Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-29 20:26:48    
Opera ya Kibeijing Siyo "Sanaa ya Machwea"

cri

Opera ya Kibeijing yenye historia ya zaidi ya miaka 150, inapendwa sana na mashabiki wake. Kwa kuwa ina usanii wa kiwango cha juu, na inachezwa kote nchini, inachukua nafasi ya kwanza miongoni mwa aina 300 za opera ya China, ndiyo maana imepewa hadhi ya "Opera ya Taifa".

Kwa miaka mingi sasa, watazamaji wa opera ya Kibeijing wamekuwa wakipungua. Baadhi ya watu wanadhani kwamba japo opera hiyo ni nzuri, lakini sasa inakabiliwa na changamoto na kugeuka kuwa "sanaa ya machwea". Baada ya kuingia miaka ya 1990, idara za utamaduni za serikali za mitaa ambazo ziliongozwa na Wizara ya Utamaduni, zilifanya bidii na kuchukua hatua nyingi za kuistawisha Opera ya Kibeijing. Bidii kubwa ilikuwa ni kufanya maadhimisho ya miaka 200 tangu Opera ya Kianhui iingie kutumbuiza Beijing. Opera ya Kianhui ni chimbuko la Opera ya Kibeijing.

Ufumbuzi wa kustawisha Opera ya Kibeijing ni kuwavutia watazamaji vijana na kuwafundisha wachezaji vijana. Jumba la Opera ya Kibeijing la Shanghai lilijitokeza bure jijini Beijing, likitaka kuifanya "Opera ya Kibeijing Kuwalenga Vijana". Mchezo wa kwanza ulikuwa ni "Caocao na Yangxiu" ambao ulijinyakulia tuzo ya Dhahabu katika Tamasha la Kwanza la Opera ya Kibeijing. Watazamaji walijaa, mchezo wenyewe ulifanyika kwa saa mbili na kupongezwa kwa makofi zaidi ya mara 20. Hali hii inadhihirisha kuwa vijana nao pia wanaipenda Opera ua Kibeijing. Baada ya mchezo kumalizika, Shang Changrong, msanii mzee maarufu akiwa analengwalengwa na machozi, alishuka kutoka jukwaani, akapeana mikono na vijana na kuweka saini yake.

Hivi leo, Jumba la Opera ya Kibeijing la China, Jumba la Opera ya Kibeijing la Beijing, Jumba la Opera ya Kibeijing la Tianjin na Jumba la Opera ya Kibeijing la Shanghai yameanzisha vikundi vya Opera ya Kibeijing vya vijana. Zaidi ya hayo, vikundi vyingi vya Opera ya Kibeijing pia vimeanzisha vikundi vya vijana. Vikundi hivi vya vijana vinaonesha michezo mingi mizuri, wachezaji wake kadhaa wamepata maendeleo na kuwa na kiwango cha juu cha usanii. Bi. Shi Min mwenye umri wa miaka 22 alipata tuzo ya Plum, tuzo ya juu kabisa ya opera na tamthilia nchini China. Sasa, yeye ni uti wa mgongo wa Jumba la Opera ya Kibeijing mjini Shanghai.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-29