Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-28 17:04:38    
Maisha ya waislamu katika mtaa wa kabila la Hui wa Niujie mjini Beijing

cri

Mtaa wa Niujie uko katika sehemu ya kusini ya Beijing, tofauti na mitaa mingine mjini Beijing, kwenye mtaa huo wanaishi waislamu zaidi ya elfu kumi, na majengo na vyakula vya huko vyote vinaonesha mtindo wa kiislamu. Zamani mtaa wa Niujie ulikuwa ni njia nyembamba, kando mbili za njia kulikuwa nyumba mbovu za mawe zisizokuwa na ghorofa, na hali ya makazi ya huko ilikuwa duni sana.

Kuanzia mwaka 1997, serikali ya mji wa Beijing ilifanya ukarabati kwenye mtaa wa Niujie. Baada ya ujenzi wa miaka kadhaa, hivi sasa mtaa wa Niujie umekuwa na sura mpya kabisa wenye mtindo wa kikabila. Mkazi wa mtaa huo Bi. Qian Yanyi anasema:

"Sasa wakazi wa mtaa huo wamehamia katika nyumba mpya zilizo maridadi. Barabara ya mtaa wa Niujie imepanuliwa kuwa na mita 40 kutoka ile ya mita 7 au 8, kando mbili za barabara kuna maduka na mikahawa mingi inayouza vyakula vya kiislamu. Katika mtaa wa Niujie, kuna shule za msingi na sekondari za kabila la wahui, hospitali ya kabila la Hui na nyumba ya wazee ya kikabila inayoweza kuwapokea wazee 400. Kwa jumla mtaa wa Niujie umeweka mazingira mazuri ya kiutamaduni, kimatibabu na kimaisha kwa wakazi wa kabila dogo.

Umaarufu wa mtaa wa Niujie si kama tu unatokana na kuishi kwa idadi kubwa ya watu wa kabila la Hui, bali pia kutokana na msikiti maarufu wenye historia zaidi ya miaka 1000. Baada ya kufanyiwa ukarabati mara nyingi, msikiti wa Niujie hivi sasa umekuwa sehemu muhimu ya kufanyia shughuli za dini ya kiislamu katika sehemu ya kaskazini mwa China.

Watu wa kabila la Hui wanachukua asilimia 20 ya idadi ya watu wa mtaa wa Niujie, wengi wao ni waumini wa kiislamu, ambao wana desturi ya kuishi kwenye sehemu inayozunguka msikiti, waislamu wa mtaa wa Niujie wanashikilia desturi za jadi, wengi wao kila siku wanakwenda msikitini kuswali. Imam wa msikiti wa Niujie Bwana Yin Guofang akifahamisha kuwa:

"Msikiti wa Niujie unaendesha ibada tano kila siku, kila mara huwa na waumini takriban 100 hadi 150. Inapofika Ijumaa idadi hiyo inafika 500 hadi 800, na wakati wa kusherehekea sikukuu ya idi el fitri kunakuwa na waumini zaidi ya 2000."

Bw. Yin alisema kuwa, ofisi ya usimamizi wa mtaa wa Niujie inafuatilia sana maisha ya waislamu, kila wiki kada wa kabila la Hui Bw. Zhang Lianci anakwenda msikitini kukutana na maimamu, kuzungumza na waislamu wanaofanya ibada msikitini, na kusikiliza maoni yao kuhusu mazingira ya mtaa na shida zao za kimaisha. Anakabidhi maoni anayoyakusanya kwa wasimamizi wa mtaa ili masuala yatatuliwe katika muda mfupi.

Kwa mfano kila mara waislamu wanatakiwa kutawadha kabla ya swala, hivyo msikiti unahitaji maji mengi zaidi kuliko sehemu nyingine. Ili kurahisisha maisha ya kidini kwa waislamu, wahusika wa ofisi ya usimamizi wa mtaa huo waliwasilisha suala hilo kwa idara husika ya mji wa Beijing ili litatuliwe haraka.

Ofisi ya usimamizi wa mtaa wa Niujie pia inafuatilia sana elimu, inawapa zawadi walimu wa shule za mtaani kila ifikapo siku ya walimu, na kuwapa msaada wa fedha za masomo wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kuingia chuo kikuu. Mwaka jana, wanafunzi 54 katika mtaa wa Niujie walifaulu mtihani wa kuingia chuo kikuu. Mzee Qian Decai anayeishi kwenye mtaa huo anafurahia sana jambo hilo. Anasema:

"Zamani katika mtaa wa Niujie watu wachache sana waliweza kupata elimu ya chuo kikuu, lakini hivi sasa kusoma chuo kikuu kumekuwa jambo la kawaida. Katika jumba ninaloishi kuna wanafunzi kadhaa waliofaulu kuingia katika vyuo vikuu maarufu vya Qinghua na Beijing."

Kutokana na hali maalum ya wakazi wa mtaa wa Niujie, jinsi ya kuwaandaa makada vijana wa kabila la Hui imekuwa moja ya kazi muhimu za ofisi ya usimamizi wa mtaa huo. Kila mwaka mtaa huo huwaajiri wanafunzi wanaohitimu kutoka chuo kikuu kufanya kazi pamoja nao. Vijana hao licha ya kujifunza ujuzi kuhusu makabila madogo na dini yao, pia wanatakiwa kuwatembelea wakazi nyumbani kwao ili wafanye kazi vizuri zaidi.

Licha ya watu wa kabila la Hui, watu wa makabila mengine ya Han na Man pia wanaishi katika mtaa wa Niujie. Japokuwa imani yao ya dini na desturi zao za maisha ni tofauti, lakini wakazi wote wanaishi kwa kusikilizana na kuheshimiana.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-28