Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-26 16:41:22    
Barua 0426

cri
Msikilizaji wetu Abdillahi W. Shaban wa sanduku la posta 1304 Kakamega Kenya ametuletea barua akianza kwa kutusalimu na kutueleza kuwa yeye huko Kenya ni mzima kabisa. Ameandika barua hii kwa lengo la kushukuru kutokana na barua ambazo tumekuwa tukimwandikia mara kwa mara, na kusema anamwomba mwenyezi mungu atujalie sisi zote afya njema na kuendelea na uhusiano mzuri. Na anatutakia kila la kheri kwa kazi tunayowafanyia wasikilizaji wa Radio China kimataifa, pia anatushukuru kwa kuwatumia bahasha zilizolipiwa gharama za stempu ili kurahisisha mawasiliano kati yetu. Lakini anasema kuwa yeye bado anatatizo, kwani kila anapokwenda posta kutuma barua zake China, anakatazwa na kuambiwa kuwa bahasha hazipokelewi kwenye posta ya huko.

Kuhusu jambo hili wasikilizaji kadha wa kadha wamekuwa wakilituletea barua kutuambia kuwa, bahasha tunazowatumia hazikubaliwi katika posta zilizo jirani nao. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu wanaozipokea bahasha tunazowatumia wataweza kuzituma barua bila vikwazo. Mwanzo tatizo hili lilikuwepo kwenye sehemu kubwa lakini kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo tatizo hilo linapungua. Tumeambiwa kuwa bahasha hizo zinatumika, na wasikilizaji wetu wengi wameshatumia bahasha hizo kutuletea barua bila matatizo na bado wanaendelea kufanya hivyo. Kwa hiyo tunatumai kuwa Bw Abdillahi Shaban utaweza kutuma barua bila tatizo.

Msikilizaji wetu Richard Chenibei Mateka wa sanduku la posta 65 Kapkateny Mlima. Elgon Kenya, ametuletea barua akitoa salamu na pongezi kwa watangazaji na wasikilizaji wa Radio China Kimataifa. Pia anasema kutokana na matangazo yaliyosikika kwenye idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa, kuna siku alipokea wageni na marafiki waliomtembelea nyumbani kwake, wakimtaka awatembeze ili wajionee maendeleo na mafanikio ya jamii ya Sabaot, kama walivyosikia katika historia na utamaduni kwenye matangazo hayo. Anasema baada ya kuwatembeza waliahidi kurudi mwaka huu wakiwa wengi zaidi ili wajionee zaidi maendeleo hayo.

Anasema wageni wake pia walimwambia wakiweza watajitahidi kuweka raslimali zao huko, na yeye mwenyewe bwana Mateka aliwaahidi kuwasaidia kutafuta sehemu moja kama makao kwa wageni hao, ambao pia walivutiwa na uchumi na biashara, utalii na utamaduni wa waafrika na vyakula vya kuhifadhi mwili na kuongeza kuishi miaka mingi hadi miaka mia moja ishirini na tano.

Pia anasema Jamii ya Sabaot inaomba kurudiwa kwa matangazo kuhusu historia na utamaduni ya wasabaot, kwani baada ya kusikia Idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa ikiwazungumzia, wengi hawakuamini kama wanajulikana kimataifa na sasa amewaelimisha kuitisha mikutano kuhusu utangazaji na utalii na manufaa yake kupitia idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema kuwa yeye ataendelea na kazi yangu kwa bidii na kuimarisha matangazo na vipindi vya idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa, kujuliana hali na kuwafahamisha wachina na wakenya undugu, upendo na maisha bora kwa kuboresha vipindi na matangazo ya Radio China Kimataifa.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-26