Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-12 16:21:52    
Barua 0412

cri
Msikilizaji wetu Makoye Mazoya wa sanduku la posta 200 Magu Mwanza Tanzania ametuletea barua akianza kwa kutusalimu wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anatuarifu kuwa amepokea kalenda ya mwaka 2005 na bahasha ya kutumia barua ambayo imelipiwa, anatoa shukrani kwa zawadi nzuri, pia anatupongeza kwa kuandaa jarida dogo la daraja la urafiki ambalo litakuwa na mkusanyiko wa barua na makala, anasema analisubiri kwa hamu jarida hilo.

Yeye hana mengi, na anamalizia kwa kusema kuwa, mbali na kuwa msikilizaji wa Radio China Kimataifa, pia analipenda Taifa la China. Anaipenda China kutokana na uungaji mkono wake kwenye maswala ya sera ya kidiplomasia, kuishi kwa amani, kupinga umwamba, na kusaidia kueneza teknolojia kwenye nchi zinazoendelea. Anasema China ni mlinzi wa amani duniani, kwa hiyo yeye anaipenda China kwa moyo mmoja, na anauombea urafiki kati ya wachina na nchi zinazoendelea udumu milele

Msikilizaji wetu mwingine John Amwayi Atenya wa sanduku la posta 3448 Nakuru Kenya ametuletea barua akitusalimu wafanyakazi wa Radio China kimataifa, na kutoa shukurani kwa barua tuliyomtumia. Kwenye barua yake pia ana mapendekezo kuhusu kipindi cha salamu zenu. Anasema yeye ni mmoja wa wapenzi wa salamu, na salamu ni kitu kinachomfurahisha. Huwa anafurahi sana kusikia salamu zake zikisomwa au akisikia anasalimiwa na wasikilizaji wengine. Kama kuna uwezekano anaomba muda wa kipindi hicho uongezwe.

Anasema huko Kenya kuna watu wengi wanaotuma salamu ambao wanafanya kazi mbalimbali, baadhi yao ni waganga wa kienyeji, wengine ni marubani, wengine ni wahubiri, wengine ni mafundi wa nguo, na wengine ni mafundi seremala na wengine hawana hata ajira, lakini ni wapenzi wakubwa wa salamu. Kwa kupitia kipindi cha salamu watu wa hali mbalimbali wanaweza kufahamiana, anasema itakuwa vizuri zaidi kama muda wa kipindi hicho utaongezwa.

Kutokana na barua tunazopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu wengi, tumetambua kuwa wasikilizaji wetu wengi wanapenda sana kipindi cha salamu kutokana na desturi za barani Afrika. Tunapenda kuwaambia tena wasikilizaji wetu kuwa, malalamiko na mapendekezo yenu kuhusu kuongeza muda wa kipindi cha salamu zenu, tunayazingatia na tunayafikisha panapo husika. Kama tulivyoeleza katika kipindi kilichopita idara husika ikitupa ruhusa ya kuongeza muda katika vipindi vyetu siku zijazo, tutaongeza kwanza muda wa kipindi cha salamu zenu, tunaomba wasikilizaji wetu mtuvumilie.

Na msikilizaji wetu James Ambinda Warita ambaye barua zake huhifadhiwa na Malaki Ochieng Ochindo wa sanduku la posta 15090, Nakuru Kenya, naye katika barua yake anasema angelipenda kipindi cha salamu zenu kiongezwe muda wa kusoma kadi za wapenzi wa salamu. Pia anapendekeza kuwe na muziki wa kuwaburudisha mashabiki wakati tunaposoma kadi za wasikilizaji.

Pia anapendekeza tuwe na mwaliko kwa mashabiki kutembelea idhaa ya kiswahili ya RadioChina Kimataifa. Anasema hapo Kenya wasikilizaji wana uhuru wa kutembelea kituo cha matangazo cha KBC na kuonana na watangazaji wake ana kwa ana. Pia anasema lingekuwa jambo la busara kwa watangazaji wa Radio China kuwatembelea wasikilizaji na marafiki wa Radio China kimataifa katika mataifa mbalimbali duniani, ili wasikilizaji wafahamiane na watangazaji wao wa Radio China kimataifa uso kwa uso. Vile anasema kungekuwa na shindano la kumi bora kwa watu waliotuma kadi nyingi na wapewe zawadi, ili kuwe na wasikilizaji wengi.

Anasema tutakapochapisha jarida dogo wapenzi wa salamu wangependa wanaposoma jarida hilo, waone hata picha za watu wanaotoa maoni. Kwa hiyo anapendekeza kuwa kwenye jarida hilo ziwepo picha za wasikilizaji. Anasema yeye analisubiri kwa hamu jarida hilo, na atafurahi sana kama atafanikiwa kusoma jarida hilo.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu James Ambinda Warita kwa maoni yake na mapendekezo yake kuhusu kuvutia wasikilizaji wengi zaidi. Mapendekezo yako yametusaidia, na kuhusu jarida usiwe na wasiwasi, endelea kusikiliza matangazo yetu na litakapokuwa tayari tutawafahamisha wasikilizaji wetu, jarida hilo tunaliandaa kwa ajili yenu.

Msikilizaji wetu Oscar J. Saulo wa sanduku la posta 227 Mbeya Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, ana mambo mengi sana yanayomfurahisha kutokana na ushirikiano na Radio China kimataifa katika mawasiliano ya barua. Pia anafurahia matangazo ya Radio China kimataifa ambayo huko Mbeya yanawafikia vizuri, anashukuru sana na anatuunga mkono tuendelee hivyo hivyo.

Pia amefurahi kuwa mwaka huu wa 2005 tutatoa jarida dogo la Daraja la urafiki, kazi hii ni nzuri sana kwani ana matumaini kuwa gazeti hilo litaimarisha mawasiliano kati ya Radio China kimataifa na wasikilizaji wake. Anatusihi tuendelee na kazi hiyo, anasema sasa anaanda barua nyingine yenye hadithi nzuri sana anatumai kuwa sisi na wasikilizaji tutaifurahia. Pia anafurahi sana kama tutamtumia barua.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-12