Shirika la nishati duniani siku chache zilizopita lilitoa ripoti ya uchunguzi ikitoa mwito wa dharura kwa nchi zinazoagiza mafuta kuchukua hatua madhubuti kujitahidi kupunguza matumizi ya mafuta. Ripoti hiyo iitwayo "Kuokoa mafuta kwa dharura" itatangazwa rasmi tarehe 28 mwezi huu, itakuwa waraka wa kimsingi wa mkutano wa mwaka wa mawaziri wa shirika hilo unaotarajia kufanyika mwezi ujao kujadili namna ya kukabili suala la kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa.
Hivi karibuni, bei ya mafuta katika soko la kimataifa inapanda haraka, katika soko la New York bei ya mafuta imefikia dola za kimarekani 58 kwa pipa, ambayo imeweka rekodi mpya ya kihistoria ya bei za mafuta. Wataalamu wanachambua kuwa, sababu kuu za upandaji wa bei za mafuta ni kuwa, mwaka huu mahitaji ya mafuta yataongezeka kwa asilimia 2 kuliko mwaka jana, bei za mafuta katika soko la kimataifa huenda itaongezeka kufikia dola za kimarekani 105 kwa pipa.
Licha ya hayo, mambo mengine yanayosababisha ongezeko kubwa la bei za mafuta ni kuwa, mahitaji ya mafuta duniani yanaongezeka kwa kiwango kikubwa; hali ya vurugu ya kisiasa inaendelea katika sehemu muhimu zinazozalisha mafuta;na ni vigumu kupata nishati nyingine inayoweza kutumika badala ya mafuta katika muda unaokadiriwa.
Katika ripoti hiyo, shirika la nishati duniani linapendekeza kuchukua hatua mwafaka za kubana matumizi ya mafuta, kwa mfano kupiga marufuku baadhi ya magari kutoka nje katika siku zilizowekwa, kupunguza kwa kiwango kikubwa au kuondoa kabisa nauli ya zana za mawasiliano ya umma, kuhimiza kutumia gari kwa pamoja, kufupisha saa za kazi na kujitahidi kufanya kazi nyumbani.
Kwa mujibu wa takwimu, matumizi ya mafuta katika sekta ya uchukuzi ni kubwa sana, tena yanaongezeka kwa haraka. Kama hazitachukuliwa hatua za kubana matumizi ya mafuta, ifikapo mwaka 2030, matumizi ya mafuta katika sekta ya uchukuzi yatachukua asilimia 55 ya jumla ya uzalishaji. Ripoti hiyo imeona kuwa, ni afadhali tuanze kubana matumizi ya mafuta kabla ya kukumbwa na mgogoro wa mafuta.
Shirika la nishati duniani lilianzishwa mwaka 1974 baada ya kutokea mgogoro wa mafuta mwanzoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita. Majukumu yake mawili makubwa ni kusimamia usalama na utoaji wa bidhaa za mafuta za nchi wanachama, kuratibu akiba ya kimkakati ya mafuta ya mahitaji ya siku 90 ya nchi wanachama. Shirika hilo limepanga kuwa, kama kiasi cha utoaji wa mafuta duniani kinapungua kwa asilimia 7, yaani mapipa milioni 6 kwa siku, basi nchi zinazoagiza mafuta zinapaswa kuchukua sera ya dharura ya kubana matumizi ya mafuta. Kutokana na hali ya hivi sasa ya nishati, nchi wanachama zinapaswa kuchukua hatua husika wakati kiasi cha utoaji wa mafuta kinapungua kwa mapipa milioni moja au mbili kwa siku.
Vyombo kadhaa vya habari vya nchi za Ulaya vinaona kuwa, ripoti hiyo imeonesha wasiwasi wa shirika la nishati duniani kuhusu usalama wa utoaji wa mafuta duniani, upandaji wa bei za mafuta na athari mbaya dhidi ya uchumi wa duniani, pia inamaanisha kuwa, shirika hilo limeanza kurekebisha sera zake. Siku za usoni litafuatilia zaidi jinsi ya kubana matumizi ya nishati, wala siyo kusisitiza tu kuongeza uzalishaji wa mafuta.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-05
|