Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-07 16:34:16    
Watu wa kabila la wamiao wanaopenda muziki na nguo za rangi

cri

Lusheng ni aina moja ya filimbi ya China inayopendwa na watu wa kabila la wamiao. Watu wengi wa kabila la wamiao wanaishi katika mikoa ya Guizhou, Guangxi na Yunnan kusini magharibi mwa China.

Katika vijiji vya wamiao, wavulana wakipiga muziki wa filimbi wasichana huwa hawawezi kujizuia kucheza ngoma. Watu wa kabila la wamiao hueleza hisia zao za furaha na huzuni kwa kupiga filimbi.

Lusheng ni ala iliyotengenezwa kwa mianzi, watu wa makabila mengi madogo waishio kusini mwa China wanapenda kupiga filimbi ya aina hiyo. Tofauti na makabila mengine, watu wa kabila la wamiao wanapopiga Lusheng wanapaswa kufuata utaratibu maalum. Msanii wa kabila la wamiao aliyepiga Lusheng kwa miaka mingi Bwana Tang Fei alifahamisha kuwa:

"Muziki wa Lusheng hupigwa katika wakati uliowekwa, yaani kila baada ya mavuno ya majira ya mpukutiko na wakati wa kusherehekea sikukuu na mwaka mpya. Kutokana na desturi hairuhusiwi kupiga filimbi baada ya mwezi wa Mei. Inasemekana kuwa, filimbi ikipigwa baada ya mwezi wa Mei, mimea ya nafaka mashambani haitakua vizuri."

Katika vijiji vya watu wa kabila la wamiao, kila filimbi inapopigwa, watoto kwa watu wazima hujipanga kwenye duara kucheza kwa kufuata sauti za muziki wa filimbi. Wanaposherehekea sikukuu muhimu, wapiga filimbi kumi kadhaa au mia kadhaa hupiga filimbi kwa pamoja, na umati mkubwa wa watu wanacheza, hali yake inakuwa ni ya furaha sana. Katika sikukuu ya jadi ya watu wa kabila la wamiao ya "nguo ya kushonwa kwa manyoya ya ndege ", utaweza kuona tamasha ya upigaji wa Lusheng.

"Sikukuu ya nguo ya kushonwa kwa manyoya ya ndege" hufanyika katika majira ya mchipuko. Wanaume kwa wanawake wa kabila la wamiao wanaojipamba maridadi wanamiminika kwenye mteremko wakipiga Lusheng na kucheza ngoma kwa furaha na shangwe.

Mavazi ya watu wa kabila la wamiao yanajulikana kwa rangi mbalimbali za kupendeza na mitindo mingi. Sikukuu huwa ni wakati kwa wasichana kuonesha mavazi yao maridadi na usanii wao wa kushona nguo. Msichana Wei Yanyan wa kabila la wamiao alifahamisha kuwa:

"Mavazi ni kama kitabu cha historia cha kabila la wamiao kinachovaliwa mwilini. Kabila la wamiao ni kabila lililohamahama, wakati wa kuhamia sehemu ya kusini, wanawake walishona historia kwenye mavazi na kutembea nayo hadi mbali. Kila walikoenda huenda pamoja na utamaduni wao."

Watu wa kabila la wamiao wanaopenda maumbile hushona picha za ndege, vipepeo, ng'ombe, dragoni, milima, mito na miti kwenye mavazi, wanasema kuwa, hizo ni ishara za heri na baraka. Rangi kuu ya mavazi ya kabila la wamiao ni zambarau na buluu, na sketi ni mavazi yenye umaalum zaidi wa kikabila. Sketi za wanawake hushonwa lesi za rangi nyekundu, buluu na zambarau, na hutundikwa tufe nyeupe zilizotengenezwa na nyuzi, tufe hizo zinaashiria manyoya ya ndege. Mapambo ya kichwani wasichana wanayovaa pia yana umaalum sana, katika utosi wa kofia yenye rangi ya fedha vinawekwa vitu vya mapambo vilivyotengenezwa kwa umbo la manyoya ya rangi nyekundu na buluu. Wasichana wa kabila la wamiao wanaonekana maridadi zaidi wakivaa kofia za aina hiyo.

Mkuu wa wilaya inayojiendesha ya kabila la wamiao ya Rongshui ya mkoa wa Guangxi Bw. Wei Mingshan alisema:

"Wilaya hiyo imesifiwa kuwa ni 'maskani ya sikukuu mia moja', ina sikukuu katika majira yote, desturi nyingi za kikabila zenye umaalum wake, huoneshwa katika wakati wa kusherehekea sikukuu za aina mbalimbali kama vile kupambanisha farasi na kupiga Lusheng."

Wilaya ya Rongshui iliyoko milimani kaskazini mwa mkoa wa Guangxi, inahifadhi vizuri mila na desturi za kikabila ambazo huwavutia watalii wengi. Maendeleo ya utalii yamebadilisha hali ya maisha ya wakazi wa huko. Kwa mfano, mapambo ya fedha yaliyoonesha utajiri sasa yamekuwa mapambo ya siku za kawaida ya wasichana. Tamasha la nyimbo na ngoma na upigaji wa Lusheng lililofanyika wakati wa sikukuu sasa limekuwa njia ya kuwakaribisha watalii. Mishono ya tarizi na mapambo ya fedha yamekuwa vitu vya sanaa vya kumbukumbu nzuri kabisa kwa watalii. Sanaa hizo si kama tu zimewapatia pato watu wa kabila la wamiao, bali pia zinawafahamisha watalii utamaduni wa kabila la wamiao.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-07