Tarehe 2 Aprili, matokeo ya uchaguzi mkuu wa bunge la Zimbabwe yalitangazwa, chama tawala cha nchi hiyo ZANU-PF kilipata ushindi kwa kupata theluthi mbili ya viti vya bunge. Lakini chama kikubwa kabisa cha upinzani cha nchi hiyo MDC kilidai kuwa, uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu, hivyo kilikataa kukubali matokeo yake. Uingereza,Marekani na jumuiya kadhaa za kimataifa pia zililaani kuwa, uchaguzi huo haukuwa wa haki. Kutokana na hali hiyo, serikali ya Zimbabwe imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha utulivu wa nchi hiyo.
Chama cha MDC kililaani kuwa, upigaji kura huo haukuwa wa haki, vyombo vya habari vya nchi hiyo vilivyodhibitiwa na chama tawala na vilikuwa na upendeleo dhahiri, chama tawala kiliwabembeleza wapiga kuwa kwa kuwapatia msaada wa chakula. Chama cha MDC kilitishia kuanzisha shughuli za kubatilisha matokeo ya uchaguzi. Kwa hivyo rais Mugabe wa Zimbabwe, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha ZANU-PF alisema kuwa, chama chake hakiwezi kurudi nyuma, uamuzi uliotolewa na wananchi hauwezi kubadilika. Alikionya chama cha MDC kukubali kushindwa, na kutozusha mgogoro.
Wachambuzi wanaona kuwa msimamo wa kutoshirikiana wa chama cha MDC hautaleta tishio kubwa kwa chama tawala, chama cha ZANU-PF kinaweza kudhibiti hali ya Zimbabwe.
Kwanza, chama cha MDC hakiwezi kulingana na chama cha ZANU-PF katika athari yake nchini humo na uwezo wa kuitawala nchi hiyo. Chama cha ZANU-PF kilichoitawala Zimbabwe kwa miaka 25 kilipata zaidi ya theluthi mbili ya viti vya bunge, matokeo hayo yameonesha heshima yake nchini humo. Lakini chama cha MDC kilichoundwa mwaka 1999 kinatambuliwa kuwa chama kisicho na mwongozo dhahiri wa kuendesha mambo. Japokuwa chama cha MDC kilidai kufanya mageuzi, lakini hakina mpango halisi wenye ufanisi, hivyo hakiwezi kuungwa mkono na umma wa wakazi wa nchi hiyo.
Pili, chama tawala cha Zimbabwe kimefanya maandalizi ya kuhakikisha utulivu na usalama wa nchi hiyo. Zimbabwe ni nchi yenye mfumo kamili wa kisheria. Ili kuhakikisha utulivu na usalama wa nchi hiyo baada ya upigaji kura, polisi wa Zimbabwe wamechukua hatua mwafaka kama vile kupiga marufuku wakazi kutembea na silaha, kuimarisha doria katika mitaa ya makazi, maduka na barabara muhimu. Ilipofika jana, hali ya sehemu mbalimbali nchini Zimbabwe ilikuwa shwari, hakutokea maandamano makubwa na mgogoro wa kutumia nguvu.
Tatu, japokuwa Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya na jumuiya kadhaa za kimataifa zinalaani kuwa , uchaguzi wa bunge wa Zimbabwe haukuwa wa haki, lakini umoja wa maendeleo ya kusini ya Afrika SADC, Umoja wa Afrika, Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na nchi nyingine jirani zote zimeeleza kuunga mkono matokeo ya uchaguzi. Ujumbe wa ukaguzi wa umoja wa SADC jana ulisema kuwa, uchaguzi huo ni wa amani na wa kuaminika, umeonesha matakwa ya wananchi. Nchi jirani zote zinatumai kuwa Zimbabwe itadumisha hali ya utulivu. Hii itakisaidia chama tawala cha Zimbabwe kupambana na shinikizo la nchi za magharibi. Marekani na Uingereza zinapaswa kuzingatia msimamo wa nchi jirani zake kabla ya kuchukua hatua dhidi ya Zimbabwe.
Kulingana na uchaguzi wa awamu iliyopita wa bunge la Zimbabwe ambao ulikumbwa na mgogoro mara kwa mara, upigaji kura wa bunge hilo ulifanyika katika hali ya amani. Wachambuzi wanaona kuwa, jambo hilo limeonesha kupevuka kisiasa kwa watu wa Zimbabwe. Inaaminika kuwa, watu wengi wa Zimbabwe watathamini hali ya utulivu ya nchi hiyo, kujishughulisha katika harakati ya kustawisha uchumi wa nchi wala siyo kuchagua mgongano wa kisiasa.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-04
|