Tarehe 25, mgombea wa rais kutoka chama tawala cha Togo Bw. Faure Gnassingbe na kiongozi wa chama muhimu cha upinzani Bw. Gilchrist Olympio huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria walikubali kwa kauli moja kuwa, endapo chama chochote kitashinda kwenye uchaguzi wa rais, kiwe Chama tawala cha Muungano wa umma wa Togo au chama cha upinzani, Togo itaunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayowakilisha maslahi ya wananchi wote. Makubaliano hayo yanatazamiwa kuwa hatua muhimu ya kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Togo.
Ili kuondoa migongano kati ya vyama mbalimblai vya Togo katika uchaguzi wa rais, na kupunguza hali ya wasiwasi nchini humo, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo siku hiyo huko Abuja, aliitisha mazungumzo kati ya wawakilishi wa chama tawala cha Togo na Muungano wa vyama vya upinzani. Bw. Faure na Bw. Olympio wakiwakilisha vyama vyao walishiriki kwenye mazungumzo hayo.
Wakati wa mazungumzo hayo, rais Obasanjo amevitaka vyama mbalimbali vya Togo kuheshimu matokeo ya uchaguzi, na kulinda amani na utulivu wa nchi hiyo. Baada ya mazungumzo hayo ya saa tano, rais Obasanjo alitangaza kuwa, chama tawala cha Togo na Muungano wa vyama vya upinzani vimekubali kuwa, chama chochote kati ya vyama viwili kikishinda kwenye uchaguzi, kitaunda serikali ya umoja wa kitaifa, na kuwashirikisha wawakilishi wa vyama mbalimbali. Aidha, vyama mbalimbali vya Togo, Umoja wa Afrika na ECOWAS zitapeleka wawakilishi kuunda tume maalum, ili kusimamia maendeleo ya hali ya Togo na hali ya utekelezaji wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Mbali na hayo, vyama mbalimbali vya Togo vitathibitisha tena katiba ya sasa, ili kuhakikisha inaonesha vya kutosha moyo wa "demokrasia, haki za binadamu, utaratibu wa sheria na kuwashirikisha watu wote katika mambo ya kisiasa."
Mgogoro wa kisiasa nchini Togo unatokana na kufariki dunia kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Gnassingbe Eyadema. Wakati huo, ili kuhakikisha nchi hiyo ina kiongozi, Bunge la umma la Togo lilifanya marekebisho ya katiba chini ya uungaji mkono wa jeshi, na kumteua Bw. Faure kuwa spika, na baadaye kushika madaraka ya rais. Lakini kitendo hicho kililaaniwa na jumuiya ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Afrika na vyama vya upinzani vya nchi hiyo. Kutokana na shinikizo kubwa kutoka nchini na nchi za nje, Bw. Faure alijiondoa kutoka kwenye wadhifa wa urais, na kutangaza kurejesha utaratibu wa katiba, na kufanya uchaguzi wa rais, na alishiriki kwenye uchaguzi akiwa mgombea urais kutoka chama tawala.
Upigaji kura katika uchaguzi wa rais wa Togo ulimalizika tarehe 24 usiku, lakini chama tawala cha Togo na Muungano wa vyama vya upinzani vimelaumiana kufanya udanganyifu katika uchaguzi huo, na kuchochea migogoro kati ya waungaji mkono wa pande hizo mbili, na kusababisha vifo vya watu wengi. Kabla ya hapo, pande hizo mbili zilifanya mapambano ya kumwaga damu wakati wa kampeni za urais, na kuchochea mgogoro nchini humo.
Watu wanaona kuwa, chama tawala cha Togo na Muungano wa vyama vya upinzani vimefikia makubaliano kuhusu suala la serikali ya umoja wa kitaifa ni kwa ajili ya kuepukana na fujo kubwa zaidi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu. Sababu muhimu ya hali hiyo ni kuwa, rais wa zamani wa Togo Gnassingbe Eyadema alishika madaraka kwa miaka 38, hali hiyo imewafanya watu wengi waone uchovu. Wakati Eyadema aliposhika madaraka, vyama vya upinzani vilizuiwa kushiriki kwenye shughuli za kisiasa nchini humo, na vyama hivyo vinataka kujihusisha na mambo ya kisiasa baada ya kufariki dunia kwa Eyadema. Aidha, nguvu za vyama hivyo viwili zinalingana. Kutokana na hali hiyo, chama chochote kati ya hivyo kinaweza kushinda, ni vigumu sana kwa chama kimoja kushika madaraka peke yake.
Wachambuzi wanaeleza kuwa, ingawa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ni njia nzuri kuondoa mgogoro wa kisiasa nchini Togo, lakini vyama mbalimbali vya Togo vinapaswa kuondoa migongano iliyopo kati yao kwa muda mrefu kwa hatua halisi, na kutekeleza kwa makini makubaliano yanayohusika, kwa njia hiyo vitarejesha amani na utulivu wa nchi hiyo kama ilivyokuwa zamani.
Idhaa ya Kiswahili 2005-04-26
|