Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-27 20:16:23    
China kutekeleza utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano

cri
    China ni nchi kubwa ya kilimo ambayo asilimia 70 ya wananchi wake ni wakulima. Katika miaka ya 50 ya karne iliyopita, China iliwahi kutekeleza utaratibu wa matibabu ya ushirikiano vijijini, ili kutatua suala la matibabu kwa wakulima. Lakini hivi sasa utaratibu huo wa zamani haufanyi kazi kwenye sehemu nyingi, kutokana na ukosefu wa fedha. Kutokana na kutokuwa na utaratibu wenye ufanisi wa huduma za matibabu, na maendeleo ya polepole ya uchumi wa vijiji, hivi sasa tatizo la matibabu kwa wakulima bado lipo vijijini, na linasababisha familia nyingi ziwe maskini.

    Ili kubadilisha hali hiyo, China ilifanya majaribio ya kuanzisha utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano kwenye vijiji kadhaa.

    Bw. Wu Junzhang wa mji wa Gong Zhuling, mkoani Jilin, katika siku za karibuni, alivunjika shingo. Mke wake alimwambia mwandishi wa habari kuwa kwa bahati, yeye alijiunga na utaratibu wa matibabu ya ushirikiano, la sivyo gharama kubwa za matibabu zingewaletea matatizo ya kiuchumi. Alisema: "Bila kutarajia tumenufaika na utaratibu huo mara baada ya kujiunga nao. Hapo awali tuliwaiga watu wengine kujiunga na utaratibu huo, kitu tulichofikiri ni kuwa tutapata ruzuku ya matibabu. Hivi karibuni mume wangu alivunjika shingo vibaya, na mfuko wa matibabu ya ushirikiano ukampa ruzuku ya zaidi ya yuan elfu 3, la sivyo, tungekopa fedha hata tusingeweza kulipa madeni mpaka sasa."

    Hivi sasa, watu wengi wananufaika na utaratibu huo kama Bw. Wu Junzhang. Utaratibu huo mpya unaendeshwa kama ifuatavyo: wakulima wakitoa yuan 10 kwa mwaka wanaweza kujiunga na utaratibu huo, na serikali inatoa ruzuku nyingine ya yuan 20, halafu fedha hizo, yaani yuan 30 kwa mwaka, zitalimbikizwa kwenye akaunti maalum kama mfuko wa matibabu. Wakulima waliojiunga na utaratibu huo wakimwona daktari kwenye hospitali zilizoteuliwa, watarudishiwa baadhi ya gharama za matibabu. Lakini hospitali hizo zinachaguliwa kwa vigezo makini. Mkuu wa idara ya usalama ya mji wa Gong Zhuling Bw. Li Xiaochun alisema: "Idara ya afya ya mji huo ilichagua hospitali 8 za ngazi ya mji zenye hali nzuri na teknolojia ya kisasa, na hospitali nyingine 22 za ngazi ya wilaya kuwa hospitali zilizoteuliwa kushiriki kwenye utaratibu wa matibabu wa ushirikiano, pia idara hiyo inazitaka hospitali za ngazi ya wilaya zianzishe vituo vya matibabu kwenye vijiji vya mbali, na kutoa huduma kwa wakulima mara mbili kwa wiki."

    Ili kuhakikisha mfuko wa matibabu unatumiwa na wakulima, mji huo ulianzisha tume ya usimamizi iliyoundwa na maofisa wa idara ya uendeshaji wa mashitaka, idara ya usimamizi na idara ya fedha, na tume hiyo itasimamia na kukagua matumizi ya mfuko wa matibabu kila baada ya muda fulani. Aidha, ili utekelezaji wa utaratibu huo uwe wazi zaidi, serikali ya mji huo iliweka matangazo yanayoonesha hali ya matumizi ya mfuko wa matibabu kwenye hospitali. Mpaka sasa, asilimia 80 ya wakulima wa mji wa Gong Zhuling wamejiunga na utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano.

    Utaratibu huo wa majaribio hivi sasa umeanzishwa Jiutai, mji mwingine wa mkoa wa Jilin. Wakulima wa huko wanajiunga haraka na utaratibu huo. Mkulima Bw. Wang Zhongliang wa kijiji cha Gouwai cha mji huo, hivi karibuni alilazwa hospitali ni kutokana na kuumwa tumbo, kwa kuwa amejiunga na utaratibu wa matibabu ya ushirikiano, amerudishiwa gharama za matibabu ya yuan mia 4. Bw. Wang alisema kwa furaha: "Serikali inatoa huduma nzuri kwa sisi wakulima kupitia utaratibu huo. Utaratibu huo umeondoa shida zetu nyingi. Siku za zamani, kila baada ya kuumwa, sisi wakulima tulikuwa tunakabiliwa na matatizo ya kiuchumi. Ingawa ruzuku ya matibabu ni kidogo, lakini fedha hizo zimetusaidia sana."

    Kwa kuwa tunanufaika na utaratibu huo bila kutozwa fedha nyingi, hivi sasa, asilimia 85 ya wakulima wa mji wa Jiutai wamejiunga na utaratibu huo mpya, na hali ya kutokuwa na fedha za kutosha za matibabu inapungua. Bi. Jiang Enqin, ambaye anashughulikia utaratibu huo wa mji wa Jiutai alisema kuwa, kutokana na matatizo ya kiuchumi, wakulima wakiumwa walikuwa hawataki kumwona daktari, lakini baada ya kuanzishwa kwa utaratibu huo, wakulima wengi wanakwenda kumwona daktari wanapoumwa.

    Hivi sasa, wakulima karibu milioni 2 wa mkoa wa Jilin wamejiunga na utaratibu huo mpya, na wakulima wamerudishiwa gharama za matibabu zaidi ya yuan milioni 21.

    Hivi sasa, mbali na mkoa wa Jilin, utaratibu mpya wa majaribio wa matibabu ya ushirikiano umeanzishwa kwenye wilaya zaidi ya 300 nchini China, na watu zaidi ya milioni 70 wamejiunga na utaratibu huo. Naibu waziri wa afya wa China Bw. Zhu Qingsheng alisema: "Mpaka sasa, mfumo wa usimamizi na uendeshaji wa utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano umeanza kukamilishwa, ambapo hali ya matibabu kwa wakulima imeboreshwa, na mzigo wa gharama za matibabu kwa wakulima umepungua."

    Imefahamika kuwa katika siku za usoni, China itaendelea kurekebisha na kukamilisha mpango wa majaribio ya utekelezaji wa utaratibu huo, ili wakulima wanufaike zaidi na utaratibu huo. Wakati huo huo, China itaendelea kueneza utaratibu huo, inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2010, utaratibu huo utatekelezwa kwenye vijiji vyote vya China, ambapo suala la matibabu kwa wakulima litatatuliwa kimsingi.

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-27