Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-14 19:45:30    
Ujumbe wa Baraza la Usalama waitembelea Haiti

cri

Ujumbe unaoundwa na wanadiplomasia kutoka nchi 15 wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana ulifika huko Port-au-Prince, mji mkuu wa Haiti, na kuanza ziara ya siku tatu nchini humo. huo ni ujumbe wa kwanza kutumwa na Baraza la Usalama kwa nchi za Caribbean. Katika ziara hiyo, ujumbe huo utakutana na viongozi wa serikali ya muda ya Haiti na mkuu wa tume maalum ya Umoja wa Mataifa nchini humo, na kuwasiliana na vyama mbalimbali na wananchi wa nchi hiyo. Wachambuzi wanaona kuwa, ziara hiyo inabeba majukumu mengi.

Kwanza, ziara hiyo inaonesha kuwa jumuiya ya kimataifa inafuatilia hali ya nchi hiyo na kuwa na nia kubwa ya kutatua suala hilo. Katika miaka 200 tangu nchi hiyo ipate uhuru, hali ya nchini humo iliendelea kuvurugika, vita, ghasia na uasi vilitokea mara kwa mara, uchumi wa nchi hiyo uko nyuma sana na nchi hiyo imekuwa nchi maskani kabisa katika kizio cha Magharibi. Mwezi Februari mwaka jana, rais wa zamani wa nchi hiyo Bw. Jean-Bertrand Aristide alijiuzulu na kukimbilia nchi za nje kutokana na shinikizo kutoka nchini na duniani, tukio hilo lilisababisha hali nchini humo kubadilika kuwa mbaya zaidi. Aidha, mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani na kukarabati nchi hiyo pia unakabiliwa na matatizo mbalimbali. Mwezi uliopita, askari wawili wa kulinda amani nchini humo waliuawa na wanamgamo wanaoipinga serikali ya nchi hiyo. Kutokana na hali hiyo, nia ya jumuiya ya kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa imezidi kuwa muhimu.

Pili, ujumbe huo utakagua kazi za tume maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti ili kuhimiza Baraza la Usalama likubali kurefusha kipindi cha majukumu ya tume hiyo. Tume hiyo ilifika nchini humo mwezi Juni mwaka jana, na inaundwa na askari 6012 na polisi 1400 kutoka nchi 30 duniani. Kutokana na utaratibu husika, Baraza la Usalama litajumuisha kazi ya tume hiyo mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu na kuamua kama litarefusha au la kipindi cha majukumu ya tume hiyo. Tangu kufika nchini humo, tume hiyo imefanya kazi muhimu katika kutuliza hali ya nchini humo, kutoa misaada ya kibinadamu na kuandaa uchaguzi mkuu na kazi hizo zinasifiwa na pande mbalimbali.

Tatu, ujumbe huo utasifu kazi ya serikali ya muda ya Haiti, kusukuma mbele mazungumzo kati ya vyama mbalimbali vya nchi hiyo na kazi ya kunyang'anya silaha kutoka kwa wanamgambo haramu. Wakati uchaguzi mkuu wa Haiti unapokaribia siku hadi siku, hivi karibuni, polisi ya nchi hiyo na tume hiyo zimeshirikiana na kuongeza nguvu ya kupambana na wanamgambo haramu, na kuwaua kwa nyakati tofauti viongozi wawili wa kundi la wanamgambo wanaoipinga serikali. Hivyo, moja ya majukumu makubwa ya ujumbe huo ni kuwasiliana na vyama mbalimbali vya Haiti na kuwashawishi wasameheane na kutimiza maafikiano ya taifa.

Nne, kuhimiza jumuiya ya kimataifa itekeleze ahadi za kutoa misaada kwa Haiti na kusukuma mbele ukarabati wa uchumi wa nchi hiyo. Jumuiya ya kimataifa ilifanya mikutano miwili ya kimataifa ya kutoa misaada kwa Haiti katika mwezi Julai mwaka jana na mwezi Machi mwaka huu, nchi na jumuiya za kimataifa zilizohudhuria mikutano hiyo ziliahidi kutoa misaada ya dola za kimarekani zaidi ya bilioni 2, lakini mpaka sasa asilimia 20 tu ya ahadi hizo zimetekelezwa. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Haiti Bw. Juan Gabriel Valdes aliainisha mara nyingi kuwa, kutotekelezwa kwa ahadi hizo kumezuia vibaya kazi ya ukarabati wa nchi hiyo.

Kwa ujumla, hivi sasa hali ya nchini Haiti inaelekea kuwa nzuri. Hali ya usalama imeboreka na kazi ya maandalizi ya uchaguzi mkuu inaendelea hatua kwa hatua. Ripoti mpya iliyotolewa jana na Jumuiya ya fedha ya kimataifa IMF imeainisha kuwa, mwaka huu uchumi wa Haiti unatarajiwa kuondokana na hali ya kupungua iliyoendelea kwa miaka mingi, na kuongezeka kwa asilimia 2.5. kutokana na hali hiyo, ziara ya ujumbe huo wa Baraza la Usalama inatazamiwa kupata mafanikio mema na kuhimiza Haiti itimize maafikiano ya taifa na kustawisha nchi mapema.

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-14