Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-14 16:25:37    
Mkutano wa kimataifa wa kuichangia Sudan misaada yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 4.5

cri

Mkutano wa kimataifa wa kuipatia Sudan misaada ulifungwa tarehe 12 huko Oslo, mji mkuu wa Norway. Pande mbalimbali zilizohudhuria mkutano huo ziliahidi kuchangia dola za kimarekani bilioni 4.5 kwa ajili ya ukarabati na maendeleo ya Sudan baada ya vita kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2007. Kiasi hicho kimezidi kile cha dola za kimarekani bilioni 3.6 kilichodakiriwa hapo awali.

Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni waziri wa maendeleo na utoaji misaada wa Norway Bi. Hilde Johnson alieleza baada ya mkutano huo kuwa, ingawa bajeti za utoaji misaada za nchi mbalimbali zilipungua sana baada ya kuzipatia misaada nchi zilizokumbwa na maafa ya tsunami yaliyotokea mwaka jana katika bahari ya Hindi, lakini fedha zilizozidi kuliko zilivyokadiriwa zinaonesha hamu za nchi mbalimbali kuusaidia ukarabati wa Sudan. Fedha hizo zitatumika katika kuunga mkono mkataba wa amani wa Sudan uliosainiwa mwezi Januari mwaka huu, hasa kwenye kuondoa njaa, kuwasaidia wakimbizi katika ukarabati wa makazi yao na kujenga shule, barabara na hospitali.

Mkutano huo ulifunguliwa tarehe 11 na uliwashirikisha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan, malkia wa Norway Bi. Sonja, makamu wa kwanza wa rais wa Sudan Bw. Ali Taha, kiongozi wa kundi la upinzani la zamani SPLM Bw. John Garang na wajumbe kutoka nchi na jumuiya za kimataifa zipatazo 60. China na nchi kadhaa za kiarabu pia zimepeleka wajumbe kuhudhuria mkutano huo.

Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Bw. Robert Zoellick alieleza kwenye mkutano kuwa Marekani inaahidi kuipatia Sudan msaada wa dola za kimarekani karibu bilioni 1.7 katika muda wa miaka mitatu ijayo, Umoja wa Ulaya dola za kimarekani milioni 765, Uingereza dola za kimarekani milioni 545, Norway dola za kimarekani milioni 250, na Uholanzi itachangia dola za kimarekani milioni 220.

Kutokana na kuwa bado kuna mambo yasiyotulia nchini Sudan, mkutano huo pia ulijadili uwezekano wa kupeleka jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa katika sehemu hiyo katika siku za baadaye, ili kuhakikisha misaada hiyo inawafikia watu wa Sudan wanaohitaji misaada. Balozi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Sudan Bw. Jan Pronk na wengine walizisifu nchi mbalimbali zitoe michango kwa juhudi, huku wakizihimiza pande mbalimbali zitekeleze ahadi zao na kuhakikisha fedha hizo zinafikishwa kwa wakati.

Wakati huo huo, Marekani pia imetoa masharti kwa kuambatana na msaada kwa kwa Sudan. Bw Robert Zoellick alisisitiza kuwa iwapo serikali ya Sudan na pande zilizopambana katika sehemu ya Darfur hazitaacha mapambano kati yao ili kuimarisha usalama wa sehemu hiyo, na kuchukua hatua halisi katika mchakato wa amani, Marekani na nchi nyingine zitashindwa kutoa misaada hiyo kamili kwa utekelezaji wa mkataba wa amani wa Sudan.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-14