Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-05 15:47:11    
Barua 0405

cri

Msikilizaji wetu Johari Ali Isa Milanzi sanduku la posta 1620, Tabora, Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anaomba tumweleze machache kuhusu Radio yetu. Kwanza anasema katika eneo analokaa yeye huko Tabora, hali ya usikivu wa matangazo si nzuri, hivyo anaomba Radio China iboreshe mtambo ili wasikilizaji waweze kuipata kwa urahisi na waisikie vizuri.

Kuhusu suala hilo, kila mara mnapotuarifu huwa tunatoa ripoti kwa idara husika ya radio yetu, wahusika wanafanya juhudi kurekebisha hali hiyo. Usikivu mbaya unatokana na sababu mbalimbali, wakati fulani mabadiliko ya hali ya hewa huwa ni sababu kubwa, tumeambiwa kuwa, katika siku za usoni, Radio China kimataifa itajenga kituo chake cha kurusha matangazo barani Afrika, ili kuboresha usikivu wa matangazo ya Radio China kimatafia, tunaomba wasikilizaji wetu mtuvumilie, tuna imani kuwa siku za usoni hali itakuwa nzuri.

Lingine analozungumzia ni kipindi cha salamu zenu, anasema anafurahia kuwepo kwa kipindi hicho, lakini pia anasema hakikidhi haja ya wasikilizaji kwani zinasomwa kadi 4 ama 5 tu na kwa masharti ya watu 6. Anapendekeza uongozi ujaribu kusikiliza malalamiko ya wasikilizaji na ikiwezekana mapendekezo yao yatekelezwe.

Wiki zilizopita tulijibu swali kama hili, na tulisema kuwa kutoka na muda mfupi tuliopangiwa, hatuwezi kusoma kadi nyingi katika kipindi hicho na kuacha habari na vipindi vingine. Katika siku zijazo, tukikubaliwa kuongeza muda wa vipindi vyetu, tutaongeza kwanza muda wa kipindi cha salamu zenu. Tunaomba wasikilizaji mtuelewe na mtambue ugumu tulionao katika kugawa muda wa vipindi. Kutokana na muda tuliopangiwa, Idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa kila siku inatangaza kwa muda mfupi sana, hatuwezi kusoma salamu zenu kwa muda mrefu na kuacha vipindi vingine. Pia tunapenda mfahamu kuwa mapendekezo yenu yote mnayotutumia, huwa tunayafikisha mahali panapohusika, mkumbuke kuwa wenye maamuzi ya mwisho kwenye mpango wa vipindi, ni wakuu wa redio na sio idhaa yetu, watakapopitisha sisi tutatekeleza haraka.

Bwana Johari milanzi pia anatoa shukurani kwa kuwatumia wasikilizaji maswali mbalimbali na anasema nao wanajitahidi kuyajibu, ila majibu yanachelewa sana kutoka, huwa wanasubiri majibu mpaka wanasahau. Pia anaomba na hili nalo tujaribu kuliangalia. Vilevile anasema yeye ni msikilizaji mpya kabisa wa Radio China, hii ndio mara yake ya pili kutuma barua. Anatoa pongezi kwa kuwatumia bahasha ambazo wanazituma bila kubandika stempu. Anasema hii ni radio pekee inayofanya hivi, anatoa tena pongezi. Anaomba awe mwanachama kamili, na anaomba tumtumie majarida yanayoelezea teknolojia mpya, kilimo, matibabu ya dawa za kienyeji na maendeleo kwa jumla. Mwisho anatuambia kuwa huko kwao mjini Tabora wameanzisha klabu yao ya watu 54 ya kutuma salamu inayoitwa unyanyembe salam club. Wanaomba tuwatumie bahasha kama tulizomtumia, kalenda na Nembo za radio China kimataifa.

Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Johari Milanzi, wewe na wasikilizaji wenzako wote mnakaribishwa kuwa wasikilizaji wa kudumu, ni matumaini yetu kuwa wanachama wa klabu yenu watasikiliza vipindi vyetu na kutuletea maoni na mapendekezo, ili kutusaidia tuongeze mvuto wa vipindi vyetu katika radio na tovuti yetu.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-05