Viongozi na wawakilishi kutoka nchi karibu 30 za Afrika wamekutana leo huko Sharm el-sheikh nchini Misri, kushiriki mkutano wa 13 wa kamati ya utendaji ya viongozi wa nchi kuhusu "ushirikiano mpya wa maendeleo ya uchumi barani Afrika NEPAD". Viongozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali wakiwemo wa Umoja wa Afrika watajadili njia mwafaka za kuhimiza maendeleo ya bara la Afrika kwa ushirikiano mkubwa.
"ushirikiano mpya wa maendeleo ya uchumi barani Afrika" ulithibitishwa kwenye mkutano wa 37 wa wakuu wa Umoja wa Nchi huru za Afrika, OAU mjini Lusaka mwaka 2001, ambao ni programu ya ustawishaji wa uchumi na jamii. Jambo linalostahili kutajwa ni kuwa baadhi ya masharti yanayoambatana na misaada inayotolewa na baadhi ya nchi za nje yanaathiri nchi zinazosaidiwa, lakini "NEPAD" inasisitiza nchi za Afrika zijenge uhusiano mpya wa kiwenzi wa kunufaishana na nchi nyingine duniani.
Ili kujenga uhusiano huo mpya, mpango umesisitiza kuwa katika mazingira ya utandawazi nchi za Afrika zinatakiwa kuwa na mshikamamo mkubwa zaidi na kujenga uhusiano mzuri wa ushirikiano, ili kukabili kwa pamoja changamoto ya utandawazi. Licha ya hayo, mpango mpya unasisitiza kuanzisha uhusiano mpya wa ushirikiano na wa kunufaishana pamoja na nchi nyingine duniani, ili kuleta manufaa kwa nchi za Afrika na zilizoendelea kutokana na utandawazi na kupunguza athari mpya zinazoletwa na utandawazi.
Ili kuhakikisha "ushirikiano mpya wa maendeleo ya uchumi barani Afrika" unatekelezwa bila vipingamizi, kamati ya utendaji ya mpango huo mpya iliamua kujenga utaratibu wa kusimamiana wa Afrika. Mkutano wa sasa wa kamati ya utendaji utaorodhesha suala la mfumo wa kusimamiana kuwa ajenda muhimu ya mkutano. ili kuhimiza nchi za Afrika zitumie vigezo vya kimataifa katika shughuli za maendeleo na kutekeleza kanuni za uwazi. Nchi zinazoshiriki kwenye mpango huo zinapaswa kueleza wazi hali kuhusu usimamizi wa serikali, sera za uchumi na haki za binadamu na kuwa tayari kukaguliwa na nchi wanachama wengine kwa kufuata kigezo cha kimataifa. Endapo nchi fulani mwanachama haitapitishwa katika ukaguzi, kitendo cha mfumo wa ukaguzi kitaitaka nchi hiyo kufanya marekebisho na kuipa ushauri kamili. Endapo nchi hiyo itashindwa kufikia kiwango kinachotakiwa na kigezo hicho, basi nchi hiyo haitaweza kunufaika na mpango huo mpya kama wanachama wengine. Nchi zile zilizofikia kigezo hicho zitanufaika kutokana na misaada ya kimatafa na uwekezaji wa nchi za kigeni. Hivi sasa nchi 24 za Afrika zimejiunga na mfumo huo wa ukaguzi.
"ushirikiano mpya wa maendeleo ya uchumi barani Afrika" umefanya kazi muhimu sana katika kuhimiza kuboresha utawala. Ongezeko la uchumi wa Afrika limezidi kiasi cha ongezeko la idadi ya watu kwa miaka 6 mfululizo. Katika mwaka uliopita, ongezeko la uchumi katika sehemu ya kusini mwa Sahara lilifikia kiwango cha juu zaidi kuliko lile la miaka 8 iliyopita, na mwaka huu linatarajiwa kufikia kiwango cha juu zaidi. Mazingira ya usalama ya bara la Afrika pia yanaboreshwa hatua kwa hatua, mwanzoni mwa mwaka huu sehemu za kusini na kaskazini za Sudan zimesaini mkataba wa amani; hali ya kisiasa nchini Somalia na Liberia inaelekea kuwa ya utulivu. Yote hayo yamechangia ufanisi wa"ushirikiano mpya wa maendeleo ya uchumi barani Afrika" na kuinua kiwango cha maisha ya watu.
"NEPAD ilianzishwa na kutekelezwa na Umoja wa Afrika, lakini athari yake imekwenda nje ya Afrika. Mkutano wa viongozi wa kundi la nchi nane utakaofanyika huko Scotland mwezi Julai mwaka huu utaichukulia NEPAD kuwa moja ya ajenda za mkutano.
Hata hivyo, maendeleo ya Afrika yanakabiliwa changamoto kali, nchi nyingi za Afrika bado ziko nyuma kimaendeleo, zinabeba madeni mengi, kuna mapambano mengi na tatizo la kuenea kwa ukimwi.
Watu wanatarajia mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika utafanikiwa na kuhimiza utekelezaji wa NEPAD.
Idhaa ya Kiswahili 2004-04-20
|