Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-22 16:09:43    
Mboga zapatikana mkoani Tibet

cri

Bi. Caidanzhuoma alipakia kweye baiskeli yake mboga nyingi. Mboga hizo za majani alizinunua kwenye soko kubwa la mboga baada ya kutoka kazini. Katika miaka ya karibuni mboga za aina nyingi zenye bei nafuu zinapatikana katika soko la Lhasa mkoani Tibet, magharibi mwa China. Kupatikana kwa mboga hizo kumebadilisha chakula chake ambacho hakikuwa na mboga kwa miaka mingi na pia kumeboresha maisha yake.

Siku hizi mboga zimekuwa kitoweo muhimu katika chakula cha Watibet. Hapo zamani Watibet walikuwa wanaweza tu kula nyama ya ng'ombe na mbuzi, makopo ya chakula, mbatata na mboga zilizokaushwa, lakini leo mboga za aina mbalimbali tena mbichi zinapatikana mkoani humo, chakula cha Watibet kimeanza kubadilika taratibu.

Mwandishi wetu siku chache zilizopita alimkuta Bi. Caidanzhuoma na kuzungumza naye. Bi. Caidanzhuoma ana umri wa miaka 49, alizaliwa na kukulia mkoani Tibet. Alisema, "Sijawahi kula mboga toka utotoni mwangu, na baadaye ingawa zilipatikana katika mji wa Lhasa, lakini bei zilikuwa aghali, sikuweza kumudu."

Miaka 10 iliyopita kilikuwa hakuna kilimo cha mboga, tatizo la mboga lilikuwa kubwa, figili, mbatata kilikuwa kitoweo pekee cha miaka mingi, na mboga chache mbichi zilizokuwa zinapelekwa huko kutoka nje ya mkoa zilikuwa zinauzwa kwa bei kubwa. Kumbukumbu zinaonesha kuwa mwaka 1981 ni tani 2.6 tu za mboga zilizozalishwa mkoani Tibet ambazo kwa wastani kila Mtibet hakupata kilo 14 kwa mwaka, au kilo moja kila baada ya siku 25.

Ili kuinua maisha ya Watibet na kutatua kabisa tatizo la mboga, kuanzia mwaka 1990 serikali ya mkoa wa Tibet inatenga yuan milioni 5 kwa mwaka kwa ajili ya kuanzisha bustani za mboga na kutatua kabisa tatizo hilo.

Mkuu wa Taasisi ya Sayansi ya Mboga mkoani Tibet Bw. Dai Guoan alisema, "Kutokana na tabia ya hali ya hewa na udongo mkoani Tibet, aina mpya za mboga zinazovumilia baridi katika uwanda wa juu zilianza kupandwa, na mboga zilianza kupatikana kwa wingi."

Mwaka 2004 maeneo ya kilimo cha mboga yalifikia hekta elfu 16, aina za mboga zilifikia 200 na mazao yalifikia tani laki 3.48 ambazo ni ongezeko la mara 12.34 kuliko mwaka 1981. Kwa wastani kila Mtibet aliweza kupata kilo 134 za mboga kwa mwaka na kila baada ya siku tatu anapata kilo moja ya mboga. Tatizo la mboga limepungua mkoani humo.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Kilimo na Ufugaji ya Mkoa wa Tibet Bi. Gao Ling alisema, "Sasa miji ya Lhasa, Shannan, Rikaze, Changdu, Linzhi na baadhi ya wilaya zinapata mboga kutoka mkoani humo kwa asilimia 85, sehemu zenye baridi kali kutokana na mwinuko wa ardhi pia zimeanza kulima mboga kwa kutumia bustani za kufunikwa kwa plastiki.

Hivi sasa vitoweo vya mboga zilizozalishwa mkoani Tibet vinapatikana katika mikahawa yote mjini Lhasa, na ukiwa na bahati hata unapatiwa waridi jekundu mezani lililopandwa kiungani mwa Lhasa ndani ya kibanda kilichofunikwa kwa plastiki.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-22