Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-02 18:36:12    
ECOWAS washindwa kwa muda katika kusuluhisha mgogoro wa kisiasa nchini Togo

cri

Ofisa wa Umoja wa ECOWAS tarehe 1 Mei alithibitisha kuwa, Shirikisho la vyama vya upinzani la Togo siku hiyo lilikataa pendekezo lililotolewa na ECOWAS kuhusu chama tawala na vyama vya upinzani kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hivyo ECOWAS imeshindwa kwa muda katika kusuluhisha mgogoro wa kisiasa nchini Togo.

Mgogoro huo wa kisiasa wa Togo ulisababishwa na migongano kuhusu uchaguzi wa rais. Kamati ya uchaguzi ya nchi nzima ya Togo tarehe 26 ilitangaza kuwa, matokeo ya hesabu za kura za hatua ya mwanzo yameonesha kuwa, mtoto wa rais wa zamani Eyadema Bwana Faure alipata ushindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 24. Baada ya kujulikana kwa matokeo hayo, waungaji mkono wa shirikisho la vyama vya upinzani walifanya fujo katika sehemu kadhaa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 10 na wengine zaidi ya mia moja kujeruhiwa. Fujo hizo pia ziliwafanya wakimbizi wa Togo zaidi ya elfu 10 na wageni walioishi nchini humo kukimbilia nchi jirani Benin na Ghana. Baadaye mgombea wa urais wa shirikisho la vyama vya upinzani Emmanuel Bob Akitani alitangaza kuwa ameshinda katika uchaguzi na kujiita kuwa ni rais.

Ili kuondoa mgogoro huo wa kisiasa, ujumbe wa ECOWAS ulioongozwa na katibu mkuu mtendaji wake Mohamed Ibn Chambas tarehe 30 Aprili ulifika Lome, mji mkuu wa Togo kufanya usuluhishi. Ujumbe huo kwa nyakati tofauti ulikutana na rais wa muda wa Togo Abass Bonfoh, waziri mkuu Kofi Sama pamoja na mwenyekiti wa chama tawala cha Shirikisho la umma la Togo ambaye pia ni mgombea wa urais wa chama hicho Bwana Faure na wawakilishi wa shirikisho la vyama vya upinzani.

Katika mazungumzo hayo, Bwana Chambas alisisitiza msimamo wa ECOWAS wa kuunga mkono vyama mbalimbali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, na kuvisihi tena vyama hivyo na waungaji mkono wao wajizuie, kulinda utulivu wa nchini humo na kuacha mara moja vitendo vyovyote ya kimabavu. Bwana Bonfoh na Bwana Faure walieleza kuwa, serikali ya Togo na chama tawala vinakubali kabisa maoni ya ECOWAS kuhusu kuunda serikali ya umoja, na kukaribisha shirikisho la vyama vya upinzani kujiunga na serikali ya umoja, lakini shirikisho la vyama vya upinzani linashikilia maoni yake tofauti, wawakilishi wake walisema kuwa, hawataweza kufanya hivyo kabla ya kutatuliwa kwa mgogoro wa uchaguzi wa rais, tena walidai ufutwe uchaguzi uliofanyika, ama kuhesabu upya kura zilizopigwa.

Baada ya uchaguzi wa Togo uanzishwe, jumuia ya kimatafia ilisifu utaratibu na matokeo ya uchaguzi huo. Matokeo ya uchaguzi huo yalipojulikana, ECOWAS iliyosimamia uchaguzi huo ulisema mara moja kuwa, utaratibu wa uchaguzi mzima kijumla ulilingana na kigezo cha kimataifa, vyama mbalimbali vinapaswa kuheshimu matokeo ya uchaguzi.

Wakati huo huo ingawa Umoja wa Ulaya na Marekani zilikuwa na mashaka kuhusu hali ya haki ya uchaguzi huo, lakini hazikutoa maoni yao tofauti, bali zilivitaka vyama mbalimbali vya Togo viunde serikali ya shirikisho ili kulinda amani na utulivu nchini humo. Na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Nigeria Olusengun Obasanjo alisisitiza kuwa Umoja wa ECOWAS, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa una madaraka ya kuweka vikwazo kwa upande wowote unaoharibu makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Hivi sasa jumuia ya kimataifa imelaani vikali vitendo vya waungaji mkono wa vyama vya upinzani kwa kuwashambulia wakazi na wageni walioishi nchini humo kwa vurugu zao, shirikisho la vyama vya upinzani linakabiliwa na shinikizo kubwa.

Vyombo vya habari vinaona kuwa, Umoja wa ECOWAS na Umoja wa Afrika huenda utafanya tena usuluhishi ili kuvihimiza vyama mbalimbali vifikie makubaliano ya kuondoa mgogoro wa hivi sasa.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-02