Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-14 16:59:39    
Kununua zawadi ya gazeti kumfurahisha rafiki yako

cri

Msichana Zhang Xue mwenye umri wa miaka 23 anayefanya kazi katika kampuni moja ya mjini Beijing, siku moja alipata zawadi ya siku ya kuzaliwa. Alipofungua kasha la zawadi lenye rangi ya waridi aliona gazeti la Beijingribao lililochapishwa katika siku aliyozaliwa, zawadi hiyo ilimfurahisha sana.

"Mwanzoni nilifikiri ni chocolate, sijawahi kupokea zawadi namna hii ya siku ya kuzaliwa, nilifurahi sana. Kwangu mimi zawadi hiyo ina maana zaidi kuliko zawadi nyingine kama maua."

Zawadi hiyo maalum aliyopokea msichana Zhang Xue ilinunuliwa kutoka kwenye duka la zawadi za siku ya kuzaliwa la Beijing liitwalo "Miaohang". Duka hilo linashughulikia zawadi za magazeti ya zamani, biashara yake ni nzuri sana. Siku chache zilizopita, mwandishi wa habari alipotembelea duka hilo lililoko kaskazini mwa Beijing alikuta ndani ya duka hilo yamejaa magazeti ya aina mbalimbali.

Mwendesha duka anaitwa Zheng Jun mwenye umri wa miaka 40. Bw. Zheng Jun alisema kuwa, hivi sasa, amekuwa na magazeti ya aina mbili yaliyochapishwa katika miaka 50 ya nusu ya mwisho ya karne iliyopita, yaani gazeti la Renminribao na gazeti la Beijingribao. Magazeti hayo ya kawaida yaliyochapishwa zamani yamekuwa zawadi nzuri za siku ya kuzaliwa.

Bw. Zheng Jun anasema kuwa, sababu muhimu ya magazeti hayo kupendwa na watu wengi kama zawadi ya siku ya kuzaliwa ni kutokana na thamani yake ya kiutamaduni. Mtu atafurahi sana kupokea gazeti lililochapishwa katika siku alipozaliwa, na kufahamu mambo makubwa yaliyotokea nchini na duniani wakati ule. Bw. Zheng Jun anasema:

"Gazeti lenyewe lina thamani ya kihistoria na kiutamaduni, wakazi wengi wa Beijing, mji mkuu wa China wanathamini sana mambo ya kiutamaduni. Gazeti hilo litamfahamisha hali ya historia na jamii alipozaliwa, hivyo litakuwa kitu chenye maana sana kwa aliyepokea zawadi hiyo."

Bw. Zheng Jun siku zote anapenda sana kukusanya magazeti ya zamani. Kufungua duka hilo kulitokana na habari aliyosikia kutoka kwenye radio ikisema kwamba, mchezaji maarufu wa riadha wa China alipokea zawadi ya gazeti la Times la Uingereza lililochapishwa katika siku alipozaliwa, jambo hilo lilimfurahisha sana. Habari hiyo iligusa hisia zake za biashara, hivyo alishughulikia upya magazeti aliyokusanya, alinunua magazeti mengi ya zamani, akafungua duka hilo katika nusu ya mwisho ya mwaka jana.

Bw. Zheng alisema kuwa, uuzaji wa magazeti ya siku ya kuzaliwa huendeshwa kwenye mtandao, bei za magazeti hayo hutofautiana kutokana na wakati wa kuchapishwa. Kwa mfano, gazeti lililochapishwa katika miaka ya 50 ya karne iliyopita linauzwa kwa yuan 300, na lile lililochapishwa katika miaka ya 90 ya karne iliyopita linauzwa kwa yuan 90 hivi.

Msaidizi wake anasema kuwa, mwanzoni watu wachache tu walikuja kununua magazeti, sasa watu wengi zaidi wanalifahamu duka hilo na biashara imekuwa nzuri siku hadi siku, kwa wastani kwa siku moja duka linaweza kupata wateja zaidi ya kumi. Watu wengi baada ya kununua magazeti hutoa maoni yao kwenye tovuti. Mteja mmoja wa kike alisema kuwa: "Nashukuru Bw. Zheng kwa kunisaidia kukamilisha tumainio langu, kuniwezesha kumpa mume wangu furaha ya mshangao wakati wa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, kweli hii ni zawadi nzuri."

Watu wanaonunua magazeti wanatoka katika fani mbalimbali, wengi zaidi ni walimu na makarani wa kampuni. Bi. Yang Shaoming mwenye umri wa miaka 27 mwaka huu anafanya kazi katika chuo kikuu kimoja cha Beijing. Siku chache zilizopita, alimnunulia mume wake zawadi ya gazeti. Alisema kuwa, alifanya hivyo kutokana na kutaka kueleza hisia zake kwa njia mpya. Bi. Yang anasema:

"Naona ni jambo la ajabu kumfahamisha mume wangu mambo yaliyotokea duniani katika siku alipozaliwa, hivyo naona kumpa zawadi ya gazeti kuna maana zaidi kuliko zawadi nyingine."

Mtaalamu anayefanya utafiti kuhusu hali ya jamii wa Beijing anaona kuwa, watu wengi kupenda kununua zawadi ya gazeti, kunaonesha mabadiliko ya ufuatiliaji wa wachina kuhusu maisha yenye umaalum.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-14