Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-06 20:58:33    
Hali ya wasiwasi yatokea tena katika mchakato wa kisiasa wa Kyrgyzstan

cri

    Mkutano wa bunge la Kyrgyzstan uliopangwa kufanyika tarehe 5 umeahirishwa. Kwa mujibu wa mpango uliowekwa, suala la kujiuzulu kwa rais Askar Akayev lingejadiliwa kwenye mkutano huo.

    Rais Akayev wa Kyrgyzstan tarehe 4 huko Mosccow alisaini taarifa ya kujiuzulu kwa hiari. Kutokana na makubaliano kati ya ujumbe wa Kyrgyzstan na Akayev mkutano wa bunge la Kyrgyzstan utafanyika tarehe 5, ambapo utathibitisha na kupitisha taarifa ya Akayev, kupanga tarehe ya uchaguzi wa urais na kupitisha taarifa ya kutoa uhakikisho kwa rais wa zamani Akayev, ili kukomesha hali ya wasiwasi wa kisiasa nchini Kyrgyzstan. Lakini ilipofika tarehe 5, theluti mbili tu ya wabunge walihudhuria mkutano huo wa wajumbe wote. Kwa mujibu wa sheria ya Kyrgyzstan, taarifa ya kujiuzulu kwa rais ni sharti isomewe kwa wajumbe wote wa bunge, hivyo mkutano huo umeahirishwa hadi tarehe 6.

    Sababu ya kuahirishwa kwa mkutano huo ni wabunge kuwa na maoni tofauti kuhusu suala la kujiuzulu kwa rais Akayev. Baadhi ya wabunge walisema hawapokei ombi la kujiuzulu la rais Akayev, bali wanaona kuwa rais Akayev anapaswa kufikishwa bungeni na kuhukumiwa. Mjumbe Azimbek Beknazarov, ambaye pia ni kaimu mwendeshaji mkuu wa mashitaka, alisema kuwa kuna tofauti kati ya kulazimishwa kujiuzulu kwa rais na kupokea ombi lake la kujiuzulu kwa hiari. Ameona kuwa baada ya rais Akayev "kutoroka" kutoka nchini Kyrgyzstan, hana haki ya kujiuzulu. Maoni hayo ya Bw. Beknazarov yanaungwa mkono na baadhi ya wabunge, ambao ni wabunge wa kundi la upinzani la zamani.

    Kutokana na hali hiyo, rais Akayev tarehe 5 alipohojiwa huko Mosccow alisema kuwa kuahirishwa kwa mkutano wa bunge la Kyrgyzstan kunatokana na sababu za kisiasa na za kiufundi. Aliona, kwa mujibu wa katiba ya Kyrgyzstan na utaratibu wa sheria wa nchi karibu zote duniani, rais analazimishwa kujiuzulu anapokuwa na hatia ya kuhaini taifa au hatia nyingine kubwa, na yeye hana hatia ya aina hiyo. Alisema kuwa kujiuzulu kwake ni kwa ajili ya maslahi, utulivu na amani ya taifa, kurudisha utaratibu wa katiba na kuisaidia serikali ya hivi sasa kufanya uchaguzi wa urais kihalali. Alisema, kwa mujibu wa katiba ya Kyrgyzstan, bunge kukubali kujiuzulu kwake kunaambatana na maslahi ya serikali ya hivi sasa, ama sivyo, hali isiyo ya tulivu ya Kyrgyzstan itakuwa ya utatanishi zaidi. Mbunge mmoja Bw. Tashkul Kereksizov siku hiyo alisema, bado kuna uwezekano kuwa mkutano unaopangwa kufanyika tarehe 6 kuahirishwa tena kutokana na kutohudhuriwa na baadhi ya wabunge.

    Wachambuzi wamesema kuwa hali ya taarifa ya kujiuzulu kwa rais Akayev kutopitishwa kwenye bunge la Kyrgyzstan itaathiri utulivu wa nchi hiyo. Kwanza, hali hiyo itachelewesha uthibitishaji wa tarehe ya uchaguzi wa urais, na hali ya kutokuwa na rais mpya itakuwa kikwazo katika kurudisha hali ya kisiasa ya Kyrgyzstan kuwa ya kawaida. Pili, vitendo vya baadhi ya wabunge vimeonesha kuwa kuna maoni tofauti hata mgongano ndani ya kundi la upinzani, hali ambayo itaufanya mchakato wa kisiasa ya Kyrgyzstan ukwame. Kiongozi maarufu wa kundi la upinzani la Kyrgyzstan Bw. Feliks Kulov tarehe 5 alitangaza kuwa kama mahakama itathibitisha kuwa hana hatia, yeye atashiriki kwenye uchaguzi wa urais. Kitendo chake hicho kimedhihirisha mgongano kati yake na kaimu waziri mkuu Bw. Kurmanbek Bakiyev, na hali ya kisiasa ya Kyrgyzstan huenda itakuwa na vurugu. Tatu, tarehe 5 alfajiri, mkuu wa idara ya ufisadi ya wizara ya mambo ya ndani ya Kyrgyzstan Bw. Oran Aliyev aliuawa, tukio ambalo limeonesha kuwa hali ya usalama bado inakabiliana na changamoto, na hali ya wasiwasi ya kisiasa nchini Kyrgyzstan itaathiri juhudi za serikali ya hivi sasa ya nchi hiyo katika kuhakikisha usalama.

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-06