Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-05 15:40:54    
Maendeleo ya kasi ya sekta ya teknolojia ya kisasa ya mji wa Beijing

cri

Takwimu mpya zinaonesha kuwa pato kutokana na uzalishaji wa sekta ya teknolojia ya kisasa la mji wa Beijing kwa mwaka 2004, lilikaribia Yuan za Renminbi bilioni 40 zikiwa ni karibu 10% ya pato la Beijing. Hivi sasa bidhaa nyingi zimezalishwa kwa hakimiliki ya China, ambazo zimekuwa na nguvu kubwa ya ushindani kwenye masoko. Habari zinasema kuwa maendeleo hayo yalitokana na mazingira bora na sera za uungaji mkono za Beijing katika mitaji, teknolojia na wataalamu.

Kabla ya miaka zaidi ya 10 iliyopita, kulikuwa na mtaa mmoja wa Zhongguancun uliojulikana kwa uuzaji wa bidhaa za elektroniki katika wilaya ya Haidian, sehemu ya kaskazini magharibi ya Beijing. Wakati ule, shughuli muhimu za kampuni zilizoko kwenye mtaa huo zilikuwa ni kuunganisha vipuri vya elektroniki vya aina mbalimbali vilivyoagizwa kutoka nchi za nje na kisha kuwauzia watu. Lakini kampuni hizo hazikuwa na uwezo wa uvumbuzi. Lakini baada ya kuendelezwa kwa miaka zaidi ya 10, mtaa huo uliojulikana kwa biashara ya bidhaa za elektroniki umekuwa moja ya maeneo makubwa ya sayansi na teknolojia nchini. Kampuni nyingi zilizoko katika eneo hilo sasa zimeendelezwa kuwa na uwezo wa kufanya utafiti na uzalishaji zenye teknolojia ya kisasa. Hivi sasa bidhaa zinazozalishwa katika eneo hilo licha ya kuuzwa hapa nchini bali pia zinapendwa kwenye masoko ya nchi za nje.

Habari zinasema kuwa ili kuunga mkono maendeleo ya sekta ya uzalishaji ya teknolojia ya kisasa, Beijing imebuni sera za kuharakisha maendeleo ya sekta ya uzalishaji ya teknolojia ya kisasa zikiwa ni pamoja na kuhamasisha kampuni za nchini na za nchi za nje kujenga vituo vya utafiti mjini humo; kupunguza ushuru na kodi na kutoa mikopo nafuu ya serikali kwa kampuni za software na dawa.

Mjumbe wa kamati ya sayansi na teknolojia ya Beijing Bw. Li Shizhu alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa hatua hizo za serikali ya Beijing zimechangia maendeleo ya sekta ya uzalishaji ya teknolojia ya kisasa, hususan ya uzalishaji wenye hakimiliki za China yenyewe. Alisema,

"Beijing sasa imefikia hatua ya kuzalisha bidhaa kwa teknolojia ya kiwango cha juu yenye haki-miliki zake yenyewe, tofauti na hali ya hapo mwanzoni ambapo iliweza tu kuunganisha vipuri vilivyozalishwa nchi za nje. Katika miaka hiyo, Beijing imepiga hatua kubwa katika jitihada ya kuwa na haki-miliki zake yenyewe. Mfano mmoja ni kufanikiwa katika uvumbuzi wa teknolojia ya uzalishaji wa COMS chips ambazo zinahitajiwa katika upande wa mawimbi ya picha video zikiwemo kamera za teknolojia ya tarakimu na simu za mkononi."

Bw. Li alisema kuwa hapa Beijing kuna taasisi muhimu za utafiti na vituo vikuu vingi, hivyo ina nguvu kubwa ya utafiti wa sayansi, wataalamu wengi na mitaji mingi, ambavyo vimeanzisha mazingira bora kwa maendeleo ya sekta ya uzalishaji ya teknolojia ya kimaendeleo.

Simu za mikononi zilizozalishwa na kampuni ya Samsung ya Korea ya Kusini zinapendwa sana na vijana nchini, lakini teknolojia ya uzalishaji wa COMS chips za multimedia za picha, ambazo ni vipuri muhimu vya simu za kampuni hiyo, ilivumbuliwa ka kampuni moja ya elektroniki inayojulikana kwa jina la Nyota ya China iliyoko katika eneo la sayansi na teknolojia ya Zhongguancun. Katika kampuni hiyo waandishi wetu wa habari waliona COMS chips za aina nyingi kubwa na ndogo na zenye maumbo mbalimbali. Habari zinasema kuwa chips hizo zinauzwa sana katika masoko ya nchini na ya nchi za nje, hususan ni kuwa COMS chips za kuingiza picha katika kompyuta zimechukua nafasi ya zaidi ya 60% katika masoko ya dunia. Ingawa chips hizo zinaonekana ni ndogo sana na kutovutia macho baada ya kufungwa katika Video kamera, simu za mkono na kamera za tarakimu, lakini zinafanya kazi muhimu sana katika vitu hivyo.

Naibu mkurugenzi mkuu wa kampuni ya elektroniki ya Nyota ya China Bw. Zhang Hui alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa katika muda wa miaka mitano tangu kuanzishwa kwa kampuni yao, wamefanya utafiti na uvumbuzi wa kuzalisha COMS chips za aina mbalimbali zinazotumika katika multimedia. Aliongeza kuwa hivi sasa kampuni yao imekuwa na hataza zaidi ya 300. Alisema,

"Tangu mwanzoni tulizingatia hifadhi ya haki-miliki, kuinua kiwango cha teknolojia na kuongeza nguvu ya ushindani"

katika miaka ya karibuni serikali na eneo la sayansi na teknolojia ya Zhongguancun vinatekeleza sera nafuu ili kuvutia uwekezaji wa nchi za nje na wanafunzi wa China wanaosoma katika nchi za nje. Mjumbe wa kamati ya usimamizi wa eneo hilo bibi Zhao Mulan alisema,

"Pato la eneo la Zhongguancun lilichukua 13% ya pato la Beijing mwaka 2000, lakini lilichukua karibu 18% ya pato la Beijing katika mwaka jana."

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-05