Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-29 20:31:41    
Kuzidisha ujirani mwema na ushirikiano na kuenzi Moyo wa Bandung

cri

Kuanzia tarehe 20 hadi 28 Aprili, Rais Hu Jintao wa China alifanya ziara nchini Brunei, Indonesia na Philippines, kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Asia na Afrika wa mwaka 2005 na kushiriki shughuli za kuadhimisha miaka 50 ya mkutano wa Bandung.

Waziri wa mambo ya nje Bwana Li Zhaoxing aliyefuatana na rais Hu katika ziara hiyo alisema kuwa, ziara hiyo ya rais Hu Jintao imeonesha umaalum wa aina nne.

Kwanza, ziara hiyo imeimarisha urafiki wa jadi na kufungua ukurasa mpya wa ujirani mwema.

Mawasiliano kati ya China na nchi za Brunei, Indonesia na Philippines yamekuwa na historia ndefu ya zaidi ya miaka elfu moja, hivi sasa nchi hizo tatu zinakabiliwa na jukumu la pamoja ya maendeleo. Katika ziara yake hiyo, viongozi wa pande mbili mbili wamepata maoni ya pamoja kuhusu kuendeleza uhusiano wa pande mbili mbili.

Rais Hu Jintao aliwapa pole tena wananchi wa Indonesia waliokumbwa na maafa kutokana na tetemeko la ardhi kwenye bahari ya Hindi, na ndege maalum aliyopanda rais Hu ilichukua vifaa vya misaada vya tani 50 vilivyopelekwa kwa wananchi wa Indonesia waliokumbwa na maafa, ambavyo vimeonesha urafiki mkubwa wa wananchi wa China kwa wananchi wa Indonesia, na vimesifiwa sana na serikali ya Indonesia na wananchi wake.

Pili, ziara hiyo imezidisha ushirikiano wa kunufaishana na kusukuma mbele maendeleo kwa pamoja.

Katika ziara hiyo katika nchi hizo tatu, yalisainiwa makubaliano 30 ya ushirikiano yanayohusu sekta za siasa, uchumi na biashara, usalama, sayansi na teknolojia, utamaduni, afya na nyiginezo. Urafiki na ushirikiano huo wa kunufaishana hakika utatia nguvu mpya kwenye uhusiano kati ya China na nchi hizo tatu, ambao umewanufaisha wananchi na kuhimiza maendeleo ya nchi hizo.

Tatu, ziara hiyo imesukuma mbele ushirikiano wa kikanda na kuhimiza amani na utulivu.

Nchi za Brunei, Indonesia na Philippines zote ni nchi wanachama wa Umoja wa Asia ya kusini mashariki. Rais Hu Jintao amesisitiza kuwa, China inapenda kuimarisha ujirani mwema, urafiki na ushirikiano kati ya China na nchi mbalimbali za Umoja wa Asia kusini mashariki, kutimiza maendeleo na usitawi kwa pamoja, na kupanua mawasiliano na ushirikiano katika mambo ya kimataifa na kikanda. Viongozi wa nchi tatu Brunei, Indonesia na Philippines walisifu sana umuhimu wa kiujenzi wa China katika kanda hiyo, na wameahidi kushirikiana na China katika kujenga siku nzuri zaidi za usoni za kanda hiyo.

Nne, ziara hiyo imeenzi Moyo wa Bandung na kuhimiza kushirikiana pamoja kujenga siku za usoni.

Mkutano wa Asia na Afrika uliofanyika miaka 50 iliyopita ulikuwa mnara katika harakati za ukombozi wa kitaifa za Asia na Afrika na kuleta athari kubwa nzuri kwa maendeleo ya uhusiano wa kimataifa. Hivi leo viongozi wa nchi 89 wamekutana pamoja kujadili uhusiano wa Asia na Afrika katika hali mpya, mkutano huo ulitoa Taarifa kuhusu uhusiano mpya wa kiwenzi na kimkakati kati ya Asia na Afrika.

Kwenye mkutano huo Rais Hu Jintao alifafanua maoni na mapendekezo ya China kuhusu kuanzisha na kujenga uhusiano mpya wa kiwenzi na kimkakati kati ya Asia na Afrika, ili kusaidiana, kunufaisha, kujipatia maendeleo kwa pamoja, na kukabiliana na changamoto za utandawazi wa uchumi duniani, mapendekezo yake yamekubaliwa na washiriki wa mkutano kutoka nchi nyingi.

Bwana Li Zhaoxing alisema kuwa, ziara hiyo ya rais Hu Jintao imepata mafanikio dhahiri na kutimiza lengo la kuzidisha urafiki, kuhimiza ushirikiano, kuimarisha mshikamano na kupata maendeleo kwa pamoja.

Idhaa ya kiswahili 2005-04-29