Rais Levy Patrick Mwanawasa alikutana na ujumbe wa kutoa mkono wa pole wa serikali ya China unaoongozwa na Bw. Chen Jian ambaye ni msaidizi wa waziri wa biashara ya China na Bw. Wu Xiaohua ambaye ni naibu mkurugenzi wa tume ya usimamizi wa raslimali za taifa ya baraza la serikali la China tarehe 24 huko Ndola, mji mkuu wa mkoa wa Copperbelt, nchini Zambia.
Bw. Chen Jian alimwelezea rais Levy Patrick Mwanawasa maombolezo ya rais Hu Jintao wa China, serikali na watu wa China kutokana na watu waliokufa katika ajali ya mlipuko iliyotokea hivi karibuni katika kiwanda cha baruti cha BGIMM kinachoendeshwa kwa mitaji ya China. Chen Jian alisema kuwa upande wa China unaona masikitiko makubwa kutokana na idadi kubwa ya watu waliokufa na kujeruhiwa katika ajali hiyo, na serikali ya China inapenda kushirikiana na upande wa Zambia katika kutafuta vyanzo vya ajali hiyo na kutoa uungaji mkono wa kiteknolojia na msaada unaohitajika. Bw. Chen Jian alisema kuwa serikali ya China imeamua kuipatia serikali ya Zambia misaada ya fedha taslimu za dola za kimarekani laki tano na vitu. Alisema kuwa urafiki kati ya China na Zambia umepitia muda na mabadiliko ya hali, upande wa China unapenda kushirikiana na upande wa Zambia, kuvuka shida za njiani kuelekea mbele na kuhimiza uhusiano wa kirafiki na kishirikiana kati ya pande hizo mbili uendelee zaidi.
Rais Levy Patrick Mwanawasa alitoa shukrani zake kwa ujumbe wa serikali ya China kuitembelea Zambia na kumtaka Chen Jian afikishe salamu zake kwa rais Hu Jintao. Alisema kuwa ingawa Zambia na China zinatengana kwa umbali mkubwa, lakini baada ya ajali hiyo kutokea, watu wa China wameonesha ufuatiliaji na huruma kubwa na serikali ya China imetuma mara moja ujumbe wa ngazi ya juu kutoa mkono wa pole kwa watu wa Zambia, watu wa Zambia wanashukuru na kutiwa moyo na jambo hilo. Rais Mwanawasa aliishukuru serikali ya China kwa kutoa msaada wa dharura na uungaji mkono na misaada mbalimbali iliyotolewa kwa Zambia kwa muda mrefu. Alieleza imani yake kuwa ajali hiyo haitaathiri urafiki wa jadi na uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Baada ya mkutano huo, rais Mwanawasa na ujumbe wa kutoa mkono wa pole wa serikali ya China kwa pamoja ulikagua mahali palipotokea ajali hiyo, kuwapa mbirambi watu waliofiwa na wakazi wenyeji, na kwenda hospitali kuwatazama watu waliojeruhiwa.
Ujumbe wa kutoa mkono wa pole wa serikali ya China uliwasili nchini Zambia tarehe 23 usiku wa manane.
Tarehe 20 asubuhi, mlipuko ulitokea katika kiwanda cha baruti kinachoendeshwa kwa mitaji ya China cha eneo la viwanda vya China lililoko mjini Kalulushi, mkoani Copperbelt, Zambia.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-25
|