Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-29 20:33:44    
Maonesho ya sanaa za uchongaji ya Zimbabwe

cri

Maonesho ya Sanaa za uchongaji wa mawe za Zimbabwe yalifanyika kuanzia tarehe 9 hadi 24, Aprili kwenye Duka la Sanaa la Afrika lililoko kwenye kituo cha maduka cha Jinyuan ("Golden Resources Shopping Mall") hapa Beijing. Tarehe 20, mwandishi wetu wa habari alitembelea maonesho hayo kwenye kituo hicho, ambacho ni kituo kikubwa zaidi cha maduka nchini China. Katika kipindi cha leo, tunawaletea maelezo kuhusu hali halisi ya maonesho hayo.

Katika miaka ya hivi karibuni, maonesho mengi ya sanaa za Afrika yamekuwa yakifanyika katika miji mikubwa ya China ikiwemo Beijing na Shenzhen, na aina mbalimbali za sanaa zenye mtindo wa kiafrika zinazoonesha mawazo maalum ya ubunifu waliyo nayo wasanii wa Afrika, zinawapendeza sana watu wa China. Maonesho hayo ya sanaa za uchongaji ya Zimbabwe, yaliyofanyika hivi karibuni yamewaletea wakazi wa Beijing aina mpya ya sanaa kutoka Afrika.

Mwendeshaji wa Maonesho ya Uchongaji wa mawe ya Zimbabwe Bw. Guan Shucheng anaona kuwa, kadiri kiwango cha maisha ya watu kinavyoinuka, ndivyo wachina wanavyokuwa na mahitaji makubwa zaidi ya utamaduni na sanaa. Wachina wameanza kujitafutia vitu vilivyotofautiana na vya wengine, na mambo ya kimaumbile. Kutokana na umbali mkubwa kati ya China na Bara la Afrika, utamaduni wa mtindo pekee na sanaa zenye mvuto mkubwa za Afrika ni kitu kigeni kwa wachina, na zinawavutia sana wachina. Bw. Guan Shucheng alisema maonesho hayo yametoa fursa nzuri katika kujulisha utamaduni wa Afrika kwa wachina. Bw. Guan anasema:

"Tunataka kuwaoneshea wachina sanaa na utamaduni wa Afrika, na kuzidisha maelewano na mawasiliano ya utamaduni kati ya pande hizo mbili."

Bw. Guan amesema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, wachina wanapendelea mambo ya kimaumbile, wakati huo huo, nchi nyingi zaidi za Afrika zimeanza kuwapokea watalii wa China kutokana na kukuzwa kwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili, na wachina wengi wameanza kulifahamu zaidi bara la Afrika na kutaka kufanya utalii barani Afrika. Bw. Guan anataka maonesho hayo yawe kuwa daraja la kukuza mawasiliano ya utamaduni kati ya watu wa China na Afrika.

Maana ya jina la Zimbabwe ni Mji wa Mawe kwa lugha ya kienyeji, na nchi hiyo inajulikana duniani kutokana na uchongaji wake wa mawe wenye mtindo maalum. Kijiji cha Tangananga ni chimbuko la uchongaji wa mawe wa Zimbabwe, pia ni kituo kikubwa zaidi cha uchongaji wa mawe barani Afrika. Michongo mingi iliyooneshwa kwenye maonesho hayo ya Zimbabwe ilichaguliwa kwenye kituo hicho.

Mkuu wa Duka la sanaa la Afrika bibi Hao Yanhua alimwambia mwandishi wa habari kuwa, wachongaji wote hawajifunzi uchongaji shuleni, hivyo michongo yao inatokana na ubunifu wao wenyewe. Bibi Hao anasema:

"Uchongaji wa mawe wa Zimbabwe unaonesha miungu na vitu vinavyoabudiwa, baadhi ya wakati wachongaji wanapata mawazo kutokana na hali ya maisha. Wachongaji wenyeji wa Zimbabwe wanaheshimu sana mawe watakayoyatumia katika uchongaji, wanaona kuwa mawe pia yana uhai, na inapaswa kuchonga kwa kufuata maumbo yake ya asili."

Bibi Hao alieleza kuwa, uchongaji wa Zimbabwe unafanyika kwa aina nne za mawe zikiwemo: Green Serpentine, Springstone, Black Soapstone na Opal Stone, mawe hayo yenye sifa ya juu, ni mali kubwa kwa wachongaji wa huko.

Kwenye maonesho hayo, mwandishi wa habari aliona kuwa, kati ya michongo mbalimbali, kuna sanamu za binadamu na michongo ya wanyama zinazoonekana kama zenye uhai, pia kuna michongo inayoonesha tu mawazo ya wachongaji isiyofanana na vitu halisi.

Michongo hiyo yenye mitindo maalum inawavutia wateja wengi walionunua vitu madukani, na watazamaji waliotembelea kuangalia maonesho hayo. Bw. Zhang ni mhariri wa kituo cha televishani hapa Beijing, alimwambia mwandishi wa habari kuwa, anapenda sana sanaa za Afrika, kama vile vinyago vya Tanzania na anavutiwa sana na vinyago vya twiga. Akiwa mhariri wa televisheni anataka kuandaa kipindi cha televisheni kuhusu maonesho hayo. Baada ya kuona maonesho hayo, ana matumaini makubwa ya kwenda Afrika kujionea mandhari ya huko.

Mbali na watu wa kawaida, mwandishi wetu wa habari pia alikuta wajemadari wazee kutoka "Shirikisho la wasanii wa maandiko na uchoraji wa Jenerali" ambao walitembelea maonesho hayo. Jenerali Huang Wanrong ni mkuu wa shirikisho hilo. Baada ya kutazama maonesho hayo alisema kwa furaha:

"Zimbabwe ni nchi yenye historia ndefu ya utamaduni, na inajulikana sana katika sanaa ya uchongaji wa mawe." Maonesho hayo ya uchongaji wa mawe yanaunganisha vizuri binadamu na mambo ya kimaumbile, mawazo ya watu na vitu halisi. Bw. Huang alisema kuwa, sanaa ya uchongaji wa mawe ya China inaonesha zaidi mtindo wa jadi, na sanaa za Afrika zinaonesha hali ya zama za hivi leo. Pande hizo mbili zinaweza kufanya mawasiliano mazuri, ili kufundishana."

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-29