Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-27 14:46:47    
Ibrahim Al-Jafari awasilisha orodha ya majina ya baraza la mawaziri kwa tume ya urais ya Iraq

cri

Msemaji wa Bw. Ibrahim Al-Jafari aliyeteuliwa kuwa waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Iraq tarehe 26 alithibitisha kuwa, Bw Jafari ametoa orodha ya majina ya baraza la mawaziri na kumpa rais Jalal Talabani. Kama orodha hiyo itakubaliwa na tume ya urais inayoundwa na rais na makamu wake wawili, Bw Jafari atawasilisha orodha hiyo ijadiliwe kwenye bunge la umma la mpito la Iraq.

Kiongozi nambari mbili Bw. Jawad Al-Maliky wa Chama cha kiislam Dawa kinachoongozwa na Bw Jafari tarehe 26 alidokeza kuwa baraza jipya la mawaziri litakuwa na mawaziri 33, kati ya hao 17 wanatoka Chama cha muungano wa shirikisho la Iraq ambacho ni chama kikubwa kabisa kwenye bunge la Iraq, 8 wanatoka katika Chama cha muungano wa Kurd na Chama cha Suni kinachochukua asilimia 20 ya idadi nzima ya Wairaq kitakuwa na nafasi 6. Maofisa wengine wa Chama cha muungano wa shirikisho la Iraq walieleza kuwa serikali mpya itakuwa na manaibu waziri wakuu watatu ambao watatoka kwenye vyama vya muungano wa Kurd na Suni, shirikisho la vyama linaloongozwa na waziri mkuu wa serikali ya muda Bw. Iyad Allawi halitashika nafasi hata moja.

Vyombo vya habari vya kiarabu viliainisha kuwa orodha hiyo inaonesha kuwa mpango wa kuundwa kwa serikali mpya umethibitishwa na umeleta matumaini kwa ajili ya kuondoa hali ya kukwama ya kisiasa iliyosababishwa na makundi mbalimbali kugombea nafasi za baraza la mawaziri katika wiki kadhaa zilizopita na kufanya juhudi kwa ajili ya kumaliza hali ya machafuko ya hivi sasa. Kama orodha hiyo itakubaliwa na tume ya urais, pia itaungwa mkono na bunge na kuufanya uteuzi wa waziri mkuu na orodha ya baraza jipya la mawaziri ipitishwe na upigaji kura wa bunge bila vikwazo.

Lakini wachambuzi waliainisha kuwa Bw. Jafari alitoa orodha hiyo ya baraza la mawaziri katika hali ya kukabiliwa na shinikizo. Kwa upande mmoja, Wairaq wanaoteswa na mashambulizi ya kila siku wanataka kuunda serikali mpya haraka iwezekanavyo, ili kurejesha usalama na utulivu nchini. Kwa upande mwingine, kutokana na maslahi yake yenyewe, Marekani pia imeweka shinikizo kwa viongozi wa Iraq mara kwa mara na kuwahimiza waunde baraza hilo haraka zaidi. Kwa hiyo wachambuzi wanaona kuwa orodha hiyo ilitolewa na Jafari bila kujadiliwa ipasavyo, kwa hiyo si rahisi kuungwa mkono na makundi mengi.

Zaidi ya hayo, kundi la Allawi limeondolewa katika baraza la mawaziri, na uwakilishi wa serikali mpya pia umepungua. Kundi la Allawi litakuwa chama kikubwa kabisa kisicho tawala, jambo hilo litakuwa wingu jeusi kwa serikali mpya ya Jafari kutumia mamlaka yake bila vikwazo.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-27