Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan Bw. Jalail Abbas Jilani tarehe 11 alisema kuwa, hali ya hivi sasa inaonesha kuwa, madhumuni ya kundi la Iraq la kumteka nyara ofisa wa ubalozi wa Pakistan nchini Iraq ni kupata fedha. Mpaka sasa mateka huyo yuko salama, na serikali ya Pakistan inafanya juhudi zote kumwokoa mateka huyo.
Habari zinasema kuwa, m-Pakistan huyo aliyetekwa nyara anaitwa Malik Muhammad Javed, ana umri wa miaka 46, na alikuwa amefanya kazi kwa miaka 6 kwenye ubalozi wa Pakistan nchini Iraq, na ni msaidizi wa ubalozi tu wala si mwanadiplomasia. Bw. Javed, alipotea usiku wa tarehe 9 baada ya kwenda kwenye msikiti ulioko karibu na makazi yake. Baada ya kupata habari kuhusu kupotea kwa mfanyakazi huyo, serikali ya Iraq ilitoa ahadi ya kutoa habari zote zinazohusika kuisaidia Pakistan kumtafuta. Tarehe 10 alasiri, wizara ya mambo ya nje ya Pakistan ilitoa taarifa ikithibitisha kuwa, Bw. Javed ametekwa nyara, na Kundi la Omar bin Khattab lilitangaza kumteka nyara Bw. Javed. Baada ya hapo, msemaji wa serikali ya Pakistan ambaye pia ni waziri wa habari Bw. Sheikh Rashid Ahmed aliitisha mkutano na waandishi wa habari huko Islamabad akilaani vikali tukio hilo, na kutaka wateka nyara wa Iraq wamwachie huru mateka huyo. Bw. Rahid alisema kuwa, wateka nyara waliwasiliana na serikali ya Pakistan, na kutoa madai kadhaa, lakini hakudokeza hali halisi. Pia alieleza kuwa, Pakistan haitaondoa maofisa wake kutoka ubalozi wake nchini Iraq, na wala haitafunga ubalozi nchini humo. Serikali ya Pakistan itafanya juhudi kadiri iwezekanavyo kumwokoa mfanyakazi huyo wa ubalozi aliyetekwa nyara.
Tarehe 11, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Pakistan Bw. Jilani kwenye mkutano na waandishi wa habari alisemea inawezekana kuwa utekaji nyara huo unadhamiria kupata fedha, lakini hali hiyo haijathibitishwa bila ya ushahidi wa kutosha. Lakini mpaka sasa mateka huyo bado yuko salama, na serikali ya Pakistan inafanya juhudi zote kumwokoa. Bw. Jilani alisema kuwa, kundi la Omar bin Khattab ni kundi lisilojulikana nchini Iraq. Bw. Javed aliyetekwa nyara anawasiliana na ofisa wa ubalozi, na walizungumza kwa simu tarehe 10 usiku. Waziri mkuu wa Pakistan Bw. Shaukat Aziz siku hiyo aliitisha mkutano maalum kujadili masuala kuhusu kumwokoa Bw. Javed. Mkutano huo uliamua kuwa, Pakisatn itatuma mjumbe maalum nchini Iraq kufanya majadiliano na serikali ya Iraq, ili kuhimiza Bw. Javed aachiwe huru mapema. Aidha, serikali ya Pakistan itawasiliana na chama cha kiislamu cha Iraq chenye athari kubwa, ili kupata misaada kutoka kwenye chama hicho katika uokoaji wa mateka.
Mpaka hivi sasa, makundi ya uhalifu ya Iraq yamewateka nyara wageni zaidi ya 200, madhumuni ya utekaji nyara ni kudai majeshi ya nchi za nje yaondoke kutoka Iraq au kupata fedha. Bw. Javed ni m-Pakistan wa nne kutekwa nyara nchini Iraq. Mwezi Julai mwaka jana, dereva wa Pakistan aliachiwa huru siku 8 baada ya kutekwa nyara, siku kadhaa baadaye, wa-Palestina wawili waliofanya kazi kwenye kampuni ya Kuwait walitekwaji nyara na kuuawa nchini Iraq. Watekaji nyara hao waliitaka serikali ya Pakistan kutopeleka askari nchini Iraq. Baada ya hapo, serikali ya Pakistan iliwataka wananchi wake wasifanye utalii nchini Iraq.
Pakistan ni mshirika muhimu wa Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi, lakini kuna migongano kati yao kuhusu suala la kupeleka jeshi nchini Iraq. Marekani imeitaka mara nyingi Pakistan ipeleke jeshi nchini Iraq, lakini kila mara Pakistan inakataa. Kutekwa nyara kwa ofisa wa ubalozi wa Pakistan kunaonesha kuwa, hali ya usalama nchini Iraq bado ni ya wasiwasi, na utekaji nyara unafanyika mara kwa mara. Namna ya kuboresha hali ya usalama ni changamoto muhimu kwa serikali ya mpito ya Iraq itakayoundwa hivi karibuni.
Idhaa ya Kiswahili 2005-04-12
|