Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-06 21:52:46    
Russia kuadhimisha kwa shangwe miaka 60 ya ushindi wa vita vya kulinda taifa

cri
    Huu ni mwaka wa 60 tangu ushindi upatikane katika vita vya kupambana na ufashisti duniani, na tarehe 9 Mei itakuwa siku ya maadhimisho miaka 60 ya ushindi wa vita vya kulinda taifa la Russia. Russia itafanya sherehe kubwa tarehe 9 huko Moscow, ambapo viongozi wa zaidi ya nchi 50 pamoja na Umoja wa Mataifa na jumuiya nyingine za kimataifa wakiwemo rais Hu Jintao wa China, rais Bush wa Marekani, rais Chiraq wa Ufaransa na chansela wa Ujerumani Gerhard Schroeder watashiriki kwenye sherehe hiyo kutokana na mwaliko.

    Katika majira ya joto ya mwaka 1941, wafashisti wa Ujerumani walianzisha uvamizi wa ghafla dhidi ya Urusi. Wananchi wa Urusi walifanya mapambano dhidi ya uvamizi wa wafashisti wa Ujerumani ili kulinda taifa lao. Baada ya mapambano ya kumwaga damu ya miaka minne, wanajeshi na wananchi wa Urusi walifanikiwa kulinda mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi, pia walijiunga pamoja na wananchi wa nchi mbalimbali duniani katika kutokomeza kabisa njama ovu za nguvu ya wafashisti. Usiku wa tarehe 8 Mei, 1945, yaani ilikuwa alfajili mapema ya tarehe 9 Mei ya saa za Moscow, mwakilishi wa makao makuu ya jeshi la Ujerumani alisaini taarifa ya Ujerumani ya kusalimu amri kwa Urusi, Uingereza na Marekani. Hii ilionesha kukomeshwa kwa vita vya pili vya dunia katika medani ya kivita ya Ulaya, pia ilionesha kumalizika kwa ushindi kwa vita vya Urusi vya kulinda taifa.

    Ushindi wa vita vya Urusi vya kulinda taifa ulitoa mchango mkubwa kwa ajili ya kupatikana kwa ushindi katika mapambano dhidi ya wafashisti duniani. Wakati huo huo, wananchi wa Urusi walitoa mihanga mikubwa katika vita hivyo, ambapo watu wa Urusi wapatao milioni 27 walipoteza maisha katika vita vya kulinda taifa. Katika miaka mingi iliyopita, kuadhimisha ushindi wa vita vya kulinda taifa ni shughuli kubwa zinazofanyika nchini Russia na nchi nyingine za Shirikisho la jamhuri huru. Mwaka huu ni mwaka wa 60 wa ushindi wa mapambano dhidi ya wafashisti duniani, hivyo siku ya kuadhimisha ushindi wa vita vya kulinda taifa la Russia imekuwa na umuhimu maalum, pia imekuwa tukio kubwa linalofuatiliwa na wananchi wa nchi mbalimbali duniani. Sherehe hiyo itakayofanywa na Russia imekuwa sehemu moja muhimu ya shughuli za kuadhimisha ushindi wa mapambano dhidi ya wafashisti duniani.

    Kwa mpango uliowekwa, tarehe 9 Mei, gwaride kubwa litafanyika kwenye uwanja mwekundu wa Moscow, ambapo wapiganaji wazee zaidi ya 2000 wa jeshi jekundu la Urusi ya zamani walioshiriki kwenye vita vya kulinda taifa, watashiriki kwenye gwaride hilo. Baadhi ya wapiganaji wazee miongoni mwao watatazama gwaride pamoja na viongozi kutoka nchi mbalimbali, na wengine watapanda magari mbalimbali yaliyoundwa kwa kufuata aina mbalimbali za magari ya zamani wakikakaguliwa; baadaye viongozi watakaoshiriki shughuli hiyo, wataweka maua kwa heshima kwenye makaburi ya wapiganaji waliojitoa muhanga na kupigwa picha pamoja; hatimaye rais Putin na mkewe wataandaa tafrija kuwakirimu viongozi wa nchi mbalimbali na wake zao watakaoshiriki kwenye shughuli ya maadhimisho hayo.

    Watu watakaoshiriki shughuli za kuadhimisha ushindi wa vita vya kulinda taifa la Urusi huko Moscow wanatazamiwa kufikia milioni 7, hata waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali duniani watafikia 3000. Ofisa mmoja wa serikali ya Moscow ameeleza imani yake kubwa kuwa, sherehe ya kuadhimisha miaka 60 ya ushindi wa vita vya kulinda taifa itakuwa mkutano mkubwa wa amani, na shughuli mbalimbali zitakazofanyika kwenye sherehe hiyo zitafanikiwa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-05-06