|
Waziri mkuu wa India Bwana Manmohan Singh jana huko New Dheli alifanya mazungumzo na rais Pervez Musharaf wa Pakistan ambaye yuko nchini India kutazama mchezo wa kriketi na kufanya ziara isiyo rasmi. Japokuwa mazungumzo yao hayakupata mafanikio makubwa, lakini viongozi hao wawili wamezidisha uaminifu na kufikia maoni ya pamoja katika kuongeza maingiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, na kutia uhai mkubwa kwa mchakato wa amani ya nchi hizo mbili.
Hii ni mara ya kwanza kwa rais Musharaf kuitembelea India katika miaka minne iliyopita. Jana asubuhi, Bw. Singh na Musharaf walitazama kwa pamoja mchezo wa kriketi kati ya India na Pakistan, baadaye walifanya mazungumzo kwa saa mbili, wakikumbuka mchakato wa mazungumzo ulioanzishwa mwaka jana, kujadili hali ya Asia ya kusini na kufanya mashauriano kuhusu suala la Kashmir na masuala mengine.
Katibu wa mambo ya nje wa India Bw. Shyam Saran alifahamisha kuwa, viongozi hao wawili walikubali kuunda kamati ya muungano ya biashara ya India na Pakistan ili kusukuma mbele uhusiano mzuri zaidi wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili; kukubali kuongeza mabasi yanayokwenda na kurudi kati ya miji mikuu miwili ya sehemu ya Kashmir zilizo chini ya udhibiti wa kila upande, kuanzisha usafirishaji wa shehena kwa malori kupitia sehemu ya Kashmir, na kuanzisha usafiri wa reli kati ya mji wa Munabao wa jimbo la Rajasthan la India na mji wa Khokrapar wa mkoa wa Sindh mwezi Desemba mwaka huu. Zaidi ya hayo, pande hizo mbili pia zimekubali kuunda kamati ya muungano inayoshughulikia utatuzi wa suala la mto wa barafu wa Siachen, na kuwaalika wataalamu kutoka nchi ya tatu kusaidia kutatua suala la boma la Baglihar linalogombewa.
Wachambuzi wameona kuwa, viongozi wa India na Pakistan kutumia "diplomasia ya mchezo wa kriketi" kuboresha uhusiano wa nchi hizo mbili kutokana na sababu kadhaa. Kwanza, baada ya kutokea kwa tukio la "9/11", Marekani ilianzisha vita dhidi ya ugaidi duniani. Ili kudumisha utulivu wa sehemu ya Asia ya kusini, na kuogopa maslahi yao kuathirika kutokana na uingiliaji kati wa Marekani, nchi hizo mbili zinapaswa kulegeza uhusiano wao na kutatua migongano yao zenyewe.
Pili, kwa upande wa Pakistan, kuongeza hali ya wasiwasi kwa suala la Kashmir bila shaka kutaathiri maendeleo ya uchumi nchini humo. Na kulegeza uhusiano kati yake na India kutamwezesha Musharaf kushughulikia zaidi mgogoro wa nchini kati ya vyama vya kisiasa na nguvu za kisiasa za kidini. Kwa upande wa India, kutatua suala la Kashmir kutasaidia kuizuia Marekani isiingilie kati sana mambo ya Asia ya kusini, na kujiwezesha kushughulikia zaidi mambo ya kimataifa na kutafuta hadhi ya nchi kubwa kwenye jukwaa la kimataifa.
Tatu, wanaviwanda na wafanyabiashara wa India na Pakistan wanataka kuboresha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
Lakini japokuwa viongozi wa nchi hizo mbili wameonesha udhati wa kuboresha uhusiano wao, na kuchukua hatua mwafaka, lakini kwa kuwa suala la Kashmir linahusiana na maslahi ya kimsingi ya nchi hizo mbili, hivyo si rahisi kwa nchi hizo mbili kusawazisha misimamo yao. Kabla ya mazungumzo hayo, Bw. Singh aliwahi kusema kuwa, anatumai nchi hizo mbili zitaimarisha maingiliano ya watu na bidhaa katika sehemu ya Kashmir ili kurahisisha suala la mpakani hatua kwa hatua. Jana alisisitiza kuwa, haiwezekani kuweka upya mstari wa mpaka katika sehemu hiyo na kupinga kuweka kikomo cha muda wa kutatua suala la Kashmir. Lakini Bw. Musharaf kabla ya kuitembelea India alisisitiza kuwa, Pakistan daima haitakubali mstari wa mpaka wa hivi sasa wa sehemu ya Kashmir. Hivyo mchakato wa amani wa India na Pakistan bado una njia safari ndefu.
Idhaa ya Kiswahili 2005-04-18
|