Msikilizaji wetu Mogire Machuki wa kijiji cha Nyakware sanduku la posta 646, Kisii Kenya ametuandikia barua akianza kwa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wa idhaa ya kiswahili. Anasema huko Kenya wanashukuru mungu kuwa mwaka 2005 unaendelea vizuri, na yeye kama alivyoahidi kwenye barua yake ya mwaka jana, mwaka huu wa 2005 atazidisha na kuboresha mawasiliano kati yake na Radio China Kimataifa baada ya mwaka jana kuwa kimya kiasi.
Ingawa mwaka uliopita hakuwasiliana nasi kama mwaka juzi, lakini hii haimaanishi kuwa alikuwa hafuatilii matangazo yetu ya Radio. Anasema alisikiliza takribani asilimia 75 ya vipindi vilivyotangazwa, na hilo kwake sasa hivi ni utaratibu wake, kwani kwa wiki moja hususan siku za Jumapili lazima atembelee tovuti ya Radio China kimataifa Idhaa ya Kiswahili na kiingereza. Kukaa kwenye kompyuta kwa muda wa saa nne mfululizo inamaana kuwa tovuti ya CRI ni bahari ya kujiongezea busara, busara ambazo sio rahisi kupatikana kwingineko. Kwanza tovuti ya Radio China Kimataifa inafunguka kwa haraka na bila usumbufu wowote, na pili kwa tovuti zote ambazo ametembelea, anaona ni tovuti ya Radio China pekee yake ambayo vipindi vyake vinasikika kwa sauti na vipo kwa maandishi. Pia tovuti hiyo imejaa makala kadha wa kadha ambazo ni za kupendeza.
Taabu ambayo wanaendelea kukumbana nayo huko, ni ile gharama wanayolipa baada ya kumaliza kusoma kurasa za tovuti. Hapo Kisii hali ya mawasiliano bado ni ya hali ya chini na wanaomiliki kompyuta ambazo zimeunganishwa na mtandao wa Internet ni wachache. Lakini kutokana na upendo alionao kwa Radio China kimataifa, gharama sio shida, nia yake ni kuifahamu China zaidi, na ndio sababu anatembelea tovuti ya radio China kimataifa na kufuatilia vipindi vyake radioni.
Sambamba na uungaji mkono wa kuchapishwa kwa jarida dogo la "Daraja la Urafiki" na Radio China Kimataifa na wasikilizaji wa Radio China kimataifa, naye pia anatoa shukrani zake za dhati kwa CRI kwa hatimaye kufikia hatua hii ya kuchapisha jarida hilo. Anaamini kuwa jarida hilo pia tutaliweka kwenye tovuti. Ombi lake ni kuwa, kama ikiwezakana theluthi ya jarida hilo itengwe kwa ajili ya wasikilizaji. Theluthi nyingine itumike kuchapisha mambo yanayohusu China (hasa maswala ya China) na theluthi iliyobakia iwe ya "kutoka kwa wanaotuunga mkono". Na mwisho gazeti hili liwe na chemsha bongo ya kila mwezi swali likitolewa kutoka matangazo yetu. Hii itatoa changamoto kwa wasikilizaji kuzidi kuisikiliza zaidi Radio China Kimataifa.
Kuhusu jarida hilo dogo, tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, toleo la kwanza litachapishwa hivi karibuni, kwenye jarida hilo, tutanukuu barua za wasikilizaji wetu na makala mbalimbali, polepole ndio mwendo, tunataka kulifanya jarida hilo liwe na mvuto kwa wasikizaji wetu kutokana msaada wa wasikilizaji wenyewe. Kutokana na jinsi litakavyokuwa, jarida hilo hasa tutawatumia wasikilizaji wetu, na halitawekwa kwenye tovuti.
Bwana Machuki anasema kuwa, mwaka 2004 alipokea barua kadha wa kadha kutoka kwetu na zote ziliandamana na bahasha maalum ambazo tayari zimelipiwa gharama za stempu, hata barua hii aliyoiandika ametumia bahasha hiyo. Anatumai kuwa barua hii itatufikia tofauti na kipindi fulani ambapo barua zilikuwa zinarejeshwa kwake. Kwa hiyo ni matumaini yake ni kuwa tutaendelea kumtumia bahasha hizi ili wazidi kuwasiliana nasi kwa njia iliyo rahisi na haraka zaidi Anasema siku hizi gharama ya kutuma barua kwa posta moja kwa moja mpaka China imepanda maradufu kwa hiyo anaishukuru Radio China kwa utaratibu huo.
Akimaliza barua yake anasema kuwa, mwaka jana alitutumia barua kadha kwa njia ya e-mail, lakini hata moja haikujibiwa, kwa hiyo mwaka huu ameamua kutuma barua zaidi kwa njia ya posta. Anasema kama alivyoahidi mwaka huu atawasiliana nasi mara kwa mara na hivi sana anaendelea kuandaa makala maalum kuhusu mji wa "kisii na wakisii" kwa ajili ya jarida la Daraja la urafiki ambayo ataiambatanisha na picha.
Kuhusu suala barua za e mail kutosomwa, tunaomba utuwie radhi. Kwa kuwa wenye jukumu la kujibu hizo barua pepe ni wachache na wana majukumu mengi, ndiyo maana wakati fulani hali kama hiyo inatokea, hivyo tunaomba wasikilizaji wetu mtuvumilie kwa siku chache. Sasa hivi vijana wa idhaa yetu wanafanya bidii kujifunza mambo ya ofisi. Katika siku chache zijazo tuna uhakika wataweza kubeba majukumu makubwa zaidi katika idara yetu. Lakini hiyo haina maana kuwa hatutajibu barua pepe moja kwa moja, tutaendelea kuzifuatilia kwa juhudi.
Msikilizaji wetu Isack Kulwa wa sanduku la posta 161, Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akianza kwa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji, anasema yeye ni mzima na anaendelea kuisikiliza radio China kimataifa. Anatupa pole kutokana na kazi za kila siku za kuboresha idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, kwani kuna mambo mbalimbali yanayoonekana kuwa tumefanya ili kuwaelimisha na kuwaburudisha wasikilizaji wetu. Anatoa pongezi kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa.
Anasema huenda tukamshangaa msikilizaji kama yeye ya kuwa alikuwa wapi lakini ukweli ni kwamba amekuwa msikilizaji wetu kwa muda mrefu, lakini alikuwa bado hajaanza kuwasiliana nasi. Ukweli ni kwamba uaminifu wa Radio China kimataifa kwa wasikilizaji wake umemvutia sana hadi kufikia uamuzi huo wa kuwasiliana nasi zaidi.
Anasema Radio China kimataifa imekuwa ikiandaa mashindano mbalimbali ya chemsha bongo na haikosi kutoa zawadi kwa washindi nafasi ya kutembelea Radio China kimataifa baada ya kuonekana wamepata ushindi. Mfano huko Tanzania msikilizaji mmoja amewahi kutembelea Radio China kimataifa, baada ya kupata ushindi naye si mwingine ni ndugu Kilulu Kulwa. Na vilevile Radio China kimataifa haiachi kutoa zawadi kwa washiriki wa mashindano hayo. Na pia anapongeza uamuzi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa wa kuchapisha gazeti dogo la Daraja la urafiki.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-19
|