Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-12 16:25:45    
Umoja wa Mataifa wasisitiza kutunza dunia, maskani pekee ya binadamu

cri

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika yake yametoa ripoti kadhaa mfululizo zikieleza tishio kubwa kwa mfumo wa ikolojia kutokana na shughuli za binadamu, zikitaka nchi zote ziamke na kuchukua hatua za kutunza dunia, maskani pekee ya binadamu.

Kikundi cha wataalamu wa mabadiliko ya hali ya hewa katika Umoja wa Mataifa tarehe 11 kilitoa ripoti yenye kichwa cha habari "Kutunza Tabaka la Ozoni na Mfumo wa Hali ya Hewa". Ripoti hiyo inasema kuwa jumuyia ya kimataifa imepunguza utoaji wa chlorofluorocarbonides, CFC, hewa inayoharibu tabaka la ozoni, na kutumia kitu kingine mbadala cha kemikali, lakini kitu hiki kinachotumika kinachangia joto la hewa. Kwa makadirio, ripoti hiyo inasema, kama hali hiyo ikiendelea bila kuchukuliwa hatua, hadi mwaka 2015 kitu hiki mbadala kitaongezeka mara mbili hadi mara 3 ndani ya hewa. Ripoti inaitaka jumuyia ya kimataifa ichukue hatua nyingine za kupunguza nusu ya CFC na kitu hicho mbadala kabla ya mwaka 2015 ili kulinda tabaka la ozoni na kudhibiti mabadiliko ya joto duniani.

Kabla ya hapo, ripoti tatu za uchunguzi zilizotolewa mwezi Machi pia zilieleza tatizo la mabadiliko mabaya ya mazingira na mfumo wa ikolojia. Ripoti ya kwanza yenye kichwa cha habari "Tathmini ya Mfumo wa Ikolojia wa Milenia" ni ripoti iliyoandaliwa na wataalamu 1300 kutoka nchi 95 kwa kudhaminiwa na Umoja wa Mataifa. Ripoti hiyo inasema kuwa 60% ya mifumo ya ikolojia inayohudumia binadamu na viumbe wengine imebadilika na kuwa mibaya, na baadhi imeharibika kabisa ambayo haiwezi kufufuka tena. Viumbe duniani wamepata hasara kubwa na hasara hiyo haifidiki. Asilimia 10 hadi 30 ya wanyama wanyonyao maziwa, ndege na wanyama wanaoishi katika maji na nchi kavu wametoweka kabisa. Ripoti inaonya kuwa hivi sasa maji na maliasili ya uvuvi haziwezi kutosheleza mahitaji ya binadamu, achilia mbali mahitaji katika siku za baadaye. Katika muda wa miaka 50 ijayo matokeo yatakuwa mabaya zaidi kutokana na mabadiliko ya mazingira, na yataathiri vibaya maisha ya binadamu. Ripoti inataka nchi zote zichukue hatua ili kupunguza kasi ya mabadiliko hayo wakati mahitaji ya binadamu yanaendelea kuongezeka.

Ripoti ya pili ilitolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO. Ripoti hiyo inasema kuwa mazingira ya kuhakikisha maisha ya binadamu yamekuwa mabaya kwa kiasi kikubwa, kama vile maji matamu, hewa safi na tabia ya hewa iliyotulia, na mazingira hayo mabaya yamekuwa yakiathiri afya ya binadamu, na athari hiyo itakuwa mbaya zaidi katika muda wa miaka 50 ijayo. Ripoti inaomba kuwa kutokana na uharibifu wa mfumo wa ikolojia, magonjwa kama kipindupindu na malaria yanaenea zaidi na magonjwa ya aina mpya yatatokea. Kutokana na mabadiliko mabaya ya mfumo wa ikolojia, lengo la maendeleo ya milenia la Umoja wa Mataifa litakuwa vigumu kutimizwa. Jumuyia ya kimataifa inapaswa ipate njia ya kuzuia na kudhibiti mabadiliko hayo ya mfumo wa ikolojia au ipate njia mpya ya kulinda afya ya binadamu.

Ripoti ya tatu ni "Tabia ya Hewa, Maji na Maendeleo Endelevu". Hii ni ripoti iliyotolewa na shirika la metolojia duniani. Ripoti inasema, hewa kabonda oksaid inayotolewa na shughuli za biandamu imeongezeka kwa 33% kuliko kipindi cha historia ya Mapinduzi ya Viwanda. Tokea karne iliyopita, mabadiliko ya joto yamekuwa ya haraka kuliko kipindi chochote katika miaka elfu kadhaa iliyopita. Matokeo hayo ya mabadiliko ya joto yamesababisha barafu katika ncha mbili za kusini na kaskazini za dunia kuyeyuka kwa kasi isiyowahi kutokea; na uso wa bahari umeinuka kwa milimita 2 kila mwaka katika karne iliyopita; viumbe wa nusu ya kizio cha kaskazini wameanza kuhamia kaskazini zaidi au kwenye ardhi iliyoinuka zaidi. Katika nusu ya kizio cha kaskazini mvua inanyesha kwa 10% zaidi kwa mwaka na mafuriko yanatokea mara nyingi barani Ulaya, lakini huku, ukame mkali unatokea barani Afrika. Maafa yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa yameongezeka mara tatu katika muda wa miaka 30. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1992 hadi 2001 watu walioathiriwa na maafa ya maumbile walifikia milioni 200.

Binadamu wana dunia moja tu. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alisema, ni kutokana na kufahamu tu hali ilivyo ya mazingira, ndipo binadamu wanapoweza kufanya uamuzi wa namna ya kupambana nayo, na ni kutokana na kutilia maanani tu maliasili ndipo binadamu wanapoweza kujenga mustakbali mzuri. Iwapo binadamu wasipochukua hatua za haraka kuboresha mazingira yanayokuwa yakibadilika kuwa mabaya, watalipa gharama kubwa kwa ajili ya mabadiliko hayo. Amezitaka serikali zote na wataalamu waimarishe maingiliano na kutoa mchango kwa ajili ya kutunza dunia na mazingira tunayoishi binadamu.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-12