Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-21 16:57:38    
Mkorea anayeendesha biashara nchini China

cri

Mji wa Weihai ni mji wa bandari wa mkoa wa Shangdong, mashariki ya China. Mji huo uko karibu na Korea ya Kusini, inachukua saa mbili tu kufika bandari ya Incheon ya Korea ya kusini kwa kupanda mashua ya kasi. Katika miaka mingi iliyopita, mji wa Weihai ulitilia maanani kujenga mazingira mazuri ya makazi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuwavutia watu wengi wa Korea ya Kusini kuwekeza vitega uchumi huko, Bw. Lin Qianxiek ni mmoja kati yao.

Bw. Lin Qianxiek mwenye umri wa miaka zaidi ya 40 mwaka huu alikuwa profesa wa kitivo cha lugha ya kichina cha chuo kikuu kimoja cha Seoul, anafahamu sana maandishi ya Kichina na utamaduni wa China. Kutokana na pendekezo la kaka yake mkubwa, mwaka jana Bw. Lin Qianxiek alikuja Weihai pamoja na familia yake, anafundisha Kikorea katika chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Xinxing cha Weihai na kuendesha jumba la Taekwond. Anasema:

"Mwaka jana nilipofika tu mjini Weihai, niliona hapa panafanana na Korea ya kusini, nilijisikia kama nimefika nyumbani. Hali ya hewa ya Weihai ni nzuri, wakazi wa hapa ni wakarimu, najisikia vizuri sana kuishi hapa."

Weihai ni mji wenye mandhari nzuri sana, mwaka 2003 ulipata tuzo ya makazi bora ya Umoja wa Mataifa. Bw. Lin anasema kuwa, anafurahia maisha ya huko. Japokuwa hawezi kuzungumza kichina, lakini jambo hilo haliwezi kumzuia kuwasiliana na wenyeji. Wanafunzi wake wanapenda sana kwenda kwenye darasa lake, Bw. Lin Qianxiek akishindwa kuwafahamisha wanafunzi wake maana yake, hutumia ishara ya mikono na lugha ya vitendo, mtindo wake wa ufundishaji huleta vichekesho darasani. Mwanafunzi wake mmoja aitwaye Chui Qing anasema:

Sauti

"Darasani kama tukishindwa kumwelewa, mwalimu Lin hutumia ishara ya mikono, mtindo wake wa kufundisha si kama tu unatuelewesha kwa urahisi, bali pia unachangamsha hali ya darasani."

Licha ya kufundisha lugha ya Kikorea, Bw. Lin pia anaendesha jumba la Taekwond huko Weihai. Alisema kuwa, kutokana na kuinuka kwa hali ya maisha, watu wanahitaji sana kujenga mwili na kuimarisha ari zao. Mchezo wa Taekwond ni aina moja ya mazoezi yanayowawezesha watu kujenga mwili na kuimarisha ari zao.

Bw. Lin Qianxiek alisema kuwa, lengo lake lingine la kuendesha jumba la mchezo wa Taekwond ni kumwandaa angalau bingwa mmoja wa daraja la dunia katika mashindano ya olimpiki yanayotarajia kufanyika mwaka 2008 mjini Beijing. Ili kutimiza lengo lake hilo, Bw. Lin amewaalika walimu wengine 5 wa mchezo wa Taekwond kutoka Korea ya Kusini kujiunga na jumba lake. Zaidi ya hayo, Bw. Lin pia anaendesha majumba ya mchezo wa Taekwond katika miji mingine ya Yintai na Weifang iliyo karibu na Weihai. Bw. Lin anasema:

"Siku za usoni nitaendesha majumba mengi zaidi ya Taekwond katika miji mingine ya mkoani Shangdong. Isitoshe, ili kuwarahisishia wachina kujifunza Kikorea na lugha nyingine, navumbua chombo cha kujifunza ambacho kitawawezesha wachina kujifunza lugha ya kikorea, kiingereza na kijapan kwa urahisi."

Licha ya wanafunzi wake katika chuo kikuu cha lugha za kigeni na jumba la mchezo wa Taekwond, Bw. Lin Qianxiek ana familia ya furaha. Anampenda sana mke wake Bi.Yun Mikeng na watoto wake wawili wanaoishi pamoja naye mjini Weihai. Bi. Yun Mikeng licha ya kujifunza kichina, kazi yake muhimu ni kumtunza mume na watoto . Kila jioni Bi. Yun Mikeng humlaki mume wake kwa vitoweo vitamu mezani na hali maridadi nyumbani.

Bila kujali uchovu wa kazi ya siku nzima, Bw. Lin Qianxiek akirudi tu nyumbani husahau uchovu na kuwa na furaha. Anacheza na watoto wake na kuimba wimbo pamoja na mke wake.

Wasikilizaji wapendwa, mnaosikia sasa ni maelezo kuhusu jinsi mkorea wa kawaida anavyoishi na kufanya kazi huko Weihai, mji wa pwani wa mkoa wa Shangdong.

Imefahamika kuwa, mjini Weihai sasa kuna kampuni zaidi ya 3000 zilizowekezwa na watu wa Korea kusini, na idadi ya wakorea wanaoishi mjini humo imefikia elfu kumi. Baadhi yao wanawekeza vitega uchumi, wengine wanashughulikia utafiti na kueneza utamaduni wa China na Korea ya kusini, na wengine wanakuja kujiburudisha katika mazingira mazuri ya makazi ya Weihai.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-21