za Magharibi zinatumia vigezo viwili tofauti katika suala la kupinga kuenea kwa silaha za nyuklia, kwamba zinashinikiza na hata kuziwekea vikwazo "nchi zisizo za kidemokrasia", na kwa "nchi zilizo za kidemokrasia" zinaziachia huru. Hali hiyo hakika haitaweza kuridhisha watu duniani. Kitendo cha Iran cha kuwatembeza waandishi wa habari kwenye sehemu yenye zana za nyuklia kinalenga kusisitiza msimamo wake na mstari wake wa mwisho katika mazungumzo yanayofikia katika kipindi muhimu na kuondoa uzushi, na kujipatia uungaji mkono kimataifa.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-01
|