Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-25 15:37:30    
Vivutio vya Sehemu ya milimani ya Yeshanpo

cri

Sehemu ya milimani ya Yeshanpo iko kilomita 100 na kitu kutoka Beijing, eneo lake ni kilomita za mraba 600, ambapo kuna vivutio mbalimbali kama vile Bonde Baili, Mto Juma, Mnara wa mapango ya sanamu za buddha, Msitu asilia wa Baicaopan, Genge la Longmeng na Mlima Jinhua, na mandhari ya Bonde Baili inawavutia watu zaidi. Bonde Baili linasifiwa kuwa ni "bonde la michoro lenye maili mia moja", na "sehemu yenye utulivu inayopendwa zaidi na watu". Bonde hilo lina hali ya maumbile ya kiasili kabisa kwenye sehemu ya Yeshanpo. Bonde hilo liliundwa na mabonde matatu marefu, urefu wake ni kilomita 22.5. Watalii wakiingia kwenye bonde hilo, wanaweza kujisikia kama vile wameingia peponi, ambapo kuna milima mirefu inayozungukwa na miti, maua na majani ya ajabu, na njia nyembamba za mawe madogomadogo zinatambaa kwa mbali. Mwongozaji wa utalii Dada Li Jing alisema:

Bonde Baili ni bonde lenye njia nyembamba sana, kando mbili imesimama milima, watu wakitembea kwenye bonde wanaweza kuona kuwa mbingu imeacha nafasi ndogo kama mwanya. Kwenye bonde hilo kuna kivutio cha Longmengtianguan ambacho daraja na ngazi moja moja zinazunguka na kuwekwa kati ya bonde la milima, watu wakipanda juu na kushuka chini kwa kufuata ngazi.

Ukifuata Bonde Baili kuelekea ndani utafika kwenye "bonde la nge", jina hilo lilitokana na majani mengi madogomadogo ambayo watu wakiyagusa, watasikia maumivu makali mara moja. Lakini watalii wengi wanapenda kwenda kwenye "bonde la nge", kwani bonde hilo ni jembamba sana, wakilala kwenye ardhi kuangalia mbingu, wataona kweli mbingu imeacha nafasi ndogo sana kama mwanya.

Mbele ya bonde hilo ni sehemu ya "mdomo wa chui", sehemu hiyo inaonekana kuwa ni sehemu inayotisha, watalii wakisimama kwenye "mdomo wa chui", watajiona kama ni wadogo kabisa, kama vile wamemezwa na "chui". Na nguzo za mawe zinazosimama kwenye milima ya kando mbili zinaonekana kama meno ya "chui". Wakielekea mbele wataona mwanga, ambapo maua mengi ya Haitang yaani maua ya mitufaa ya kichina yamechanua pote, sehemu hiyo inajulikana kuwa ni bonde la maua ya Haitan.

Inasemekana kuwa, zamani sana kulikuwa na baba mzazi Ma Sanhe na binti yake Haitang waliokuwa wakiishi kwa kuwinda wanyama. Siku moja baba na binti yake walipokuwa mawindoni, walimwona chui mmoja akija, binti alipambana kishujaa na chui yule ili kumlinda baba yake, lakini aliuawa na yule chui. Wanakijiji waliopata habari walikuja kuwasaidia, wakambeba binti huyo kurudi kijijini. Njiani damu ya binti huyo ilikuwa ikitiririka kila mahali, baadaye sehemu ambayo damu ilikuwa imetiririka yakaota maua pote bondeni, watu wakayapa maua hayo jina la Haitang, ili kumkumbuka binti Haitang.

Katika sehemu iliyo karibu na Yeshanpo kuna kijiji kimoja cha Guogezhuang. Kwenye kijiji hicho hakuna hoteli, watalii wengi wakienda huko wengi wanakaa nyumbani kwa wakulima, hoteli hizo za wakulima ni safi na za bei nafuu. Bibi Ma Cunhua na mume wake wanaofanya biashara mjini Beijing, kila mwaka ifikapo majira ya joto huenda Yeshanpo, kukaa nyumbani kwa wakulima kwa siku kadhaa.

Wanasena watu waliozoea kukaa kwenye majengo ya ghorofa mjini, wanaona raha kukaa kwa siku kadhaa nyumbani kwa wakulima.

Sehemu ya Yeshanpo ina vivutio vingi vya utalii, ingawa sehemu hiyo siyo kubwa sana, lakini kutembelea sehemu nzima kunahitaji muda.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-25