Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-08 15:59:29    
kwa nini bei ya mafuta duniani inapanda tena kwa haraka

cri

kwa kawaida, katika majira ya Spring, matumizi ya nishati ya mafuta huwa yanapungua, na bei ya mafuta katika soko la kimataifa pia inapungua. Lakini mwaka huu, bei ya mafuta imeendelea kuongezeka kuanzia mwezi Machi. Wataalamu wanaona kuwa, ongezeko hilo la bei ya mafuta linatokana na sababu nyingi ambazo haziwezi kuondolewa kwa urahisi katika muda mfupi.

Kwa msingi, bei ya bidhaa inaamuliwa na hali ya utoaji na mahitaji ya bidhaa hiyo sokoni. Kutokana na uchumi wa dunia kuendelea kuongezeka na uwezo wa uzalishaji wa mafuta wa nchi zinazouza mafuta kukaribia kikomo, uwiano wa utoaji na mahitaji ya mafuta duniani umeharibiwa.

Uchumi wa dunia unakadiriwa kuendelea kuongezeka kwa haraka kama mwaka jana. Kutokana na hali hiyo, mahitaji ya mafuta duniani yataongezeka kwa kiasi kikubwa. Hivi karibuni, shirika la nishati la kimataifa limeongeza mahitaji ya mafuta duniani kwa mwaka huu hadi kufika mapipa milioni 84.3. Marekani ikiwa ni nchi yenye matumizi makubwa kabisa ya nishati duniani, wizara ya nishati ya nchi hiyo hivi karibuni imetangaza kuwa, mahitaji ya nishati ya mafuta yameongezeka kwa asilimia 2 kuliko mwaka jana. Kwa ujumla, akiba ya mafuta asili ya nchi zilizoendelea imepungua lakini mahitaji yao ya nishati bado yanaendelea kuongezeka.

Kuhusu hali ya utoaji wa mafuta, uwezo wa uchimbaji wa mafuta wa nchi zinazozalisha mafuta na uwezo wa kusafisha mafuta duniani wote unakaribia kikomo. Hali hiyo imezidi kuimarisha matarajio ya ongezeko la bei ya mafuta sokoni. Hivyo, ingawa jumuiya ya OPEC iliongeza kikomo cha uzalishaji wa mafuta kuanzia mwezi Aprili, lakini juhudi hizo hazijasaidia kuzuia ongezeko la bei ya mafuta.

Aidha, vitendo vingi vya kubahatisha sokoni pia vimesukuma mbele ongezeko la bei ya mafuta. Hivi sasa, vitega uchumi vikubwa vya kubahatisha vimeingia kwenye soko la mafuta. Wataalamu wanaona kuwa, ongezeko la bei ya mafuta ya hivi sasa limeondokana kikamilifu na gharama za uzalishaji. Gharama ya uzalishaji wa mafuta kwa wastani ni dola 10 za kimarekani kwa kila pipa, lakini bei ya mafuta imefikia dola 60 za kimarekani. Kutokana na makadirio, hivi sasa, mahitaji ya mafuta duniani ni mapipa milioni 84 kwa siku, lakini kiasi cha biashara ya mafuta kimefikia mapipa milioni 120 hadi 160 kwa siku, kiasi cha ongezeko la bei kinachosababishwa na vitendo vya kubahatisha kimefikia dola 8 hadi 20 za kimarekani. Kutokana na utaratibu huo, soko la mafuta la dunia linalazimishwa kukabiliana na hatari na shinikizo zinazoletwa na vitendo hivyo.

Mwisho, vyanzo vyingine, vikiwemo hali ya vurugu kwenye sehemu ya Mashariki ya Kati, tishio la ugaidi dhidi ya miundo mbinu ya mafuta na kufifia kijiolojia kwa raslimali ya mafuta, vinasukuma mbele ongezeko la bei ya mafuta. Wataalamu wanaona kuwa, kipindi chenye bei ya chini ya mafuta kitamalizika, na bei ya mafuta itaendelea kushikilia kuwa kubwa katika muda mrefu ujao. Benki maarufu ya uwezekaji Goldman Sachs mwishoni mwa mwezi Machi ilikadiria kuwa, hivi sasa soko la mafuta duniani huenda limeingia kwenye mchakato wa ongezeko la bei, na bei ya mafuta ya kimataifa hatimaye inaweza kufikia dola 105 za kimarekani kwa pipa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-08