Tarehe 8 mwezi Mei mwaka 1945, Wanazi wa Ujerumani walisalimu amri kwa majeshi ya muungano. Tukio hilo liliashiria kumalizika rasmi kwa vita vya pili vya dunia katika medani ya Ulaya. Siku hiyo baada ya miaka 60, nchi mbalimbali za Ulaya zilifanya sherehe kubwa kuomboleza vifo vya makamanda na askari wa majeshi ya muungano walijiotoa mhanga na raia waliokufa katika vita hivyo.
Tarehe 8, Uholanzi ilifanya shughuli za kumbukumbu katika makaburi ya wanajeshi wa Marekani ya Margraten, mashariki ya mji maarufu Maastricht ambazo ziliwashirikisha Rais George Bush wa Marekani, malkia wa Uholanzi, askari wazee zaidi ya 100 kutoka nchini Marekani na Uholanzi walioshiriki kwenye vita ya pili ya dunia na watu wa nyanja mbalimbali. Kwenye makaburi hayo, wamezikwa askari 8300 wa Marekani waliojitoa mhanga katika vita hiyo.
Rais George Bush alipohutubia sherehe hiyo alisema kuwa makaburi hayo yapatayo elfu hivi yanaeleza kuwa Marekani ilitoa malipo makubwa ya huzuni kwa uhuru wa Ulaya, na Marekani inatumai kuwa itaendelea kushirikiana na nchi za Ulaya katika kuhimiza uhuru. Waziri mkuu wa Uholanzi Bw. Jan Balkenende katika hotuba yake alitoa heshima kwa askari wa jeshi la Marekani waliojitoa mhanga katika vita hivyo.
Siku hiyo, Ufaransa iliadhimisha kwa shangwe siku ya ushindi wa medani ya Ulaya mbele ya upinde wa Triumphal mjini Paris. Rais Jaques Chirac wa Ufaransa aliendesha mwenyewe sherehe hiyo na kukagua gwaride ya jeshi la Ufaransa. Pia aliweka shada la maua mbele ya kaburi la askari wasiojulikana waliojitoa mhanga katika vita ya pili ya dunia.
Siku hiyo, Uingereza pia ilifanya maadhimisho mbalimbali. Prince Charles wa Uingereza aliweka shada la maua mbele ya mnara wa kumbukumbu wa makamanda na askari walijitoa mhanga katika vita hivyo ulioko mjini London. Wanajeshi wastaafu na wasiostaafu wapatao elfu nne na jamaa zao walishiriki kwenye maadhimisho hayo.
Tarehe 8, Ujerumani ilifanya maadhimisho mjini Berlin. Rais Horst Koehler wa Ujerumani, chansela Gerhard Schroeder na spika Wolfgang Thierse waliweka mashada ya maua kuwakumbuka watu waliokufa katika vita hivyo katika jumba la makumbusho la watu waliokufa katika vita hiyo. Rais Koehler alieleza kuwa Wajerumani wana wajibu kukumbuka barabara mateso yote na vyanzo vilivyosababisha mateso hayo na kukataa kurudisha mateso hayo.
Wakati nchi mbalimbali za Ulaya zilipoadhimisha ushindi wa vita vya pili vya dunia, idadi ndogo ya Wanazi mamboleo nchini Ujerumani walipiga makelele yanayopingana na maadhimisho hayo na kutia wingu jeusi kwenye maadhimisho hayo. Mjini Berlin, Wanazi mamboleo wapatao 3300 waliandamana katika uwanja wa Alexander mjini Berlin na kukamatwa na polisi. Tukio hilo linawaonya watu kuwa muzimu wa unazi mamboleo haujaondolewa barani Ulaya na watu lazima wawe macho.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-09
|