Tokea tarehe 18 hadi 24 Aprili, mwaka 1955 wajumbe wa nchi 29 za Asia na Afrika walifanya mkutano huko Bandung, Indonesia. Huu ulikuwa ni mkutano wa kwanza kabisa wa nchi za Asia na Afrika. Mwanadiplomasia mzoefu wa Pakistan, waziri wa mambo ya nje wa zamani ambaye alikuwa katibu mkuu wa ujumbe wa Pakistan Bw. Agha Shaan alihurudhia mkutano huo.
Bw. Agha Shaan ambaye sasa ana umri wa zaidi ya miaka 80, lakini akili yake ni timamu. Alisema, kabla ya mkutano huo nchi nyingi za Asia na Afrika zilipata uhuru, nchi hizo zilitumai kuungana pamoja na kusema kwa sauti moja katika mambo ya kimataifa. Baada ya shughuli nyingi za matayarisho, mkutano wa nchi za Asia na Afrika kwa mara ya kwanza ulianza kufanyika tarehe 18 Aprili, mwaka 1955 mjini Bandung, Indonesia.
Bw. Agha Shaan alisisitiza, huo ulikuwa ni mkutano muhimu na wenye maana ya mbali hasa katika pande mbili zifuatazo: Kwanza, huu ni mkutano uliofanywa na nchi hizo wenyewe ambao haukuhudhuriwa na nchi za kikoloni za Magharibi, ukionesha matumaini na matakwa ya pamoja ya watu wa Asia na Afrika katika juhudi za kupinga ubeberu; Pili, huu ni mkutano wa kwanza kabisa wa kimataifa uliohudhuriwa na China mpya. Bw. Shaan alisema,
"Mkutano wa Bandung ulikuwa ni wa kwanza kabisa kwa China kujitokeza katika mkutano wa kimataifa, waziri mkuu wa China marehemu Zhou Enlai pamoja na ujumbe wake alihudhuria mkutano huo, na kwenye mkutano alieleza sera za mambo ya nje juu ya msingi wa kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani, hotuba yake ilishangiliwa."
Bw. Shaan alisema, kwa juhudi za China na nchi nyingi zilizohudhuria mkutano huo mkutano wa Bandung ulipitisha "Taarifa ya Mwisho ya Mkutano wa Asia na Afrika". Taarifa hiyo imetoa kanuni 10 za uhusiano wa kimataifa ambazo kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani zilikuwa ni msingi wake, hadi sasa athari za kanuni hizo kumi bado zinaendelea." Bw. Shaan alieleza,
"Nchi tofauti zina mfumo tofauti, kwa mujibu wa hali ilivyo na matakwa ya wananchi nchi yoyote ina haki ya kutatua matatizo yake bila kuingiliwa na nchi nyingine. Migogoro yote ya kimataifa inapaswa kutatuliwa kwa kufanya mazungumzo ili kukwepa vita."
Bw. Shaan alisema, mkutano wa Bandung umeweka msingi wa uhusiano mzuri kati ya China na Pakistan. Katika siku za mkutano huo, waziri mkuu wa Pakistan Mohammad Ali na waziri mkuu wa China Zhou Enlai walifanya mazungumzo ya karibu, hayo ni mazungumzo ya kina kwa mara ya kwanza kati ya viongozi wa China na Pakistan. Wakati huo Pakistan ilisaini mkataba wa kijeshi na nchi za Magharibi, Mohammad Ali alieleza kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na Pakistan ilikuwa ni kwa ajili ya usalama wa taifa lake, na Pakistan kamwe haitashiriki vitendo vyovyote dhidi ya China. Waziri mkuu Zhou alionesha kuelewa aliyosema. Hii ndio sababu ya kimsingi ya uhusiano mzuri wa kuamiana kati ya nchi mbili. Bw. Shaan alisema, urafiki kati ya China na Pakistan umekuwa mfano mzuri kati ya nchi zenye itikadi tofauti.
Bw. Shaan alisema, moyo wa mkutano huo ni kupinga ubeberu, ukoloni na umwamba, na kuendelea pamoja kwa uhuru na kuishi pamoja kwa amani. Aliongeza,
"Hapo zamani duniani kulikuwa na nchi mbili kubwa zenye nguvu za kupindukia, na sasa kuna nchi moja tu. Katika hali ilivyo ya sasa, moyo wa mkutano wa Bandung unafaa uwe wa kuimarisha dunia yenye pande nyingi na kukwepa kutokea kwa upande mmoja tu na kutatua migogoro yote kwa njia ya amani."
Mwishowe, Bw. Shaan alisema, kuanzisha mfumo mpya wa kimataifa duniani kunapaswa kufuata moyo wa mkutano wa Bandung kwa msingi wa kutoshambuliana, kutoingiliana mammbo ya ndani, kuishi pamoja kwa amani, kuheshimiana, kushauriana kwa usawa, kuaminiana, kunufaishana, kuendeleza uchumi kwa pamoja na kukubali aina tofauti za utamaduni.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-19
|