|
Tiara ambazo zinachukuliwa kama ni michezo ya starehe ya jadi na kwa ajili ya kusherehekea sikukuu, zimeenea sana kwa wakazi wa mijini na vijijini nchini China. Mwanzoni mwa majira ya mchipuko kabla na baada ya Sikukuu ya Qingming ya kila mwaka, ambapo hali ya hewa inakuwa nzuri na majani huchipua, na miti huchanua ni kipindi kizuri mno cha kurusha tiara.
Tiara ni kitu cha kuunganisha sanaa za mikono, michoro na maandiko. Maumbo na michoro yake vinahusu mila na desturi, ujuzi wa utamaduni na nadharia ya uzuri ya nchi. Tiara zikiwa na maumbo mbalimbali ya mbayuwayu, vipepeo, kereng'ende, samaki wa dhahabu na binadamu, iliyo kubwa ina zaidi ya mita 100; na ndogo zina sentimita kadha tu.
Tiara zote hutengenezwa kwa mianzi au mafunjo, kutiwa mapambo na kufungwa kwa kutumia karatasi zilizochorwa au vitambaa vya hariri. Tiara hurushwa kwa kamba za pamba, mkonge au nailoni au hutundikwa katika majumba au nyumbani kama mapambo.
Tiara zilianza kutengenezwa katika kipindi cha zama za Chun Qiu (770 K.K-476 K.K) na zama za Madola ya Kivita (475 K.K- 221K.K). Kutokana na mahitaji ya kupashana habari za kijeshi, watu wa kipindi hicho walitengeneza tiara za kale zilizoweza kurushwa angani kwa nyenzo za mbao zilizo kama ndege. Baadaye kutokana na kukua kwa kazi za utengenezaji wa vitambaa vya hariri na uvumbuzi wa kutengeneza karatasi, tiara za kale zilipita hatua mbalimbali za mabadiliko na ukuaji hadi kufikia za hivi sasa. Tiara za namna hizi ziko za aina mbili kubwa yaani tiara za sehemu ya kusini zenye ubora wa juu, na zile za sehemu ya kaskazini zenye upana. Beijing, Tianjin, Weifang mkoani Shandong na Sitong mkoani Jiangsu ni mahali kunakotoa tiara hizo nchini China.
Weifang mkoani Shandong, ni mji wa kale unaojulikana kwa kazi za mikono. Hadi enzi mbili za Ming na Qing mchezo huo wa kurusha tiara ulikuwa mmojawapo wa michezo ya jadi, utengenezaji na utiaji mapambo ulitokea miongoni mwa watu. Baadaye baadhi ya watu walizichukua kuwa bidhaa za kibiashara, kwa namna hiyo wasanii wengi walitokea katika maingiliano ya biashara ya kuuziana tiara, wengi wao walianzisha viwanda vingi vidogo vya kutengeneza tiara na kufungua maduka maalumu. Weifang pamekuwa ni mahali panapokusanya, kutoa na kuvumbua aina nyingi za tiara.
Tiara za Weifang zina maumbo mbalimbali yanatofautiana na zinajulikana kwa ubora wa juu wa kufunga, kutiwa mapambo, kuchora na kurusha, zina hisia za uhai wa kijadi. Watu wa Weifang kila mwaka wanafanya sherehe kubwa ya kurusha tiara ili kuwavutia watalii na mashabiki wa nchini na ng'ambo.
Idhaa ya Kiswahili 2005-04-22
|