Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-18 16:41:02    
Vitu vya mapambo kutoka nchi za Asia ya Kusini vyakaribishwa mjini Beijing

cri

Katika miaka miwili iliyopita, vitu vya sanaa na mapambo ya vito kutoka India, Nepal na Pakistan, vimekuwa vikipendwa sana mjini Beijing, na maduka yanayouza vitu hivyo yamekuwa mengi.

Katika upande wa kaskazini wa Kasri la Kifalme mjini Beijing kuna ziwa moja liitwalo Shishahai, kando ya ziwa hilo kuna duka moja linaloendeshwa na ndugu wawili, kaka na ndugu yake wa kike, duka hilo linauza vitu vya sanaa na mapambo ya vito kutoka nchi za Asia ya Kusini. Ingawa duka hilo sio kubwa lakini linajulikana kwa wengi.

Siku moja alasiri, mwandishi wetu wa habari alikwenda huko kulitembelea. Kuangalia kwa mbali, duka hilo linajitokeza zaidi kutokana na kuwa tofauti na maduka mengine mengi, kwenye dirisha kumetundikwa shashi nyeupe na kwenye mlango kuna pazia kubwa la rangi hudhurungi lenye picha za ndovu na tausi zilizotariziwa. Baada ya kuingia mlangoni alivutiwa na vitu vyenye rangi mbalimbali vilivyojaa dukani, kwenye ukuta yametundikwa mazulia yenye mapambo ya aina tofauti na mezani kuna skafu, mikoba ya ngozi na ya kitambaa, mashati na sketi zilizotariziwa kiajabu, vitu hivyo kwa kupambwa na manyoya ya kijani ya tausi vinaonekana vya kupendeza sana, huku muziki mwepesi unasikika kana kwamba unatoka mbali.

Mwenye duka anaitwa Luosang, ni kijana aliyetoka mkoani Tibet ambako ni mbali na Beijing, kutokana na jua kali huko alikoishi mkoani Tibet ngozi yake ni nyeusi, alipotambua kuwa anaongea na mwandishi wa habari kutoka Redio China Kimataifa mara aliwasalimu wasikilizaji kwa lugha ya Kitibet, akisema, "Ndugu wasikilizaji, hamjambo! Mimi naitwa Luosang, nimetoka Tibet, magharibi mwa China. Nawatakia mema."

Luosang alizaliwa katika ukoo unaotengeneza vitu vya mapambo ya fedha, miaka 7 iliyopita alikuja Beijing akafungua duka la kuuza vitu vya mapambo vya Kitibet, India na Nepal.

Bw. Luosang alimwaambia mwandishi wetu wa habari kwamba, miaka 6 iliyopita alipoanza kuuza vitu vya mapambo kutoka India na Nepal mjini Beijing, vitu hivyo vilikuwa havinunuliwi sana, lakini sasa vitu hivyo vinanunuliwa haraka sana. Alisema, "Kutokana na utalii kuimarika katika miaka ya karibuni, watu wanaokwenda India na Nepal ni wengi, na masimulizi kuhusu nchi hizo pia yamekuwa mengi. Vijana wengi wanavutiwa na utamaduni wa nchi hizo zenye waumini wengi wa dini ya Buddha. Vitu vilivyotoka kutoka nchi hizo vyote ni vya mikono na kila kimoja ni tofauti na kingine."

Wakati nilipozungumza na Luosang mteja mmoja aliyekuwa pembeni aliniambia, "Vitu ndani ya duka hili vinaweza kuridhisha wateja wanavyotaka, kwa rangi, kwa aina au kwa kuwa vya kisasa au kwa kuwa vya zamani."

Mwandishi wetu wa habari aliacha duka hili nikaenda kwenye duka lingine lililopo katikati ya mji wa Beijing ambalo pia ni dula linalouza vitu vya mapambo vya Nepal na India. Duka hilo si kubwa vilevile, ukubwa wake ni kiasi cha mita 3 tu za mraba. Hata hivyo vitu vinavyouzwa hapo ni maridhawa na vyote vilichaguliwa na mwenye duka Bi. Xiaotao yeye mwenyewe kutoka nchi za India na Nepal.

Bi. Xiaotao alikuwa na kazi yenye mshahara mkubwa, alitumia likizo yake kutembelea Tibet, huko aliona vitu vya aina mbalimbali vya mapambo ambavyo vinampendeza sana, baada ya kurudi Beijing aliacha kazi yake na kufungua duka hili.

Chimbuko la bidhaa zake ni nchi zinazotengeneza bidhaa hizo na anakwenda huko kuzichagua mwenyewe, ingawa gharama za bidha hizo zikiwa pamoja na nauli ni kubwa lakini bei anayowauzia wateja sio kubwa. Bi. Xiaotao alisema, nia yake ni kuwafahamisha tu wanunuzi bidhaa za nchi hizo. Alisema, "Bidhaa za Nepal na India zina uzuri wa aina yake, napenda kuwafahamisha wateja wangu, gharama za vitu hivyo kweli ni kubwa, lakini sitegemei kutajirika kutokana na bidhaa hizo bali nafurahia kupata marafiki kupitia bidhaa hizo."

Duka lingine alilotembea mwandishi wetu wa habari liko katika mtaa wa biashara Jiali, mwenye duka ni msichana mwenye sura ya kuvutia, anaweza kuongea Kiingereza kwa ufasaha, alijipamba kwa vito vinavyong'ara vya India, naye pia aliacha kazi yake na kufungua duka hilo baada ya kutalii Tibet. Alieleza kuwa anajishughulisha na bidhaa kutoka Nepal, India na Pakistan, licha ya duka hilo mjini Beijing naye pia amefungua maduka mengine katika miji ya Shenzhen, Shanghai na Chengdu. Duka hilo mjini Beijing linauza zaidi mapambo ya nguo na vitu vya shaba kutoka Nepal na Pakistan. Duka hilo likilinganishwa na duka lake lingine, lina utamaduni wa kidini zaidi, kwamba sanamu za Buddha ni nyingi. Alisema, "Vitu hivi vinaleta utamaduni mkubwa wa kidini wa India na Pakistan, kutokana na utamaduni wa kidini wasichana wengi wanapenda duka hilo."

Mjini Bejing kuna maduka mengi yanayouza bidhaa za nchi za Asia ya Kusini, maduka hayo si kama tu yametosheleza urembo wa wasichana, bali pia yamewasogeza Wachina karibu na utamaduni wa nchi hizo ambazo ni ngeni kwao.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-18