Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmoud Abbas tarehe 14 alitoa amri ya kufanyika kwa mageuzi ya jeshi la usalama ili kuimarisha uongozi. Hii ni hatua kubwa nyingine ya mageuzi ya usalama nchini Palestina.
Ofisa mmoja wa ngazi ya juu ambaye hakutaka kutaja jina lake alithibitisha kuwa Bw. Abbas ametoa amri ya kufanya vikosi 13 vya usalama kuwa vikosi vitatu ambavyo vitaongozwa na makao makuu ya usalama wa taifa, wizara ya mambo ya ndani na makao makuu ya upelelezi. Kutokana na mageuzi hayo, waziri wa mambo ya ndani Nasser Yousef ataongezewa madaraka zaidi, mbali na kuongoza wizara yake, pia ataongoza kikosi cha usalama wa taifa, na atasimamia mawasiliano kati ya vyombo vya uslama vya nchini na vyombo vya usalama vya nchi za nje.
Mageuzi ya jeshi la usalama ni hatua nyingine kubwa katika mfululizo wa mageuzi ya usalama. Tarehe 30 Machi watu wenye silaha wa Palestina walishambulia makazi ya Bw. Abbas yaliyoko mjini Ramallah kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Jordan, Bw. Abbas alimwondoa madarakani jemadari mkuu kutokana na udhaifu wake wa kupambana na matukio ya dharura, na kutangaza hali ya hatari kwenye sehemu ya ukingo wa magharibi ya Mto Jordan, kisha akapanga ofisi zote za jeshi karibu na makazi yake ili kurahisisha mawasiliano na kudhibiti vikosi vyote vya usalama. Baadaye alifanya mageuzi ya "mishahara ya wanajeshi na bima", na kuwastaafisha maafisa waliozidi umri wa miaka 60 na kuwapa vijana nafasi zao, ili kubadilisha damu mpya katika ngazi ya juu ya uongozi wa jeshi la usalama. Wachambuzi wanaona kuwa hatua hizo zimeweka msingi wa kufanya mageuzi hayo ya jeshi la uslama.
Vyombo vya habari vya Palestina vinaona kuwa hatua zake mfululizo za mageuzi zitaimarisha utawala, utulivu na kusukuma mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel.
Kwanza, mageuzi yatasaidia kuondoa tatizo sugu la tofauti za kisiasa kati ya vikundi vya jeshi, na kusaidia kuleta utulivu nchini humo. Kutokana na ripoti, nchini Palestina kuna askari wa usalama elfu 40 ambao wamegawanyika katika vikundi 13 vinavyotofautiana kisiasa. Kutokana na jinsi hali ya kisiasa inavyobadilika katika sehemu ya Mashariki ya Kati na nchini Palestina, vikundi vingine zaidi vinaendelea kugawanyika. Mgawanyiko wa vikundi hivyo unatokea kutokana na mazingira yaliyotatanisha ya kihistoria na ya kijamii, maslahi yao vinavyotetea ni tofauti na misimamo ya kisiasa pia ni tofauti. Baadhi vinatetea kufanya mazungumzo na Israel na baadhi vinatetea kupambana na Israel mpaka mwisho. Kutokana na kukosa uongozi mmoja na tofauti kati ya vikundi hivyo mara kwa mara vinakuwa na mgongano mkali. Hali kama hiyo sio tu ni changamoto kwa mamlaka ya utawala wa Palestina na kudhoofisha nguvu za kijeshi na pia ni tishio kwa usalama wa wananchi. Hatua za Abbas zitasaidia kubadilisha hali hiyo.
Pili, mageuzi hayo ya Abbas ni ahadi alizotoa wakati alipogombea nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi mkuu na kuleta mazingira ya kuzindua tena "mpango wa ramani ya amani" wa Mashariki ya Kati. Kufanya mageuzi ni moja ya ahadi muhimu alizotoa wakati Abbas katika uchaguzi mkuu wa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina uliofanyika mwezi Januari, na pia ni wajibu wa Palestina wa kuzindua "mpango wa ramani ya amani" wa Mashariki ya Kati. Nchi za Marekani na Israel zinatetea mageuzi ya usalama wa Palestina kama ni sharti muhimu la kuzindua "mpango wa ramani ya amani" ya Mashariki ya Kati, na Marekani imetuma mjumbe wake kumsaidia Bw. Abass kufanya mageuzi. Mageuzi ya Abbas yameonesha uaminifu wa kusukuma mchakato wa "mpango wa ramani ya amani" wa Mashariki ya Kati.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-15
|