Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-04 16:30:32    
Wasanii wa China washiriki mambo ya siasa

cri

Mkutano mkuu wa kila mwaka wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China ulifungwa siku chache zilizopita. Baraza hilo ni jumuiya ya ushirikiano wa siasa wa vyama vingi vya China, ambalo linawashirikisha wajumbe wa nyanja mbalimbali, na miongoni mwao wako wasanii wengi mashuhuri, wakiwa pamoja na wajumbe wengine wanashiriki mambo ya siasa kwa kutoa maoni na mapendekezo kuhusu mambo ya serikali.

Ushirikiano wa vyama vingi na mashauriano ya kisiasa ni mfumo unaoongozwa na Chama cha Kikomunisti cha China, huu ni mfumo wa kimsingi wa kisiasa wa China, na pia ni mfumo unaolingana kabisa na hali ilivyo ya China. Kutokana na baraza hilo la mashauriano ya kisiasa, Chama cha Kikomunisti cha China na serikali ya China vinashauriana vya kutosha na wajumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa.

Kwa mujibu wa katiba ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa, wajumbe wana haki ya kusimamia mambo ya serikali kwa njia mbalimbali na kuwasilisha maoni na matakwa ya nyanja na makabila mbalimbali. Kati ya njia hizo, iliyo bora na ya moja kwa moja ni kutoa mapendekezo mkutanoni kuhusu masuala yanayohusu wananchi moja kwa moja. Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafasihi la Mkoa wa Guanxi Bw. Lan Huaicheng ni mwandishi mkubwa, naye kwenye mkutano huo alitoa mapendekezo yake. Alisema, "Sababu yangu ya kufikiria suala la elimu ni kuwa serikali siku zote inasisitiza kustawisha elimu, lakini sera zilizopo sasa hazitufikishi mahali yanapotakiwa. Watoto wa vijijini hawawezi kuona mambo mengi, kwa hiyo wanashindwa kwa watoto wa mijini wanapochujwa katika mtihani wa kujiunga na vyuo vikuu na kupata ajira. Natumai kuwa serikali itatoa sera za kuwapa kipaumbele."

Mapendekezo ya wajumbe huwa yanashughulikiwa na idara maalumu za serikali, na idara hizo lazima zitoe ripoti kuhusu hali ilivyo ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa. Katika utelekezaji wa mapendekezo hayo, mambo yote husika yataoneshwa katika siasa na sera za serikali.

Kwenye mkutano wa kila mwaka wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa, masuala yanayofuatiliwa zaidi ni masuala ya kilimo, mambo ya vijijini, ya wakulima, mageuzi ya mashirika ya kiserikali, maendeleo ya vijijini yaende sambamba na mijini na ujenzi wa sheria. Mwimbaji mshuhuri wa China Dedema alikuja na pendekezo kuhusu sheria ya kuhifadhi mbuga za majani. Alisema, "Nimekuwa mjumbe wa Baraza hilo kwa miaka mitatu. Kutokana na mawasiliano yangu na wafugaji nafahamu kuwa wafugaji hawafahamu sana sheria kuhusu hifadhi ya mbuga za majani. Kwa hiyo kwenye mkutano nimetoa ushauri wa uenezi wa sheria ya hifadhi ya mbuga za majani miongoni mwa wafugaji. Ingawa suala hilo halihusiki na kazi yangu ya muziki, lakini nikiwa mjumbe wa Baraza hilo ni wajibu wangu kuwasilisha maoni ya wananchi."

Baraza la Mashauriano ya Kisiasa ni kama "chimbuko la akili". Nchini China kuna wajumbe ambao ni wataalamu wa nyanja mbalimbali, wanatoa mapendekezo yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na jamii.

Mjumbe Tan Wenjing ni mhariri wa Shirika la Uchapoishaji la Jieli. Bi. Tan Wenjing ni wa kabila la Wamaonan mkoani Guanxi. Alipoulizwa na waandishi wa habari alisema, "Nimefanya kazi ya uchapishaji kwa miaka 20, kitabu nilichochapisha 'nyimbo za kabila la Wamaonan' kimepata tuzo ya taifa. Nikiwa mjumbe wa Baraza nafahamu sana uzito wa heshima hiyo. Kutokana na usambazaji wa vitabu huku na huko naingiliana na watu wengi na kuelewa hali zao. Kwenye mkutano nimetoa mapendekezo mawili kuhusu namna ya kutunza mabwawa ya maji."

Mjumbe huyo alisema, kwa sababu wajumbe wanatoka kila pembe ya jamii na wanashughulika na aina tofauti za kazi, kwa hiyo wanaelewa hali ilivyo kwenye nyanja tofauti, mashauri yao ni msingi kwa serikali kutunga sera na sheria kisayansi. Ni sawa kusema kuwa katika nchi kubwa kama ya China baraza la mashauriano ya kisiasa ni muundo mzuri unaolingana na hali ya China ilivyo.

Kwenye mkutano wa mwaka huu, wajumbe kutoka nyanja ya usanii wanachukua asilimia 10 ya wajumbe wote, wajumbe hao wametoa mapendekezo yao kuhusu namna ya kuenzi utamaduni wa China na namna ya kuunganisha pamoja na utamaduni wa China na nchi za nje.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-04