Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-07 15:54:22    
Mchakato wa ukarabati wa kisiasa nchini Iraq wapiga hatua nyingine kubwa

cri

Mkutano wa nne wa bunge la mpito la Iraq tarehe 6 ulimchagua kiongozi wa Chama cha Umoja wa Wazalendo cha Kurdistan Bw. Jalal Talabani kuwa rais wa Iraq, ulimchagua kiongozi wa madhehebu ya Shia Bw. Adel Abdul Mahdi ambaye pia ni waziri wa fedha wa sasa kuwa makamu wa kwanza wa rais, na kiongozi wa kundi la madhehebu ya Suni Bw. Ghazi al-Yawar ambaye pia alikuwa rais wa serikali ya mpito kuwa makamu wa pili wa rais. Mchakato wa ukarabati wa kisiasa nchini Iraq umepiga hatua nyingine kubwa.

Vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu vinasema kuwa, bunge la mpito la Iraq kuwachagua rais na makamu wa rais kumeleta fursa ya kusimamisha mzozo wa kisiasa kati ya makundi mbalimbali katika miezi miwili iliyopita, na kuondoa vikwazo kwa uchaguzi wa waziri mkuu mpya. Kwa mujibu wa katiba ya muda ya Iraq, tume ya rais itakayoundwa na rais na makamu wawili wa rais itamchagua mgombea wa waziri mkuu na kuunda baraza la mawaziri, na kuiwasilisha orodha ya baraza la mawaziri kwenye bunge la mpito na orodha hiyo itapitishwa kwa kupigwa kura. Kwa mujibu wa mpango, baada ya Bw. Jalal Talabani, Bw. Adel Abdul Mahdi na Bw. Ghazi al-Yawari kuapishwa tarehe 7, watamchagua kiongozi wa Chama cha Shirikisho la Umoja la Iraq (the United Iraqi Alliance) Bw. Ibrahim al-Jaafari kuwa mgombea wa waziri mkuu wa serikali ya mpito, ambaye atashughulikia kuunda baraza la mawaziri. Bw. al-Jaafari atajadiliana na makundi mbalimbali katika bunge ili kuunda baraza la mawaziri litakalokubaliwa na pande zote.

Wachambuzi wanaona kuwa, kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Chama cha Shirikisho la Umoja la Iraq na Chama cha Umoja wa Wazalendo cha Kurdistan kuhusu mgawanyo wa madaraka, cheo cha spika wa bunge kitashikwa na mtu wa madhehebu ya Suni, cheo cha urais kitashikwa na Mkurd, na cheo cha waziri mkuu kitashikwa na mtu wa madhehebu ya Shia. Kabla ya hapo, kutokana na matumaini ya vyama hivyo viwili, mbunge wa madhehebu ya Shia Bw. Hajim al-Hassani amechaguliwa kuwa spika wa bunge la mpito. Kwa sababu vyama hivyo viwili vinashika theluthi mbili ya viti katika bunge, kumpitisha mgombea wa waziri mkuu Bw. Ibrahim al-Jaafari na orodha ya baraza la mawaziri katika bunge hakutakuwa jambo gumu. Kuhusu mgawanyo wa vyeo katika baraza la mawaziri, pande mbili zilikubali kuwa, kati ya mawaziri 32, Chama cha Shirikisho la Umoja la Iraq kitapata viti 16, Chama cha Umoja wa Wazalendo cha Kurdistan kitapata viti 8, na shirikisho la vyama vya madhehebu ya Suni litapata viti 6, kundi la Turkmen na kundi la Kikristo kila moja litapata kiti kimoja. Na pande mbili pia zimeafikiana kimsingi kuhusu mgawanyo wa vyeo muhimu. Watu wa Chama cha Shirikisho la Umoja wa Iraq watashika vyeo vya mawaziri wa mambo ya ndani na fedha, watu wa Chama cha Umoja wa Wazalendo cha Kurdistan watashika vyeo vya mawaziri wa mambo ya nje na mafuta, na mtu wa madhehebu ya Suni atashika cheo cha waziri wa ulinzi.

Lakini si jambo rahisi serikali mpya kukubaliwa na pande zote. Mpango wa vyama viwili haujali kundi kubwa la tatu lililopata viti 40 katika bunge yaani kundi la vyama vya madhehebu ya Shia linaloongozwa na waziri mkuu wa serikali ya mpito Bw. Iyad Allawi. Bw. Allawi anapinga nguvu ya kidini kuingilia mambo ya kisiasa na kutoa athari kwenye kazi za serikali katika siku zijazo. Mapendekezo yake yanakwenda kinyume na Chama cha Shirikisho la Umoja wa Iraq ambacho kina uhusiano mkubwa na dini, pia hayaungwi mkono na Chama cha Umoja wa Wazalendo cha Kurdistan na kundi la vyama vya madhehebu ya Suni. Hivyo kundi linaloongozwa na Bw. Allawi kushiriki kwenye serikali mpya si jambo rahisi. Pili, vitendo vya Chama cha Shirikisho la Umoja wa Iraq na Chama cha Umoja wa Wazalendo cha Kurdistanna kujadiliana faraghani pia vimeyafanya makundi madogomadogo kwenye bunge likiwemo kundi la madhehebu ya Suni kutoweza kukubali mpango huo wa kuunda baraza la mawaziri. Kwa mfano, katika uchaguzi wa spika, Bw. Yawar hakukubali mgombea wa spika kutokana na kutoridhika na mpango huo. Tatu, kundi la madhehebu ya Shia pia halikubali kundi la madhehebu ya Suni na kundi la Wakurd kushika madaraka; Bw. Yawari aliyechaguliwa kuwa makamu wa rais wa serikali ya mpito anataka kuwapatia kundi la madhehebu ya Shia maslahi makubwa kwa kutumia madaraka yake katika tume ya rais; na vyama vya kundi la madhehebu ya Suni kikwemo Chama cha Kiislam cha Iraq ambacho hakikushiriki kwenye uchaguzi mkuu pia kinataka kupata fursa ya kushiriki kwenye mchakato wa kiasa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-07