Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-07 14:39:52    
Siku ya afya duniani yasisitiza kuwathamini kina mama na watoto

cri

Shirika la afya duniani WHO leo huko Geneva limetoa ripoti ya mwaka kuhusu afya ya duniani iitwayo "Mthamini kila mama na mtoto". Ripoti hiyo imeainisha hali ya afya ya kina mama wajawazito, watoto wachanga na watoto duniani, na kujaribu kuzihimiza serikali za nchi mbalimbali, jumuiya ya kimataifa, wataalamu na familia kufuatilia suala hilo kwa kufafanua upya suala la afya ya kina mama wajawazito, watoto wachanga na watoto. Ripoti hiyo pia imezitaka pande husika zichukue hatua kukuza huduma za matibabu na kinga kwa mama na watoto.

Tarehe 7 Aprili ni siku ya afya duniani, kauli mbiu ya mwaka huu ni kumthamini kila mama na mtoto. Kuanzia mwaka 1950, Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe 7 Aprili ya kila mwaka kuwa siku ya afya duniani, na kuchagua kauli mbiu kwa kila mwaka kuhusu afya ya umma. Lengo lake ni kuinua mwamko wa binadamu kuhusu suala la afya ili kuendeleza afya. Katika siku hiyo, nchi wanachama wa WHO zitafanya shughuli za aina mbalimbali kueneza ujuzi kuhusu afya ili kuinua hali ya afya ya binadamu.

Mwaka huu WHO inafuatilia zaidi suala la wanawake na watoto. Ripoti ya afya duniani ya mwaka huu imeainisha kuwa, mama na watoto ni msingi wa familia na jamii, watoto ni mustakabali wa jamii, ambapo mama ni walezi na dhamana ya watoto. Kama afya ya mama haiwezi kuhakikishwa, basi itakuwa ni vigumu kwa watoto kukua kwa afya.

Takwimu zinaonesha kuwa, kila mwaka wanawake laki 5 na elfu 30 duniani wanakufa kutokana na matatizo ya ujauzito, kujifungua au baada ya kujifungua, wanawake milioni 300 wanaugua kutokana na kupata uja uzito na kujifungua, na wengi wao wanaishi katika nchi zinazoendelea. Hivi sasa, katika nchi zinazoendelea, ujauzito na kujifungua ni mambo muhimu yanayosababisha vifo vya wanawake. Kila mwaka watoto wachanga milioni 136 wanazaliwa, lakini karibu robo moja ya watoto hao wanakufa muda mfupi tu baada ya kuzaliwa. Kila mwaka watoto milioni 11 wasiozidi umri wa miaka 5 wanakufa kutokana na magonjwa ambayo mengi yao yanaweza kuwepa ajali, utapiamlo na umaskini. Kutokana na "lengo la maendeleo la milenia" lililowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2000, jumuiya ya kimataifa inaahidi kupunguza robo tatu ya vifo vya wajawazito kabla ya mwaka 2015, na kupunguza theluthi mbili ya vifo vya watoto wachanga. Lakini ripoti hiyo inaona kuwa, japokuwa nchi kadhaa zinazoendelea zimefanikiwa kupunguza kiasi cha vifo vya mama na watoto, lakini kwa ujumla hivi sasa bado kuna tofauti kubwa katika kufikia lengo hilo.

Ripoti hiyo imezitaka serikali za nchi mbalimbali na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua mwafaka kuimarisha na kulinda afya na usalama wa kina mama na watoto, kuinua mwamko wa mama kuhusu ujuzi husika, kuwapatia kina mama na watoto huduma za kinga na tiba zinazohitajika. Kuziweka afya ya umma na huduma za jamii katika mfumo wa kitaifa wa maradhi na kinga na tiba, na suala la afya ya kina mama na watoto linatakiwa kufuatiliwa zaidi. Nchi zinazoendelea zinatakiwa kutenga fedha nyingi zaidi katika utoaji wa huduma za afya kwa mama na watoto, kuwaandaa madaktari, wakunga na wauguzi wengi zaidi wanaowahudumia mama na watoto wachanga. Wakati huo huo, ripoti hiyo pia imesisitiza kuwa, nchi zilizoendelea zinawajibika kuziunga mkono nchi zinazoendelea katika fedha, teknolojia, mafunzo ya msingi ya afya na sekta nyingine.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-07